Tamazight

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kiberber)
Aina za Tamazight au lugha za Kiberber katika Afrika ya Mashariki

Aina za Tamazight au lugha za Kiberber katika Afrika ya Mashariki.

         Kitashelhiyt          Zayane
         Kitarifit          Kichenoua
         Kikabylia          Kichaouia
         Kitamasheq          Tamazight ya Kisahara
Alama ya barabarani ya "Stop!" kwa Kiarabu na Tamazight nchini Moroko

Tamazight ni jina la kundi la lugha zinazotajwa pia kama "lugha za Kiberber" na kuzungumzwa hasa Moroko na Algeria lakini pia kati ya wakazi wa jangwa kubwa la Sahara hadi eneo la Sahel. Ni lugha ya Waberberi wanaoishi kati ya wasemaji wa Kiarabu katika Afrika ya Kaskazini.

Tamazight ni kati ya lugha za Kiafrika-Kiasia. Wasemaji wa Tamazight watazamiwa kuwa wenyeji asilia wa Afrika ya Kaskazini kabla ya kuja kwa Waroma wa Kale au kwa Waarabu.

Tangu uenezaji wa Kiarabu matumizi ya Tamazight imerudi nyuma polepole. Wakazi wengi wa nchi za Afrika ya Kaskazini ni wa asili ya Kiberber lakini kwa kawaida kupotea kwa lugha humaanisha pia upotevu wa tabia ya kuwa Berber. Leo hii wamebaki wasemaji milioni 10 na wengi wao hutumia lugha yao pamoja na Kiarabu au Kifaransa katika maisha ya kila siku.

Mwandiko[hariri | hariri chanzo]

Tamazight imeandikwa tangu miaka maelfu. Mifano ya kale kabisa imehifadhiwa tangu 200 KK iliyoandikwa kwa mwandiko wa Tifinagh inayoendelea kutumiwa na Watuareg.

Aina ya Tifinagh imekuwa mwandiko rasmi nchini Moroko tangu mwaka 2003 pamoja na Kiarabu na Kilatini.

Tangu mwaka 1000 na uenezaji wa Uislamu lugha imeanza kuandikwa kwa herufi za Kiarabu.

Katika karne ya 20 imeandikwa mara nyingi kwa mwandiko wa Kilatini.

Katika nchi nyingi zilikuwa koloni za Ufaransa mwandiko ni Kilatini hadi leo.