Nenda kwa yaliyomo

Orientalium Ecclesiarum

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mtaguso wa pili wa Vatikano ulizingatia hali duni ya Makanisa Katoliki ya Mashariki ukaamua kuiboresha.

Ndiyo sababu tarehe 21 Novemba 1964 ulitoa hati maalumu kwa kura 2110 dhidi ya 39. Jina lake kwa Kilatini ni "Orientalium Ecclesiarum" (maana yake, "Ya Makanisa ya Mashariki").

Kwanza ulitamka kuwa hayo yanastahili kuheshimiwa sana pamoja na mambo yao yote (liturujia, teolojia, sheria za Kanisa, miundo n.k.) kama sehemu ya hazina ya Kimungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa.

Liturujia zao ziliagizwa zitunzwe kiaminifu na kurekebishwa kama zimeachana na mapokeo ya Mashariki; hasa sakramenti zirudi kufuata taratibu asili.

Mashirika ya kitawa ya Kilatini yajitahidi kuanzisha jumuia za Mashariki.

Hati inatamka wazi kwa mara ya kwanza kuwa madhehebu yote ya Kikatoliki (yaani ya mashariki na ya magharibi) yana haki na wajibu sawa hata kuhusu uenezaji Injili duniani kote.

Wachungaji wa hayo yote wazoee kushirikiana, na wanaojiandaa kupata upadri waelimishwe juu ya uhusiano kati ya madhehebu hayo mbalimbali ya Kanisa moja.

Waamini wa Mashariki wapatiwe mapadri na maaskofu wao popote wanapohitaji.

Waortodoksi wakijiunga na Kanisa Katoliki waendelee kufuata madhehebu yao, na wenye daraja kati yao waendelee kuitumia.

Kutokana na umuhimu wa patriarki kwao, hadhi na haki zake zirudishwe kama zilivyokuwa kabla ya utengano na Waortodoksi, na Makanisa yasiyo naye yafikiriwe.

Hatimaye hati hiyo inahimiza Wakatoliki wa Mashariki kushughulikia ekumeni hasa upande wa Waortodoksi, ikiruhusu kutoleana nao sakramenti kadhaa na mengineyo.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]