Lome

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Jiji la Lome
Nchi Togo

Lomé ni mji mkuu wa Togo katika Afrika ya Magharibi pia mji mkubwa wa nchi hiyo pamoja na kuwa kitovu chake cha kiutawala na kiuchumi ukiwa na wakazi wanaokadiriwa kuwa 796,000 (mwaka 2006). Iko mwambaoni mwa Ghuba ya Guinea ya Atlantiki kwenye pwani fupi ya Togo yenye upana wa km 52 pekee. Mji uko karibu na mpaka wa Ghana.

Historia ya Lome[hariri | hariri chanzo]

Wakazi wa eneo la Lome walikuwa Waewe tangu karne ya 18 BK. Jina la Lome limetokana na neno la Kiewe la "alos" linalomaanisha mti mdogo unaokua katika misitu ya pwani. Kabla ya kukua kwa Lome kitovu cha biashara ilikuwapo mji wa Aneho.

Mwisho wa karne ya 19 wafanyabiashara walianzisha soko kwenye pwani la kupokea bidhaa kutoka meli bila kulipa ushuru kwa Waingereza katika Ghana ("Koloni ya Pwani la Dhahabu") jirani. Mwaka 1880 Waafrika Chico na Octaviano Olympio walifika kama wawakilishi wa kampuni ya biashara ya Kiingereza "A. and F. Swanzy" na kujenga ghala. Misafara ya Wahausa iliingia kutoka kaskazini kubeba bidhaa kwao wakajenga kambi la kudumu. Wafanyabiashara waliendelea kujenga makao yao hapa hivyo kuanzisha mji mwambaoni kati yao pia makampuni ya Kijerumani.

Serikali ya koloni la Ghana ya Kiingereza haikupendezwa na mashindano ya kiuchumi. Waewe walijisikia hatarini kuvamiwa na Waingereza jirani. Baada ya jaribio la Waingereza kuvamia Aneho kutoka Kitta (Ghana) chifu Mlapa tar. 5.07. 1884 alifanya mkataba wa ulinzi na konsuli Mjerumani Gustav Nachtigal. Mkataba huu ulukiwa mwanzo wa koloni ya Togo ya Kijerumani.

Baada ya kuimarika kwa ukoloni wao Wajerumani walipeleka makao makuu ya utawala wao Lome tarehe 6.03.1897. Wakati ule mji ulikuwa na wakazi 2,000. Tangu 1904 bandari ilipatikana iliyofuatwa na reli kwenda Aneho (1905), Kpalime (1907) na Atakpame (1909).

Hadi mwaka 1914 mji ulikuwa na wakazi 8,000 tayari wakati wa mwanzo wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Wajerumani hawakuwa na uwezo kutetea koloni yao wakaikabidhi kwa Uingereza tar. 27. Agosti 1914 waliogawana eneo na Ufaransa mwaka 1916. Sehemu kubwa pamoja na Lome ikawa chini ya Ufaransa kama eneo la kukabidhiwa kwa amri ya Shirikisho la Mataifa. Mji uliendelea kukua haraka, ukawa na wakazi 15,000 mwaka 1930 na 30,000 mwaka 1950.

Wakati wa uhuru mwaka 1960 Lome ikawa mji mkuu wa nchi huru ya Togo ikiwa na wakazi 80,000 walioongezeka kuwa 200,000 hadi 1970.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Biashara ya nje ni hasa kahawa, kokoa, kopra na mawese. Kuna kiwanda cha petroli. Msingi wa biashara ni bandari.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]