Carlo Maria Martini
Carlo Maria Martini S.J. (15 Februari 1927 – 31 Agosti 2012) alikuwa mchungaji wa Italia wa Shirika la Yesu (Wajesuiti), kardinali wa Kanisa Katoliki, na mtaalamu wa Biblia. Alikuwa Askofu Mkuu wa Milano kutoka 1980 hadi 2004 na alipewa hadhi ya kardinali mwaka 1983.
Martini alikuwa kiongozi wa mrengo wa kiliberali wakati wa uchaguzi wa Papa mwaka 2005 baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II. Kwa mujibu wa vyanzo vya juu ndani ya Vatikani, Martini alipata kura nyingi zaidi katika raundi ya kwanza dhidi ya Kardinali Joseph Ratzinger, mgombea wa kihafidhina: 40 kwa 38. Hata hivyo, Ratzinger alipata kura nyingi zaidi katika raundi zilizofuata na kuchaguliwa kuwa Papa Benedikto XVI.[1]
Martini alijiunga na Shirika la Yesu mwaka 1944 na kuwekwa wakfu kuwa kasisi mwaka 1952. Uteuzi wake kama Askofu Mkuu wa Milan mwaka 1980 ulikuwa hali ya kipekee, kwani kawaida Wajesuiti hawateuliwi kuwa maaskofu. Alijulikana kama mwanachama wa mrengo wa kiliberali wa uongozi wa kanisa. Akisumbuliwa na aina adimu ya ugonjwa wa Parkinson, alistaafu kama askofu mkuu mwaka 2004 na kuhamia Taasisi ya Kipapa huko Yerusalemu. Aliaga dunia katika Chuo cha Aloisianum cha Wajesuiti huko Gallarate karibu na Milan miaka nane baadaye.[2]
Masaa machache baada ya kifo chake, gazeti la kila siku la Kiitaliano Corriere della Sera lilichapisha mahojiano yake ya mwisho, ambapo alisema kuwa kanisa "lipo nyuma kwa miaka 200", akiongeza: "Utamaduni wetu umezeeka, makanisa yetu ni makubwa na tupu na urasimu wa kanisa umeongezeka. Kanisa lazima likiri makosa yake na kuanza mabadiliko makubwa, kuanzia na Papa na maaskofu. Kashfa za unyanyasaji wa watoto zinatulazimisha kufanya safari ya mageuzi."[3][4]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Is Pope Francis still a Jesuit?". National Catholic Reporter (kwa Kiingereza). 2013-03-18. Iliwekwa mnamo 2018-12-20.
- ↑ L'addio a Martini, "Chiesa indietro di 200 anni", L'ultima intervista: "Perché non-si scuote, perché abbiamo paura?" Corriere della Sera, 1 settembre 2012
- ↑ Translated final interview with Martini National Catholic Reporter (NCR), 4 September 2012
- ↑ Cardinal Carlo Maria Martini, his final interview, and a damning critique that has rocked the Catholic Church The Independent, 3 September 2012
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |