Dhanabu ya Dajaja

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Dhanabu ya Dajaja (A Cygni, Deneb)
(vipimo vyote huwa na kiwango cha mashaka)[1]
Ulinganifu wa ukubwa wa Dhanabu ya Dajaja na Jua letu
Kundinyota Dajaja (Cygnus)
Mwangaza unaonekana 1.25
Kundi la spektra A2 I
Paralaksi (mas) 2.29 ± 0.32
Umbali (miakanuru) 2600 ± 200[2]
Mwangaza halisi -8.38
Masi M☉ 19
Nusukipenyo R☉ 203
Mng’aro L☉ 196,000 ± 32,000
Jotoridi usoni wa nyota (K) 8525
Muda wa mzunguko siku 80
Majina mbadala α Cygni, Alpha Cyg, 50 Cyg, Arided, Aridif, Gallina, Arrioph, HR 7924, BD +44°3541, HD 197345, SAO 49941, FK5 777, HIP 102098.


Dhanabu ya Dajaja (Deneb) katika kundinyota yake ya Dajaja – Cygnus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji wa Afrika ya Mashariki

Dhanabu ya Dajaja (ing. na lat. Deneb pia α Alfa Cygni, kifupi Alfa Cyg, α Cyg) ni nyota angavu ya tatu katika kundinyota ya Dajaja (Cygnus). Pia ni nyota angavu ya 25 kwenye anga ya usiku. Dhanabu ya Dajaja ni sehemu ya Pembetatu ya Kiangazi kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.

Jina

Dhanabu ya Dajaja ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [3]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema ذنب الدجاجة dhanab al-dajaja linalomaanisha „mkia wa kuku" [4]. Waarabu walimfuata hapa Klaudio Ptolemaio aliyeandika Ὄρνις ornis (ndege, hasa kuku) katika orodha yake ya Almagesti; wengine walisema pia Κύκνος kyknos (bata maji, Cygnus au "swan" kwa Kiingereza) na huu ndiyo ulikuwa msingi kwa jina la kimataifa ya kundinyota. Jina la Waarabu kwa nyota lilipokelewa na wataalamu wa Ulaya kwa umbo la “Deneb” [5]

Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulikubali sehemu ya kwanza ya jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa jina la "Deneb" [6] .

Alfa Cygnis ni jina la Bayer maana ina nafasi ya kwanza kufuatana na mwangaza katika kundinyota yake.

Tabia

Dhanabu ya Dajaja - Deneb ni nyota iliyo mbali kiasi ya kwamba ni vigumu kupata vipimo kamili vya paralaksi yake. Kwa hiyo hakuna uhakika kuhusu umbali wake na tabia nyingine ; umbali hukadiriwa hadi sasa kwa matokeo yanayotofautiana baina miakanuru 1500 hadi 2600. Tofauti hizi ni muhimu pia katika vipimo vingine.


Inafahamika ya kwamba Dhanabu ya Dajaja - Deneb ni nyota kubwa sana; iko kati ya nyota za mwangaza halisi mkubwa zinazojulikana. Inatoa nuru zaidi katika dakika moja kuliko Jua letu katika mwezi.

Vipimo vyote vinavyoonyeshwa katika makala hii huwa na kiwango cha mashaka. Kuna tumaini kwamba chomboanga Gaia kinaweza kuleta vipimo vyenye uhakika zaidi.


Tanbihi

  1. Viwango vinavyotajwa chini hufuata F. Schiller / N. Przybilla (2008)
  2. F. Schiller / N. Przybilla (2008) wanataja 802 ± 66 parsek
  3. ling. Knappert 1993; Knappert aliorodhesha hapa jina la "Dhanabu ya Ukabu"; hii inaonekana ni kosa maana Ukabu na Dajaja si jirani, hakuna taarifa ya "Dhanabu =mkia" katika Ukabu - Aquila. Lakini Dajaja ilikuwa na jina mbadala kwa Kiarabu hili ni "Altair" na jina lilelile lilitumiwa pia kwa nyota angavu zaidi katika Ukabu-Aquila (Altair - Tairi).
  4. Lane, Arabic - English Lexicon (1872), part 3, uk. 993 .
  5. Allen Star-Names (1899), uk. 192f
  6. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 59 (online kwenye archive.org)
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William : An Arabic - English Lexicon by in eight parts – 1872 (Perseus Collection Arabic Materials Digitized Text Version v1.1 of reprint Beirut – Lebanon 1968) online hapa
  • Schiller, F.; Przybilla, N. (2008). "Quantitative spectroscopy of Deneb". Astronomy & Astrophysics. 479 (3): 849–858 online hapa