Waalevi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Upanga wa Ali unaoitwa "Dhu-l-fiqar" ni nembo ya Waalevi. Maandishi ya Kiarabu yasema: "Ali wali-ul-Allah" = Ali ni "wali" (=rafiki, karibu na, aliyepewa mamlaka na) wa Allah; halafu ndani ya upanga "la fata ila Ali" = hakuna mshujaa isipokuwa Ali; kushoto: "la saifu ila dhu-l-fiqar" = hakuna upanga isipokuwa Dhu-l-fiqar.
Maeneo penye Waalevi katika nchi ya Uturuki

Waalevi ni jina kwa jumuiya ya kidini na kiutamaduni katika nchi ya Uturuki. Jina latokana na Ali aliyetazamiwa kuwa na tabia za kimungu katika mikondo mbalimbali ya Washia. Asili yao ni Uislamu wa Kishia jinsi ulivyoenea kati ya makabila ya Kiturki wakati walipohamia katika Anatolia (Uturuki wa leo) kuanzia karne ya 13. Idadi ya Waalevi hukadiriwa kuwa kati ya milioni 10 hadi 25.[1] Wengi wao ni Waturuki au Waturki, wengine Wakurdi.

Sehemu ya Waalevi wanajitazama kama jumuiya ya Kiislamu- Kishia, wengine kama jumuiya ya kiutamaduni au kidini isiyo kiislamu tena.

Hawana msikiti bali hukutana katika "cem-evi" (nyumba ya cem = jamii) kwa ibada inayoitwa "cem". Katika "cem" kuna masoma ya sala na mashairi na pia aina ya ngoma ya kidini ambako wote wanacheza chini ya usimamizi wa "dede" (=baba) yaani mzee au kiongozi mwenye elimu ya kidini. Wanawake na wanaume hushiriki na kucheza pamoja. Sehemu ya ibada hii ni pia kushiriki pamoja kunywa divai au maji ya matunda.

Wanawake na wanaume hutazamiwa kuwa na haki sawa na wanawale hawatakiwi kuvaa hijabu.

Menginevyo kila Mwalawi husali jinsi anavyoona mwenyewe maana wanasisitiza ni wajibu wa kila mtu kuwasiliana na Mungu na kutafuta njia yake.

Katika imani yao huamni ya kwamba Mungu (=allah) alijionyesha hasa katika Muhamad na Ali na nguvu ya kumungu ilionekana ndani ya hao wawili.

Wana pia imani kubwa katika maimamu 12 (sawa na jina kaa maimamu 12 wa Shia) lakini wanaamini tofauti na Ithnasheri wakiamini kila imamu ni umbo la Ali aliyerudi ndani yao. Imamu wa mwisho amefichwa -sawa na imani ya Ithanasheri- atarudi.

Katika maadili wanafundisha kuelekea kufikia hali ya mwanadamu kamili bila makosa atakayeshinda tamaa zake zote na kutawala mikono yake, ulimi wake na kiuno chake, kuwatendea watu wote haki bila ubaguzi na kuwasaidia katika mahitaji yao.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. ling. Krisztina Kehl-Bodrogi: From the introduction of Syncretistic Religious Communities in the Near East edited by her, B. Kellner-Heinkele, & A. Otter-Beaujean. Leiden: Brill, 1997; David Shankland: Structure and Function in Turkish Society. Isis Press, 2006, p. 81; John Schindeldecker: From his Turkish Alevis Today; David Zeidan: "The Alevi of Anatolia," 1995.