Liemba (meli)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
MV Liemba

MV Liemba (MV kwa Kiing. motor vessel) ni meli ya Kitanzania inayohudumia pwani za Ziwa Tanganyika. Ni chombo cha usafiri kwa maji chenye umri mkubwa kipo tangu mwaka 1914. Meli inasukumwa na injini ya diseli na urefu wake ni mita 67, upana mita 10 na ukubwa unatajwa ama kuwa tani 1500 au 1200. Ina nafasi ya kubeba abiria hadi 600 pamoja na mzigo tani 200 kati ya mabandari ya Ziwa Tanganyika upande wa Tanzania na mabandari ya Mpulungu (Zambia), Kalemie (J.K. Kongo) na Bujumbura (Burundi).

Historia ya ujenzi wake[hariri | hariri chanzo]

Goetzen 1915

Liemba ilijengwa Ujerumani mwaka 1913 kwa jina la "Graf von Goetzen" kwenye kiwanda cha meli cha Meyer huko Papenburg ikikusudiwa kwa huduma ya mizigo na abiria kwenye Ziwa Tanganyika. Baada ya kukamilika meli iliondolewa tena na vipande vyote hadi ribiti zake 160,000 vilifungwa katika masanduku 5,000 na kubebwa kwa meli kubwa hadi Daressalaam. Ilifika mwaka 1914 muda kidogo kabla ya mwanzo wa vita kuu ya kwanza ya dunia. Mafundi 3 kutoka Papenburg waliongozana na masanduku ya meli kwa njia ya reli hadi Kigoma. Hapa sehemu zote za meli ziliunganishwa tena kwa msaada wa wafanyakazi Waafrika 250 na Wahindi 20. Tar. 5 Februari 1915 "Graf von Goetzen" iliingizwa katika maji ya Ziwa Tanganyika.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza[hariri | hariri chanzo]

Kwa sababu ya vita iliongezwa mizinga kutoka manowari SMS Koenigsberg ikawa meli kubwa yenye silaha ziwani. Mwaka 1916 Waingereza na Wabelgiji walishambulia koloni ya Kijerumani kwa nguvu wakafaulu kuzunguka ziwa kwa njia ya nchi kavu na kukata njia ya reli kutoka Kigoma kwenda Tabora. Hapa Wajerumani waliamua kujiondoa ziwani na kuungana na jeshi lao ndani ya nchi.

Mafundi Wajerumani kutoka Papenburg waliopaswa kubaki Afrika shauri ya vita walipewa amri kuzamisha meli. Hao waliamua kwa hiari yao kutoharibu meli lakini kuizamisha kwa njia itakayowezesha kufufuka kwake. Hivyo walipaka mashine zote kwa mafuta mazito wakajaza vyumba vya mizigo kwa mchanga na kuzamisha meli polepole tar. 26 Julai 1916 kwenye sehemu ya ziwa isiyo na kina kubwa karibu na mdomo wa mto Malagarasi.

Kufufuka kama MV Liemba[hariri | hariri chanzo]

Hivyo waliwawezesha Waingereza washindi wa vita kufufusha meli mwaka 1924 na kuitumia tena wakikuta mashine zote zilifanya kazi tena baada ya kusafishwa.

Meli ilipewa jina MV Liemba kutokana jina la kale la Kifipa kwa ajili ya ziwa [1] ikaendelea kufanya huduma ziwani.

Tangu 1961 ilikuwa meli ya Jamhuri ya Tanganyika na baadaye Tanzania.

Injini ya mvuke ya awali imebadilishwa mara kadhaa sasa ni injini ya diseli. Hadi leo imeendelea kutoa huduma bila ajali kutokana na uimara wake.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

  1. Liemba ilikuwa jina la kihistoria la sehemu ya kusini ya ziwa linalojulikana tangu maandiko ya David Livingstone; linganisha: The Last Journals of David Livingstone in Central Africa from 1865 ..., Volume 1 p. 338; via google books