Nenda kwa yaliyomo

Kituo cha reli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kituo cha garimoshi)
Kituo cha reli Kigoma kwenye mwisho wa reli ya kati
Kituo kipya cha reli ya SGR mjini Nairobi

Kituo cha reli (pia: kituo cha garimoshi) ni mahali ambako abiria wanaweza kuingia na kutoka kwenye treni, na ambako mizigo inaweza kupakiwa au kutolewa.

Kituo cha abiria

[hariri | hariri chanzo]

Mara nyingi kituo cha reli huwa na angalau jukwaa moja la kupandia kwenye treni na jengo ambako tiketi zinauzwa pamoja na chumba ambako wasafiri wanaweza kusubiri. Vituo vikubwa huwa pia na huduma ya chakula au maduka kwa mahitaji ya abiria. Vituo vidogo vinapatikana bila jengo, ni jukwaa pekee penye paa ndogo kama hifadhi ya mvua na mashine ya kuuza tiketi.

Vituo muhimu ni vile vinavyohudumia abiria wengi vikiwa na nafasi ya kubadilisha treni, kwa mfano kituo cha njiapanda ambako njia mbili au zaidi ya treni zinakutana. Mara nyingi kituo muhimu iko pamoja na stendi kubwa ya mabasi ya kieneo au mjini.

Vituo vya treni hudumia treni za kila aina kama treni za mbali, za kimkoa, za mjini au za metro. Vinapatikana kama majengo kwenye ardhi au pia chini ya ardhi, wakati mwingine pia vikiinuliwa juu ya majengo mengine.

Vituo vikubwa duniani

[hariri | hariri chanzo]
  • Kituo cha reli kinachopokea abiria wengi ni Kituo cha Shinkuju jijini Tokyo, Japani, kinachotumiwa na abiria milioni 3.5 kila siku[1]
  • Kituo cha Grand Central Terminal mjini New York kina majukwaa 44[2]
  • Kituo cha Clapham Junction jijini London kinapitiwa na treni kila baada ya sekunde 20 kwenye saa kadhaa.

Kituo cha mizigo

[hariri | hariri chanzo]
Kituo cha kupanga mabehewa ya mizigo huko Ujerumani

Kituo cha kupanga mabehewa ya mizigo (Kiing. classification yard au marshalling yard) ni kituo ambako treni za mizigo hupangwa na kupokewa. Mizigo hupakiwa kwenye behewa, siku hizi mara nyingi kwa kontena; mabehewa yanayotakiwa kusafiri na kufika pamoja hupangwa katika treni moja.

Hivyo kituo cha kupanga mabehewa kina njia za reli kandokando zilizounganishwa na kuruhusu kuhamisha mabehewa kutoka njia moja kwenda nyingine ili kuunda treni.

Penye mitandao mikubwa ya reli, vituo hiyi hutumia eneo kubwa kwa idadi kubwa ya teri zinazoweza kuelekezwa mahali pengi.