Nenda kwa yaliyomo

Sanduku la posta

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Masanduku kwenye jengo la posta

Sanduku la posta (kifupi: S.L.P.; kwa Kiingereza Post Office Box, kifupi: P.O.B.) ni sanduku linalofungwa kwa kitasa linalopatikana katika jengo la posta.

Linakodiwa na mteja anayepokea ufunguo wa sanduku. Kila sanduku huwa na namba yake na namba hiyo ni anwani yake akituma au kupokea barua au vifurushi.

Wakati barua inafika kwenye ofisi husika, inawekwa katika sanduku la posta linalotajwa kwenye bahasha ya barua. Kwa kawaida masanduku hupatikana kwenye sehemu ya jengo la posta inayoweza kufikiwa wakati wote, hivyo mteja anaweza kuchukua barua saa yoyote bila kubanwa na ratiba ya ofisi.

Anwani ya mtaani na anwani ya sanduku la posta

Katika nchi nyingi mteja anaweza kuchagua kama apokee barua nyumbani kwake (akitumia anwani ya mtaa na namba ya nyumba) au kwenye sanduku la posta, au kwa njia zote mbili.

Katika nchi nyingi za Afrika, zikiwa pamoja na Kenya na Tanzania, hakuna huduma ya kupeleka barua za kawaida hadi nyumbani, hivyo sanduku la posta ni njia pekee ya kawaida kupokea barua[1]. Katika nchi hizo ni kawaida kwa watu wengi kutaja namba ya sanduku ya marafiki, shule au ofisi fulani wakihitaji kupokea barua au kifurushi.

Sanduku la posta na msimbo wa posta

Anwani inayoonyesha sanduku la posta na chini yake mahali na msimbo wa posta

Namba ya sanduku la posta lisichanganywe na namba ya msimbo wa posta (au postikodi, kutoka Kiingereza: postal code).

  • Msimbo wa posta ni namba inayohusu mji au eneo fulani; unaelekeza barua kwenda mahali fulani wakati barua zinapangwa kwa kusafirishwa mahali panapolengwa
  • Sanduku la posta ni namba inayotaja sehemu ambako barua inapofikishwa mwishoni. Hutumiwa ndani ya ofisi ya posta kwa kugawa barua kwa masanduku yaliyopo palepale.
  • Kwa hiyo katika nchi zinazotumia misimbo ya posta ni lazima kutaja zote mbili: msimbo wa posta na pia sanduku la posta (au anwani ya mtaani)

Marejeo

  1. Universal Postal Union. "Kenya" (PDF). Universal Postal Union. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-06-13. Iliwekwa mnamo 2016-02-19.

Viungo vya Nje