Carl Gustav Jung

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Carl Jung

Carl Gustav Jung (mara nyingi hutajwa kwa kifupi zaidi C.G. Jung; 26 Julai 18756 Juni 1961) alikuwa tabibu na mtaalamu wa saikolojia kutoka Uswisi aliyeandika kwa Kijerumani.

Alifanya utafiti wa tiba ya magonjwa ya akili akaunda nadharia mbalimbali zinazoendelea kutumiwa hadi leo. Ndiye aliyeanzisha mafundisho ya saikolojia ya kichambuzi (analytical psychology).

Kwa miaka kadhaa alikuwa ameshirikiana na Sigmund Freud kuendeleza mafundisho ya tiba nafsia [1] (psychoanalysis) lakini baadaye waliachana kwa sababu Jung hakukubaliana na mawazo kadhaa ya Freud, hasa nadharia yake juu ya libido.

Kati ya mafundisho yake yanayoendelea kutumiwa ni mpangilio wa aina za silika ndani ya nafsi ya watu alipotofautisha watu wenye tabia ya mdani au msondani.

Jung alifundisha pia kama Sigmund Freud ya kwamba kuna sehemu ndani ya akili isiyofikiwa na fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa juu ya mawazo na matendo yake. Ndani ya hiyo akili isiyofikika Jung alitofautisha kati ya sehemu ya binafsi, inayotunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake, na sehemu nyingine ya kijamii, inayotunza maarifa ya binadamu yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa kwa karne nyingi ndani ya roho za watu kupitia vizazi vingi.



References[hariri | hariri chanzo]

  1. udodosinafsi (BAKITA. Istilahi za Kiswahili. Baraza la Kiswahili la Taifa. ISBN 9978-903-14-2 Check |isbn= value (help). ) au uchanganuzinafsi, upembuziakili (A.M.A. Mwita; H.J.M. Mwansoko. Kamusi ya Tiba. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili - Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. ISBN 9976-911-65-3. )