Nenda kwa yaliyomo

Olusegun Obasanjo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Obasanjo mwaka 2014.

Matthew Olusegun Aremu Obasanjo (alizaliwa 5 Machi 1937) ni jenerali mstaafu wa Jeshi la Nigeria aliyepata kuwa rais wa Nigeria mara mbili. Awamu yake ya kwanza ilikuwa kama rais wa kijeshi kati ya miaka 1976 na 1979, halafu awamu ya pili kama rais aliyechaguliwa na wananchi kati ya miaka 1999 na 2007.

Obasanjo alizaliwa katika kabila la Wayoruba akalelewa kama Mkristo wa Kibaptisti.

Mwaka 1958 akajiunga na jeshi akapanda ngazi haraka. Miaka 1967-1970 alishiriki katika vita dhidi ya Biafra. Baada ya uasi wa jeshi chini ya Murtala Mohammed mwaka 1975 alipewa cheo cha makamu wa rais. Mwaka 1976 Mohammed aliuawa na wapinzani ndani ya jeshi waliokosa kumwua Obasanjo pia. Obansajo aliweza kukandamiza uasi akateuliwa na halmashauri ya kijeshi kuwa rais mpya. Alitumia nafasi yake kuandaa uchaguzi wa mwaka 1979 akakabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa, Shehu Shagari.

Kati ya 1980 hadi 1995 alikuwa na vyeo mbalimbali vya kimataifa akagombea nafasi ya Katibu Mkuu wa UM halafu alikuwa mwenyekiti wa halmashari ya Transparency International (TI).

Dikteta wa kijeshi Sani Abacha alimfunga gerezani mwaka 1995 hadi 1998.

Wakati wa uchaguzi baada ya kifo cha Abacha aligombea urais kwa tiketi ya chama cha People's Democratic Party akashinda akawa rais tena tangu 1999. Mwaka 2003 alirudishwa madarakani.

Obasanjo alijaribu kubadilisha katiba ili aweze kuwa na nafasi ya tatu lakini hakufaulu kupata wabunge wa kutosha kwa kubadilisha katiba.

Katika uchaguzi wa mwaka 2007 alisimama upande wa mgombea Umaru Yar'Adua aliyechaguliwa. Kumkabidhi madaraka kulikuwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria ya kwamba marais wawili waliochaguliwa na wananchi waliweza kufuatana.

Mnamo Agosti 2021, Umoja wa Afrika ilimteua Olusegun Obasanjo kama Mwakilishi Mkuu wa Amani katika Pembe ya Afrika[1].

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Olusegun Obasanjo kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. AU names Obasanjo High Representative for Horn of Africa Ilihifadhiwa 30 Agosti 2021 kwenye Wayback Machine., East African 27.08.2021, iliangaliwa Agosti 2021