Nenda kwa yaliyomo

Raila Odinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Raila Amollo Odinga)
Raila Amolo Odinga

Raila Odinga (alizaliwa 7 Januari 1945) ni mwanasiasa kutoka Kenya aliyehudumu kama Waziri mkuu kutoka mwaka wa 2008 hadi 2013. Anadhaniwa kuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya kuanzia 2013 kwani katiba mpya ya Kenya haina nafasi hii.

Alikuwa mbunge wa Langata kuanzia 1992 hadi 2007. Raila Odinga alihudumu kwenye baraza la mawaziri la Kenya kama waziri wa nishati kuanzia 2001 hadi 2002, na baadaye kama waziri wa barabara, kazi ya umma na makazi kuanzia 2003 hadi 2005. Odinga aliteuliwa kuwa mwakilishi wa juu wa maendeleo ya miundombinu katika Umoja wa Afrika mwaka wa 2018.

Ajulikana kote Kenya kwa jina lake la kwanza Raila, Rao au Baba. Watu wanaotoka kwenye kabila lake la waluo hupenda kumwita Agwambo, Tinga au Nyundo.

Utoto na familia

Alizaliwa 1945 katika familia ya Waluo akiwa mtoto wa chifu Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza nchini Kenya. Baba yake alikuwa kiongozi mkuu wa Waluo akatazamiwa baadaye kama mpinzani mkuu wa rais wa kwanza Jomo Kenyatta.

Kaka yake Raila, Oburu Odinga amekuwa mwanasiasa na mbunge vilevile ambapo sasa ni mbunge wa EALA.

Raila amemwoa Ida Betty Odinga na wana watoto wanne: Fidel, Rosemary, Raila jr. na Winnie.

Elimu na kazi

Raila baada ya kumaliza shule nchini Kenya alikwenda kusoma uhandisi katika Chuo cha Ufundi Magdeburg (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani) kati ya 1965 hadi 1970. Alipata digrii ya MSc kama mhandisi. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama mwalimu hadi 1974 alipokuwa naibu mkurugenzi katika Shirika la Viwango Kenya (Kenya Bureau of Standards).

Odinga mwaka 2008.

Raila alianzisha makampuni kadhaa kama vile Applied Engineering Services na Pan African Petroleum Limited. Ameendelea kuendesha kampuni ya familia ya Spectre International Limited inayoshika 40% za hisa za kiwanda cha ethanol cha Kisumu na East African Spectre inayotengeneza chupa za gesi ya kupikia. Mwaka 2007 alikadiriwa kuwa na mali yenye thamani ya takriban bilioni 4 za shilingi za Kenya.

Raila anajulikana kama mpenzi wa mpira wa miguu aliyeshiriki mara nyingi katika timu ya Bunge la Kenya. Anapenda kutazama michezo uwanjani. Katika hotuba zake alichukua mara nyingi nafasi ya mtangazaji wa redio akilinganisha siasa na mchezo wa mpira.

Maisha ya siasa

Raila alionekana katika siasa mara ya kwanza baada ya jaribio la [[Mapinduzi ya kijeshi ya 1982 nchini Kenya]]. Raila asiyewahi kuwa mwanajeshi alishtakiwa kushiriki katika mipango hii akakamatwa akafungwa katika nyumba yake kwa miezi sita na kutupwa jela bila hukumu jumla miaka nane kati ya 1982-1988, 1988-1989 na 1990-1991. Wakati ule alikanusha mashtaki lakini kutokana tawasifu iliyotolewa mwaka 2006 imeonekana ya kwamba alikuwa na habari kuhusu mipango ya mapinduzi.

Mwaka 1991 Raila aliondoka Kenya kukimbilia Norwei akihofia maisha yake. Baada ya serikali ya Moi kubadilisha katiba na kuruhusu vyama vya upinzani akarudi na kujiunga na chama cha FORD (Forum for the Restauration of Democracy) kilichoongozwa na babake. Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi akachaguliwa kama mbunge wa jimbo la Lagata mjini Nairobi.

Katika mafarakano ya FORD aliendelea upande wa babake katika Ford-Kenya. Baada ya kifo cha baba akagombea uongozi wa FORD-Kenya akashindwa na Michael Wamalwa akaondoka na kujiunga na chama kidogo cha National Development Party NDP akifuatwa na wabunge wengi wa chama kutoka eneo la Waluo.

Kukaribia serikali na muungano na KANU

Katika uchaguzi wa 1997 alimaliza nafasi ya tatu kaa mgombea wa rais baada ya Moi na Mwai Kibaki. Akaingia katika bunge kati ya vyama vya upinzani lakini akaanza kujenga maelewano na Moi na chama cha KANU. Wapinzani wake Raila walisema ya kwamba shabaha zake za kiuchumi zilikuwa sababu muhimu katika badiliko wakidai ya kwamba biashara za Raila zilisogea mbele wakati ule wa ushirioano na Moi. Watetezi wake walisema ya kwamba aliona upinzani ulikuwa umegawnyika mno akaona njia ya pekee ya kubadilisha hali ya nchi ilikuwa ushirikiano na KANU.

2001 Raila alikuwa watiri wa nishati katika serikai ya Moi akaendelea kuunganisha chama chake cha NDP na KANU akawa katibu mkuu wa chama kipya cha muungano katika mkutano ulioendeshwa dhidi ya sehemu wa viongozi wa zamani za KANU.

Farakano katika KANU na kuanzishwa kwa Rainbow NARC

Kabla ya uchaguzi wa 2002 farakano likaonekana. Inawezekana Raila alitegemea kupata nafasi ya kuwa mgombea wa urais wa KANU Mpya baada ya Moi lakini rais alianza kutangaza ya kwamba chaguo lake lilikuwa Uhuru Kenyatta. Kwenye mkutano ulionthebitisha Kenyatta kulingana na mapenzi ya Moi Raila pamoja na sehemu ya viongozi wa KANU waliondoka na kujiunga na upinzani uliowahi kuunga mkono chini ya bendera ya National Alliance of Kenya (NAK).

Raila pamoja na sehemu ya viongozi wa KANU hasa Kalonzo Musyoka, George Saitoti, Joseph Kamotho waliopinga upendeleo wa Moi kwa Uhuru Kenyatta waliondoka katika chama wakatangaza kuundwa kwa harakati ya upinde wa mvua (Rainbow Movement). Walitumia chama kidogo cha Liberal Democratic Party (LDP) kama chombo cha kisheria kwa umoja wao mpya. Rainbow waliingia mara moja katika majadiliano na NAK iliyokuwa muungano wa vyama vya upinzani wakaunda umoja mpya wa NARC (National Rainbow Coalition).

Katika NARC Raila akasimama upande wa mgombea wa urais Mwai Kibaki. Katika kipindi hiki Raila aliendelea kuwa kiongozi wa kitaifa akitanganza "Kibaki tosha" kwa maana ya kwamba aliona Kibaki alifaa kuwa rais mpya na yeye kama Mluo aliunga mkono na mgombea Mkikuyu yaani Kibaki.

Msingi wa ushirikiano ulikuwa mapatano kati ya pande za NARC yaliyoitwa "Memorandum of Understanding" (MoU). Hapo walipatana ya kuwa:

  • Kibaki atakuwa rais
  • LDP itapewa nusu ya mawaziri katika serikali
  • katika muda siku 100 katiba itabadilishwa itakayopunguza madaraka ya rais
  • sehemu ya madaraka ya rais zitakabishiwa kwa cheo kipya cha waziri mkuu
  • Raila atakuwa waziri mkuu wa NARC.

Ushindi wa NARC na mafarakano katika serikali mpya

NARC ikashinda uchaguzi na Kibaki akawa rais mpya. Raila akaingia katika serikali kama waziri wa barabara. Lakini Kibaki hakutimiza MoU. LDP haikupata nusu ya mawaziri. Mkutano wa kusahihisha katiba ulikwamishwa na na mapendekezo ya mkutano wa kutunga katiba mpya katika Bomas of Kenya hayakutekelezwa. Cheo cha waziri mkuu haukuanzishwa.

Katika miaka iliyofuata farakano ilikua. Mwaka 2005 upande wa rais Kibaki ulijaribu kuanzisha katiba mpya usiokuwa na mabadiliko mengi kuhusu madaraka ya rais. Cheo kipya cha waziri mkuu kikapangwa kuwa na madaraka machache. Vilevile ugatuzi wa madaraka hayakuonekana jinsi ilivyowahi kukubaliwa katika mkutano wa Bomas of Kenya. Katiba hii ilitakiwa kukubaliwa na wananchi wote. Kempeni ya kura hii ikagawa taifa hata mawaziri wa serikali walionekana pande zote mbili. Watetezi wa katiba iliyopendekezwa walitumia ishara ya ndizi na wapinzani walitumia ishara ya chungwa. Raila pamoja na chama cha KANU kilichokuwa chama cha upinzani tangu 2002 wakafaulu kuzuia katiba katika kura ya wananchi wote. Kibaki akajibu kwa kuachisha mawaziri wote pamoja na Raila na kutomwita tena katika serikali mpya.

Sasa Raila pamoja na Uhuru wa KANU waliunda harakati mpya ya ODM (Orange Democratic Movement) kwa kusudi la kugombea uchaguzi wa 2007.

Kiongozi wa ODM na uchaguzi 2007

Hata ODM iliona mafarakano katika maandalizi ya kumteua mgombea wa urais. Kalonzo Musyoka pamoja na wafuasi wake katika Ukambani walijiondoa Agosti 2007 wakaanzisha ODM-Kenya. Katika mkutano mkuu wa ODM Raila alipata kura nyingi kuwa mgombea wa urais. Wapinzani wake Musalia Mudavadi, William Ruto na Joseph Nyagah wakaamua kushikama naye wakabaki katika ODM. Mabaki ya KANU chini ya Uhuru Kenyatta wakajiondoa katika upinzani wakahamia upande wa rais Kibaki.

Katika kura za maoni tangu Septemba 2007 Raila alionekana mbele akielekea kuwa na nsu ya maoni yote au hata kidogo zaidi wakati rais Kibaki alifikia kiwango cha takriban 40 % pekee.

Uchaguzi wenyewe ulikuwa na matatizo kwa sababu matokeo ya kwanza yalimwonyesha Raila kuwa na kura nyingi lakini Tume la Uchaguzi lilisimamisha matangazo ya matokeo ghafla. Matangazo yaliyofuata baada ya siku mbili ghafla yalimwonyesha Rais Kibaki kuwa na kura nyingi akaapishwa haraka bila kusubiri muda wa kisheria kwa malalamiko. Odinga alitangazwa na ODM kama mshindi wa kweli na farakano hili lilisababisha ghasia kali sana zilizoendelea kukaribia hali ya vita ya wenyewe kwa wenyewe. Watu wengi walifukuzwa katika maeneo hasa ya Bonde la Ufa na pia katika mitaa ya vibanda kwenye miji mbalimbali kufuatana na kabila yao. Baada ya vifo ya watu maelfu na kuporomoka kwa uchumi nchini majadiliano kati ya pande zote mbili chini ya Kofi Annan yalileta maelewano juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na Kibaki kama rais na Raila kama waziri mkuu.

Kinara wa azimio la Umoja

Raila Odinga [1] mwaka wa 2022 ameteuliwa kuwania urais mara ya tano kwa tiketi ya Azimio la Umoja.

Tanbihi

  1. Davis Ayega (2022-03-12). "Uhuru to grace Raila's crowning as Azimio flagbearer at KICC » Capital News". Capital News (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2022-03-27.

Viungo ya nje