Akina Dada Faioli
Akina Dada Faioli ni wanawake watatu wa familia moja ya Anticoli (Campagna e Marittima, Dola la Papa, leo Fiuggi, wilaya ya Frosinone katika mkoa wa Lazio, Italia ya Kati) walioishi katika karne ya 18 na kuanzisha shirika la kitawa linaloitwa Masista wa Imakulata wa Mt. Klara.
Maisha yao
[hariri | hariri chanzo]Teresa (aliyezaliwa tarehe 2 Desemba 1715), Cecilia (aliyezaliwa tarehe 28 Februari 1719) na Antonia (aliyezaliwa tarehe 10 Juni 1723), walipofiwa mama yao walikuwa na umri wa miaka 12, 8 na 4, lakini hawakukubali kukata tamaa: walijikaza na, kupitia vifaa bora vya maisha ya Kikristo yaliyotekelezwa vizuri, walizaa matunda yaliyoweza kuchangamsha wananchi wenzao, kupata kibali cha Maaskofu, kuvuta wasichana wengine ambao wakaja kufungua shule sehemu nyingine pia.
Akina dada hao watatu mwaka 1741, kufuatana na wiki za uamsho zilizohubiriwa na mapadri Tommaso Struzzieri na Gaetano Giannini, walikuwa wa kwanza kuwajibika na "(…) katika nyumba yao iliyokuwa chini ya kanisa la parokia ya Mt. Stefano (…) waliamua kutawa; jambo hilo lilipojulikana katika eneo lile, wasichana wengine walikusanyika huko mchana ili kutimiza ibada zao. Halafu, juhudi zao zikiongezeka, walifungua huko aina ya shule ili kuelimisha wasichana katika misingi ya dini yetu takatifu". Ndivyo vyanzo vya wakati ule vinavyosimulia kifupi asili ya “safari yao takatifu” iliyofaidisha wasichana wa mji huo kabla haijaenea katika ujirani na hata kuvuka bahari.
Katika mpando, kutoka huo uwanda Trento na Trieste, unaanza “Barabara ya akina dada Faioli” inayoitwa hivyo kwa heshima ya hao Walezi-Waanzilishi watatu ambao karibu kwenye barabara hiyo tu waliishi hali yao ya kuwekwa wakfu kwa Mungu katika huduma nyenyekevu ya malezi ya msingi upande wa utu na wa dini.
Wakitegemezwa na Paroko wao mstahiki – Dekano Domenico Girolami, rafiki wa Mt. Paulo wa Msalaba – aliyewatungia Kanuni ya awali ambayo ikaja kupitishwa na Askofu Giannantonio Bacchettoni mwaka 1747, akina dada Faioli walianzisha Bweni la Anticoli, taasisi iliyofuata mfano wa kazi ya maendeleo iliyofanywa miaka ya 1700 na Watawa Walimu wa Montefiascone; ambao akina Faioli walivaa kanzu yao karibu maisha yao yote, hadi ilipokubalika Kanuni mpya iliyotungwa na Askofu Cirillo Antonini, aliyewapa kanzu ya kitawa ya Mt. Klara mwaka 1781: ndivyo lilivyoanza Shirika la Masista wa Imakulata wa Mt. Klara. Badiliko la muundo lilikamilika tarehe 4 Juni 1786 ambapo Antonini alipokea nadhiri yao ndogo ya useja mtakatifu, na hao Watawa Walimu wakawa masista kamili. Ndiyo hatima ya matukio yasiyokosa upinzani na magumu vilivyovumiliwa kishujaa kwa kimya na juhudi mpya daima.
Anayetaka kupata picha sahihi ya Bweni la Anticoli ni lazima azingatie Kanuni ya awali: "Lengo kuu la Bweni na la shule liwe kuishi kwa umakinifu na kuongea na Mungu" kwa sababu "walimu wasio na roho ya Mungu wanafaa kubomoa shule kuliko kuzijenga".
Vilevile ni lazima kuzingatia matunda ya msimamo huo, kwa kuwa utafiti wa kihistoria unaonyesha mambo ya maana sana: kati ya walelewa waliotoka mbali, tunamkuta mama wa Mt. Maria De Mattias, na kuhusu masista wawili waliotumwa wafungue shule huko Ferentino, alitoa sifa zao mmojawapo wa wale waliofaidika, Mwenye Heri Caterina Troiani.
Bila ya shaka, huo uzazi mkubwa wa kiroho ulitokana na machaguo makali: walijinyima Kifransisko mali yao yote, kwa hati rasmi mbele ya wakili, ili wamtumikie Mungu tu "ambaye, ili kumpendeza na kumtumikia kikamilifu, tukiachana na ubatili wa ulimwengu, tumetawa kwa radhi kabisa", kama alivyotamka Antonia wakati wa Mkutano wa mwaka 1781. Katika ripoti rasmi ya tarehe 22 Agosti 1779 kwa Papa Pius VI, siku chache baada ya kifo cha Teresa, Askofu Antonini mwenyewe alikariri hivi maneno ya Muungamishi asiye wa kawaida aliyeteuliwa naye kwa jumuia ya Bweni: "(…) kadiri ya dhamiri yake anatakiwa kuniambia tena ananiambia kwa heri ya kimbingu, kuwa amekuta Njiwa wengi na Bibiarusi wengi wa Yesu, waliofundishwa kuhusu njia ya Bwana kwa uangalifu wa hali ya juu, kwa usahihi makini kabisa (…) hivi kwamba kwa moyo wote wanajitahidi kumpenda, kumtumikia na kumtukuza, wakishughulikia kweli ukamilifu kwa juhudi ya hali ya juu”; akaongeza, "mimi mwenyewe, miezi michache baadaye, wakati wa ziara ya kichungaji niliyofanya katika eneo lile, nilichunguza kwa kila namna tabia zao, mienendo yao, maadili yao nikajengeka sana kwa habari nilizozipata kila mahali kulingana na matarajio yangu".
Kuhusu sifa maalumu za kila mmojawapo wa akina dada hao watatu, “waliojizoesha muda wote wa maisha yao katika maadili ya Kikristo”, maneno ya kutuangaza yanapatikana katika “Kitabu cha kumbukumbu ya akina dada marehemu” ambacho kinawatambulisha hivi: Teresa (aliyefariki tarehe 14 Julai 1779) “hasa katika upendo wa jirani kwa kumtumikia kwa huduma nyenyekevu na kwa kimya”; Cecilia (aliyefariki tarehe 13 Desemba 1789) “hasa katika sala takatifu na busara”; Antonia (aliyefariki tarehe 21 Januari 1793) “alikuwa na juhudi na bidii katika kumtumikia Mungu akitimiza maadili yote, na kupenda hasa usafi wa moyo kwa maneno na matendo vilevile”.
Maendeleo ya shirika
[hariri | hariri chanzo]Shirika la Masista wa Imakulata wa Mt. Klara walilolianzisha, hatimaye likawa na hadhi ya Kipapa mwaka 1957 kwa decretum laudis ya Papa Pius XII. Shirika, likizingatia sifa ya utakatifu wao ilivyozidi kuvuma, liliomba mwaka 1987 ifunguliwe kesi ya kuwatangaza watakatifu. Hatua ya kijimbo ya kesi hiyo ilikamilika tarehe 1 Julai 1990 lakini utafiti wa kihistoria unaendelea ili kuzidi kuthibitisha maisha, maadili na sifa ya utakatifu ya hao Watumishi wa Mungu watatu.
Masalia yao, pamoja na yale ya wenzao wa kwanza, yanatunzwa katika kanisa la Imakulata huko Fiuggi, yanapotembelewa na watu wengi ambao wanasali huko na wanapenda kuacha kwa maandishi maombi na shukrani kutokana na fadhili walizojaliwa.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Tovuti rasmi ya shirika lao kwa lugha nne, mojawapo ikiwa Kiswahili Archived 19 Agosti 2013 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Akina Dada Faioli kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |