Nenda kwa yaliyomo

Nyati-maji wa mwitu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyati-maji wa mwitu
Kundi la nyati-maji wa mwitu (Bubalus arnee)
Kundi la nyati-maji wa mwitu
(Bubalus arnee)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Artiodactyla (Wanyama wenye vidole viwili au vinne mguuni)
Nusuoda: Ruminantia (Wanyama wanaocheua)
Familia: Bovidae (Wanyama walio na mnasaba na ng'ombe)
J. E. Gray, 1821
Nusufamilia: Bovinae (Wanyama wanaofanana na ng'ombe)
Jenasi: Bubalus (Wanyama kama nyati-maji)
C. H. Smith, 1827
Spishi: B. arnee
(Kerr, 1792)

Nyati-maji wa mwitu ni wanyama wakubwa wa pori wa spishi Bubalus arnee katika familia Bovidae, ambao pia huitwa nyati-maji wa Uhindi au arni. Nyati-maji wa mwitu anafanana sana na nyati-maji (Bubalus bubalis) aliye mnyama wa kufugwa.

Fuvu la kichwa cha nyati-maji wa mwitu.

Akiwa na uzito zaidi ya tani moja, nyati-maji wa mwitu ni mnyama mkubwa mwenye nguvu sana aliye na pembe pana kuliko wanyama wengine wote katika familia ya Bovidea.[1] Pembe hizo zina umbo wa hilali na ni nzito kwenye tako na nyembamba karibu na ncha, na madume wana pembe pana kuliko majike. Mara nyingi hizo pembe zina upana zaidi ya mita mbili.[1][2][3] Kwato kubwa zinazotanuka pia ni faida kwa kutembea katika matope na vinamasi pale wanapokula nyati hao.[1][4] Mnyama huyo ana manyoya marefu ya kutawanyika, yenye rangi ya kijivu hadi nyeusi, na ana miguu meupe-michafu chini ya magoti.[2] Mkia wake ni mrefu kiasi mwenye manyoya zaidi kwenye ncha yake, naye ana alama ya 'V' nyeupe katika chini ya shingo yake.[3]

Nyati-maji wa mwitu ana urefu wa mita 2.4–3, urefu wa mkia wa mita 0.6–1, kimo cha mita 1.5–1.9 mabegani, na uzito wa hadi tani 1.2 kwa madume.[1]

Biolojia

[hariri | hariri chanzo]

Nyati-maji wa mwitu hula asubuhi na jioni, na mara nyingine usiku. Wapendelea manyasi manyevu na majani ya mimea ya majini. Wakati wa joto, wajiogesha na kuvingirika matopeni kupunguza halijoto mwilini na kujikinga na wadudu waumao.[2]

Nyati-maji wa mwitu huishi kwa makundi, lakini hawalindi eneo maalumu wao. Nyati hawa waishi kwa makundi imara yakiwa na majike na ndama wao, nao huongozwa na jike mkuu.[1] Madume huondoka makundi hayo walipo na umri wa miaka mitatu, kwa kawaida kuungana na makundi ya madume wengine takribani kumi.[1] Dume mmoja hujamiiana na majike wawili au zaidi, na kupandisha kunaweza kutokea kwa msimu wa mvua tu, au mwaka wote. Kwa kawaida majike watazaa ndama mmoja kila miaka miwili, na Nyati-maji wa mwitu watabeba mimba kwa muda wa siku 300–340, ambao ni kipindi cha mimba kilicho kirefu kuliko nyati wengine wote. Majike wataendelea kunyonyesha ndama wao kwa miezi sita–tisa, na ndama wa kike watakomaa baada ya mwaka moja na nusu, na ndama wa kiume baada ya miaka mitatu. Nyati-maji wa mwitu wanajulikana kuishi mpaka miaka 12 porini.[4]

Usambazaji

[hariri | hariri chanzo]

Ingawa Nyati-maji wa mwitu ni wenyeji wa Asia ya kusini-mashariki, nyati-maji wengine wamefugwa sana na sasa wamesambaa kufika kwingine. Wanaishi kaskazini mpaka Afrika ya kaskazini na Mashariki ya Karibu, na pia Australia, Brazil na Amerika ya kati. Hata hivyo, Nyati-maji wa kweli wa mwitu wanafikiriwa kubaki Bhutan, Nepal, Uhindi na Uthai. Wanaishi Uhindi kwa wingi kuliko nchi nyingine zozote.[2]

Nyati-maji wa mwitu wategemea sana maji, na watumia muda mwingi wao wakivingirika mitoni au matopeni. Kwa hiyo makazi ya nyati-maji wa mwitu ni makazi manyevu kwa msitu-mtoni, mapori, vinamasi na mabwawa - kwa kawaida katika maeneo ya tambarare, lakini hadi mwinuko wa mita 2800 katika Nepal.[2]

Hali ya sasa

[hariri | hariri chanzo]

Nyati-maji wa mwitu wameainishwa kama spishi hatarini na IUCN.[5]

Ingawa Nyati-maji wa kufugwa wameshamiri na kustawi, inawezekana kwamba nyati-maji wa kweli wa mwitu watatoweka hivi karibuni - labda wemeshatoweka. Idadi ya Nyati-maji wa mwitu duniani inadhani kuwa chini ya 4000, labda ndogo zaidi, lakini inawezekana sana kwamba nyati-maji wa kweli wa mwitu hawapo kabisa. Kwa bahati mbaya, ni ngumu kuhesabu kamili idadi ya nyati-maji hao kutokana na matatizo ya kutofautiana nyati-maji wa mwitu toka nyati-maji wa kufugwa ambao wametoroka kuishi mwituni.[5] Walakini, spishi hiyo inaaminika kupungukiwa sana kutokana na uwindaji, punguo la makazi, na kuzalishwa na nyati-maji wa kufugwa.[5][2] Vitisho vingine ni magonjwa na vimelea zinazopitishwa na mifugo, na ushindani wa kupata chakula na maji baina ya nyati wa mwitu na wa kufugwa.[5]

Nyati-maji wa mwitu wanalindwa na sheria katika usambazaji wao katika Bhutan, Nepal, Uhindi na Uthai, na inadhani kwamba nyati-maji wa kweli wanakuwepo katika hifadhi kadhaa. Miradi ya hifadhi inayofanywa sasa inajaribu kuhifadhi makazi ya nyati yanayopunguzwa, lakini hiyo kazi inakuwa ngumu zaidi huku idadi ya watu inaongezeka na angamizi la makazi linaendelea.[2] Kwa huzuni, mustakabali wa nyati-maji wa kweli wa mwitu hauonekani kuwa mzuri, na wapo hatarini sana wa kutoweka kwa muda wote.

Uainishaji

[hariri | hariri chanzo]

Hapo awali nyati-maji wa mwitu alikuwa akiainishwa kama nususpishi ya nyati-maji wa kaya, Bubalus bubalis arnee. Mnamo 2003, ICZN (Tume ya Kimataifa ya Istilahi za Kizoolojia) iliamua kwamba spishi ya "Bubalus arnee" ni halali, pamoja na spishi 16 nyingine za pori, katika Maoni 2027.[6][7]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 1.4 1.5 Burnie, D. (2001). Animal. Dorling Kindersley, London.
  2. 2.0 2.1 2.2 2.3 2.4 2.5 2.6 "Animal Diversity Web". 2006-02-01.
  3. 3.0 3.1 "Thai Society for the Conservation of Wild Animals". 2006-02-01.
  4. 4.0 4.1 Ashby, K.R.; Santiapillai, C. (1986-01-01). "The life expectancy of wild artiodactyl herbivores, water buffalo (Bubalus bubalis), sambar (Cervus unicolor), spotted deer (Axis axis) and wild pig (Sus scrofa) in Ruhuna National Park, Sri Lanka and the consequences for management". Tigerpaper. 13(2): 1-7.
  5. 5.0 5.1 5.2 5.3 "IUCN Red List". 2007-12-01.
  6. "Biodiversity Studies". 2003-01-01. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-06-01. Iliwekwa mnamo 2014-11-22.
  7. "Opinion 2027". 2003-03-01.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.