Mathias E. Mnyampala

Mathias E. Mnyampala (18 Novemba 1917 – 8 Juni 1969) alikuwa mwanasheria, mwandishi na mshairi maarufu kutoka nchini Tanzania.
Mathias E. Mnyampala alizaliwa tarehe 18 Novemba 1917 katika kijiji cha Ihumwa (Muntundya Ihumwa), Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, na alifariki dunia tarehe 8 Juni 1969 mjini Dodoma. Pia, zaidi ya kujulikana kama mwandishi, alikuwa mzalendo shupavu katika harakati za ukombozi kupitia chama cha TANU, akiwa pia Mkristo mtiifu wa Kanisa Katoliki aliyelitumikia kwa bidii.
Machapisho yake ya kwanza yalitokea wakati wa enzi ya ukoloni, yakiwemo kitabu cha historia ya Wagogo wa Tanganyika kilichoandikwa kwa Kiswahili (Mathias Mnyampala, 1954) pamoja na vitabu vya hadithi. Mnyampala hakuchagua lugha yake ya kiasili, Kigogo, kama lugha ya uandishi, bali alipendelea kutumia Kiswahili katika kazi zake zote za fasihi. Alitunga mashairi mengi ya Kiswahili yaliyochapishwa kwenye magazeti ya kipindi hicho. Mnyampala aliandika zaidi ya vitabu 25.
Mwandishi huyu alikuwa wa kabila la Wagogo kwa upande wa mama na baba yake. Alizaliwa katika kitongoji cha Muntundya huko Ihumwa, kijiji kilichoko Ugogo vijijini, takriban kilomita 22 kutoka Dodoma. Ingawa baadhi ya nyaraka, zikiwemo za kiofisi, hutaja mwaka 1919 kama mwaka wake wa kuzaliwa, jambo hilo halijathibitishwa na tawasifu yake, Maisha ni Kugharimia[1] (iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2013 kulingana na mswada wake wa mwaka 1968-1969), ambamo anataja mwaka 1917. Vilevile, hati ya kikoloni ya mwaka 1956 inayoeleza taarifa zake kamili za kiraia inathibitisha tarehe hiyo ya 1917[2]. Wakati huo wa utoto, herufi ya E. katika orodha ya majina yake, ambayo tunaijua kupitia barua za baadaye kuwa ni jina la Kikristo la Eugen, ilitokana na jina la Kigogo: Emnzehe.[3] Baba yake alikuwa mhunzi, hali iliyomhakikishia ukwasi fulani na umiliki wa mifugo. Ilikuwa ni maisha ya kijijini yasiyokosa changamoto za maradhi. Kwa mujibu wa tawasifu, alinusurika kifo mnamo mwaka wa 1926 akiwa na umri wa miaka 9, akapona shukrani kwa msaada wa mganga Ngalya na kwa msaada wa Mungu: « Namkumbuka mganga mmoja jina lake Ngalya [...] aliyesaidiwa na Mungu [...] nikapona kabisa ».[1] Mnyampala alijifunza kuandika Kiswahili katika misheni ya Kikristo akiwa tayari ameshaoa[1] , na hata hivyo, akaja kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri wa Kiswahili katika karne ya ishirini. Hii ni safari ya kipekee na ya kustaajabisha iliyomgeuza mwanafunzi wa ukubwani kuwa malenga wa fasihi na ushairi wa Kiswahili. Mathias E. Mnyampala alibaki kuwa Mkristo mkatoliki tangu alipoongoka kipindi hicho.
Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, alishuhudia uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 1961, na baadaye muungano wa taifa hilo huru na visiwa vya Zanzibar tarehe 26 Aprili 1964 kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka wa 1969 alishikwa na maradhi makali na kuhisi kuwa mwisho wake unakaribia, kama anavyoeleza kwenye moja ya mashairi yake ya mwisho, Ndwele Imenishika[4]. Alifariki dunia tarehe 8 Juni 1969 mjini Dodoma akiwa na umri wa miaka 51.
Kazi za ushairi za Mnyampala zina misingi mizito ya kiteolojia na kifalsafa ambayo utafiti umeanza tu kuigusa kwa juu juu. Kwa maoni ya Profesa Madumulla, Mathias E. Mnyampala sasa hivi nchini Tanzania ni "Jabali Lililosahaulika". Utafiti haujakaa kimya kuhusu kazi yake upande wa Ushairi wa Kiswahili na Historia ya Wagogo wa Tanganyika. Lakini bado matokeo yake yanahitaji kuenezwa.
Vitabu vichache vya Mathias E. Mnyampala
[hariri | hariri chanzo]- Mnyampala, M. E. (1954). Historia, mila, na desturi za Wagogo wa Tanganyika. Eagle Press.
- Mnyampala, M. (1962). Utenzi wa Enjili Takatifu. Ndanda Mission Press.
- Mnyampala, M. E. (1963). Diwani ya Mnyampala (Vol. 5). East African Literature Bureau.
- Mnyampala, M. E. (c. 1968, mswada huajachapishwa). Azimio la Arusha na Maandiko Matakatifu.
- Mnyampala, M. E. (1970). Ngonjera za ukuta. Oxford University Press.
- Shihabdin Chiraghdin na Mathias E. Mnyampala (1977). Historia ya Kiswahili. Oxford University Press.
- Mnyampala, M. E. (1995). Maddox, G. H. The Gogo: history, customs, and traditions. ME Sharpe Inc.
- Mnyampala, M. E. (2011). Historia ya Hayati Sheikh Kaluta Amri Abedi (1924-1964). Ahmadiyya Printing Press. Dar es Salam. Tanzania. ISBN 9789976891645. 109 p.
- Mnyampala, M. E. (2013). Maisha ni kugharimia. Tawasifu: Toleo la kwanza lililochapishwa baada ya kifo cha mwandishi, kutokana na mswada wa 1968–1969. DL2A - Buluu Publishing. France. ISBN 9791092789027. 112 p. [Google Books] [HAL] [Internet Archive] [Zenodo]
- Mnyampala, M. E. (2014). Ugogo na ardhi yake. Toleo la kwanza lililochapishwa baada ya kifo cha mwandishi, kutokana na mswada wa 1961. DL2A - Buluu Publishing. France. ISBN 9791092789201. 112 p. [Google Books] [HAL] [Internet Archive] [Zenodo]
Kujua zaidi kuhusu Mathias E. Mnyampala
[hariri | hariri chanzo]- (sw) Nicholaus, Kyamba Anna. (2018). Mwingilianomatini katika ushairi wa Mathias Mnyampala. PhD diss., Chuo Kikuu cha Moi, Kenya.
- (sw) Longinus, Ponera Denice. (2015). Nafasi ya ukristo katika ushairi wa Mnyampala. Ilihifadhiwa 3 Januari 2024 kwenye Wayback Machine. Shahada ya uzamili, Chuo Kikuu cha Dodoma, Tanzania.
- (sw) Madumulla, J. S. (2011). Mathias Eugene Mnyampala (Jabali Lililosahaulika).
- (en) Mulokozi, M. M., & Sengo, T. S. (1995). History of Kiswahili poetry. TUKI/Inst. of Kiswahili Research.
- (fr) Roy, Mathieu, & Mnyampala, Charles M. (2007). Picha yake Mathias E. Mnyampala. http://medihal.archives-ouvertes.fr/medihal-00517208/
- (fr) Roy, Mathieu (2013). Mathias E. Mnyampala (1917-1969) : poésie d'expression swahilie et construction nationale tanzanienne [tafsiri : Mathias E. Mnyampala (1917-1969): Ushairi wa Kiswahili na Ujenzi wa Taifa la Tanzania.] PhD diss., INALCO-Sorbonne Paris Cité, Ufaransa.
- 1 2 3 Mathias E. Mnyampala, Maisha ni kugharimia. DL2A Buluu Publishing, Paris, Ufaransa, 2013, ISBN 9791092789027. [Tawasifu ya Mathias E. Mnyampala iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2013 kutokana na mswada wa miaka ya 1968–1969.] [soma kwenye : Internet Archive] [soma kwenye : Zenodo]
- ↑ Mathieu Roy. Personal Record Form 1956 - État civil et données personnelles complètes de l'écrivain, juriste et poète tanzanien Mathias E. Mnyampala. Photography. Dodoma, Tanzania. 2008. ⟨medihal-00864020⟩ https://media.hal.science/medihal-00864020v1
- ↑ Roy, Mathieu (2013-01-18), MATHIAS E. MNYAMPALA (1917-1969) : POÉSIE D'EXPRESSION SWAHILIE ET CONSTRUCTION NATIONALE TANZANIENNE (kwa Kifaransa), Institut National des Langues et Civilisations Orientales- INALCO PARIS - LANGUES O', iliwekwa mnamo 2026-02-24. [Tasnifu ya uzamifu. Tazama kuanzia ukurasa wa 70, "Les années de jeunesse" / "Miaka ya ujana".]
- ↑ Ndwele imenishika (Mathias E. Mnyampala, 1969). Photography. Dodoma, Tanzania. 2013. ⟨medihal-00864055⟩ https://media.hal.science/medihal-00864055v1