Nenda kwa yaliyomo

Kige'ez

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kigeez)
Ukurasa wa "wedase Maryam", kitabu cha maisha ya Maria inayoonyesha picha ya Maria na mtoto Yesu pamoja na maelezo yaliyoandikwa kwa Ge'ez

Kige'ez (kwa maandishi ya Kiamhari: ግዕዝ; matamshi: gē-ĕz) ni lugha ya kale ya Ethiopia iliyozungumzwa zamani za ufalme wa Aksum. Baadaye ilikuwa lugha ya kimaandishi nchini Ethiopia hadi karne ya 19 na hadi leo ni lugha ya liturgia katika kanisa la orthodoksi la Ethiopia.

Huhesabiwa kati ya lugha za Kisemiti za kusini. Hutazamiwa kama lugha mama ya lugha za kisasa kama Kiamhari na Kitigrinya na Kitigre nchini Ethiopia na Eritrea.

Maandishi ya Kige'ez ni aina ya abugida yenye herufi 26 za konsonanti na 4 za vokali zinazounganishwa kuwa alama 202 kwa silabi zote zinazowezekana. Mifano ya kwanza inyojulikana ni kutoka karne ya 4 BK.