Mtaala

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mtaala wa kwanza kuchapwa (1576).

Mtaala (kutoka Kiarabu; kwa Kiingereza curriculum) ni mpangilio wa mambo ambayo mwanafunzi anatarajiwa kusaidiwa kujua hatua kwa hatua.

Mtaala unaweza kupanga hata ushirikiano unaotarajiwa kati ya mwalimu na wanafunzi wake ili kufikia shabaha za shule au chuo.

Nchi nyingi zina mitaala iliyopangwa kikamilifu kwa ngazi zote za elimu.

Baadhi inamuachia mwalimu nafasi kubwa zaidi ya kuona mwenyewe la kufundisha kadiri ya mahitaji ya wanafunzi wake.

Ofisi ya Kimataifa ya Elimu chini ya UNESCO ndiyo yenye jukumu hasa la kupitia mitaala na utekelezaji wake duniani kote.

Mtaala na falsafa ya nchi[hariri | hariri chanzo]

Mitaala ni jumla ya mipango na uzoefu ulioratibiwa kwa ajili ya mafunzo ya aina fulani yenye malengo maalumu kwa wanafunzi. Mipango hiyo inaweza kuwa ni mambo, matendo na uzoefu wa aina yoyote ile ambayo wanafunzi wanapata chini ya uongozi na usimamizi wa shule. Hutegemea falsafa ya nchi na siasa inayoiongoza.

Mfano: nchini Tanzania falsafa ya nchi ni: Ujamaa na Kujitegemea (kutokana na siasa iliyokuwa ikiongoza chini ya Mwalimu Julius K. Nyerere. Falsafa ya elimu ni: Elimu ya Kujitegemea (inatokana na falsafa ya nchi). Madhumuni/Malengo Makuu ya Elimu nchini yameanishwa katika Sera ya Elimu ya Taifa na katika mihtasari ya masomokwa kila ngazi (Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Juu)

Bila mwongozo wa falsafa ya nchi na madhumuni ya elimu kitaifa wakuza mitaala watakosa mwelekeo maalumu wa ukuzaji mitaala. Hivyo ina hatari ya kufanya mtaala uwe mkusanyiko wa mambo yasiyokuwa na mwelekeo maalumu kitaifa. Madhara yake ni watumiaji kukosa mwelekeo na msimamo maalumu unaolingana na mwelekeo wa kitaifa.

Sifa za mtaala[hariri | hariri chanzo]

 • Kwa kawaida mtaala huzingatia taaluma (maarifa) ufundishaji (matendo) na kujifunza (uzoefu) katika kiwango au ngazi fulani ya elimu.
 • Pia mtaala lazima uonyeshe walengwa wa mtaala (aina ya wanafunzi watakaotumia mtaala huo), kwa mfano chekechea, watoto wa shule za msingi na sekondari na walemavu
 • Muda utakaotumika kufundisha mtaala huo, kwa mfano miaka miwili saba na minne mitatu mitano n.k)
 • Sifa za walimu watakaofundisha mtaala huo mfano walimu wenye daraja A stashahada na shahada.
 • Vifaa vitakavyotumika kufundishia walengwa na njia na mbinu zitakazotumika kupima maendeleo ya wanafunzi na ubora wa mtaala.

Kwa hiyo mtaala ni jumla ya mpango uliondaliwa kwa ajili ya kufundishia na kujifunza kwa lengo la kuwapatia walegwa maarifa ,stadi na mielekeo mbalimbali. Nguzo kuu ya mtaala ni muhtasari ambayo hutumika katika kutekeleza mtaala huo.

Muhtasari: Ni mkusanyiko wa mada zinazokusudiwa ili kukamilisha kiwango fulani cha elimu , kazi au mafunzo maalumu.Katika shughuri za wakuza ukuzaji mitaala, wakuza mitaala wanapaswa kuongozwa na malengo makuu ya elimu yanayowekwa kitaifa.

Umuhimu wa kuwa na mtaala[hariri | hariri chanzo]

 • Kudhibiti mfumo wa elimu
 • Kuongoza walimu katika ufundishaji ili wasitoke nje ya malengo makuu ya elimu na falsafa ya nchi
 • Kuwezesha kurekebisha na kuendeleza elimu
 • Kuweka malengo muhimu yaliyo kusudiwakufikia katika ufundishaji
 • Kuwa dira na mwongozo muhimu kwa walimu katika ufundishaji
 • Kutaja na kuelekeza nyenzo na vifaa vya kufundishia
 • Kuelekeza malengo makuu ya elimu katika jamii husika
 • Kuchukua taswira yote ya falsafa ya elimu ya nchi inayohusika.

Matumizi ya mtaala[hariri | hariri chanzo]

 • Kusaidia walimu na wanafunzi kutambua malengo makuu yanayo kusudiwa kufikiwa katika utoaji wa elimu
 • Kufahamisha mwalimu na mwanafunzi kuhusu masomo au mada atakazo fundishwa ili kufikia malengo aliyojiwekea
 • Kumsaidia mwalimu kutambua na kuchagua njia za kufundishia zinazofaa ili aweze kufikia malengo aliyojiwekea
 • Kumsaidia mwalimu na mwanafunzi kuchagua na kufaragua vifaa vya kufundishia na kujifunzia mada mbalimbali
 • Kumwelekeza mwalimu kuhusu njia atakazopima maendeleo ya wanafunzi na ubora wa mtaala wenyewe.

Aina za mitaala[hariri | hariri chanzo]

 1. Mtaala rasmi
 2. Mtaala usiyo rasmi
 3. Mtaala ficho

Mtaala rasmi[hariri | hariri chanzo]

Ni mkusanyo wa mambo yote anayopaswa kuyafanya na kuyafahamu mwanafunzi anapokuwa darasani. Au ni mtaala uliopangwa kwa madhumuni ya kumfundisha mwanafunzi katika mfumo rasmi wa elimu.

Sifa za mtaala rasmi[hariri | hariri chanzo]

 • Huainisha na kuweka wazi mambo, matendo na uzoefu wa aina yoyote ile ambayo mwanafunzi ataupata chini ya uongozi na usimamizi wa shule yaani taaluma ufundishaji na kujifunza katika kiwango fulani cha elimu
 • Huweka wazi aina ya walengwa
 • Huweka wazi malengo ya kufundisha mtaala
 • Huweka wazi mambo, matendo na uzoefu ambao mwanafunzi ataupata chini ya uongozi wa shule au chuo
 • Huweka bayana njia ambazo mwalimu atatumia kufundishia
 • Huweka bayana njia za kupima maendeleo ya mwanafunzi
 • Huonyesha vifaa vitakavyo tumika kufundishia mtaala
 • Huwa na muda maaalumu wa kutekelezwa

Faida za mtaala rasmi[hariri | hariri chanzo]

 • Kupunguza tofauti zinazoweza kutokea iwapo kila shule au jamii itajitungia mtaala wake
 • Kurahisisha kuandaa vifaa vya kujifunzia
 • Kurahisisha ufuatiliaji na upimaji wa maendeleo ya wanafunzi
 • Huweka bayana utaratibu wa kutahini na sifa za wale watakaofuzu baada ya kufundishwa na kutahiniwa kwa kuutumia mtaala husika.

Mapungufu ya mtaala rasmi[hariri | hariri chanzo]

 • Humfanya mwanafunzi ashindwe kufanya mambo yote yaliyo nje ya darasa kama vile ufugaji uvuvi, mila na desturi ya jamii yake.

Mitaala isiyo rasmi[hariri | hariri chanzo]

Ni mtaala unaofundisha mambo yote anayopaswa kujifunza mtoto nje ya mtaala ulio rasmi katika maisha ya kawaida ya kujifunzia. Mara nyingine mtaala huu huitwa mtaala uliofichika.

Mara nyingi mitaala hiyo huandaliwa kulingana na mahitaji ya jamii ya mwanafunzi na jamii husika kwa wakati ule.

Sifa za mtaala usio rasmi[hariri | hariri chanzo]

 • Hutokana na jamii au mazingira anayoishi mwanafunzi
 • Mada au mambo anayofundishwa zinalenga kumpatia mwanafunzi maarifa na stadi za kutatua matatizo aliyo nayo kwa wakari ule
 • Hukazia maarifa na stadi zinazo lenga kutatua matatizo yanayokabili jamii husika
 • Unaweza ukakoma mara matatizo yanapomalizika
 • Kwa kawaida haupangwi na kuratibiwa na njia kwa njia zilizo rasmi
 • Mwanafunzi anaweza kupata maarifa na stadi bila kuwa chini ya usimamizi wa shule au chuo.

Mapungufu[hariri | hariri chanzo]

 • Mwanafunzi hukosa ujuzi wa maarifa yaani mambo yote yanayofundishwa darasani katika mtaaala rasmi.

Mtaala ficho[hariri | hariri chanzo]

Mtaala huu unajumuisha matendo yote yanayosaidia ujifunzaji usiokusudiwa au usioratibiwa. Kwa mfano ujifunzaji wa utii kwa mamlaka, kuwahi/kujali muda, usafiri nakadhalika. Yaani unajumuisha mambo yote ambayo hayaonekani kwenye muhtasari wa shule kama sehemu ya mtaala.

Vipengele vya mtaala[hariri | hariri chanzo]

Katika mtaala vipengele vilivyo muhimu ni vitano ambavyo hufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kutegemeana:

 1. Malengo ya mtaala
 2. Maudhui
 3. Njia za kufundishia
 4. Zana
 5. Tathmini

Vipengele hivi vitano hufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kutegemeana kama viungo vya mwili wa binadamu. Ni vigumu kuvitenganisha ila kwa faida ya kujifunza na kuelewa kwa undani, tutavitazama kimoja kimoja katika maelezo.

Malengo ya mtaala[hariri | hariri chanzo]

Malengo ni matokeo au matarajio yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mpango/programu fulani. Mtaala wowote ule lazima uwe na malengo. Katika uwanja wa elimu, malengo ya mtaala ni mabadiliko ya tabia na mwenendo wyanayotarajiwa kupatikana kwa wanafunzi baada ya kupata programu fulani ya mafunzo.

Umuhimu wa malengo ya mtaala[hariri | hariri chanzo]

Malengo kama kipengele cha msingi cha mtaala yana umuhimu mkubwa kwani:

 • Huwa ni msingi wa vipengele vingine vyote viine vya maudhui ya mtaala
 • Huwa ni msingi wa malengo katika ngazi/kiwango vyote vya elimu-elimu ya msingi, sekondari na vyuo
 • Huwa ni msingi wa shughuri za kazi za wakuza mitaala. Wakaguzi na walimu, wanafunzi na watawala wa elimu.

Malengo ya jumla na malengo mahususi[hariri | hariri chanzo]

Malengo ya jumla ni matarajio au mabadiliko kitabia ambayo tunatarajia kuyaona kwa mtu ambae amepata elimu.Malengo ya jumla ni malengo na madhumuni ya elimu kitaifa yaliyokusudiwakutimizwa na program mbalimbaliza mafunzokatika viwango mbalimbali vya elimu. Kimsingi malengo haya yanatokana na sera ya elimu katika nchi husika.

Baadhi ya malengo ya kitaifa ni

 • kuongoza kuendeleza na kukuza vitu na uwezo wa watanzania ili waweze kutumia rasilimali zilizopo kuleta maendeleo yao binafsi na kwa Taifa zima
 • Kukuza ari ya Watanzania ili wapende kuthamini utamaduni, mila na desturi za nchi
 • Kuendelezana kukuza ndani ya Watanzania moyo wa kujiamini na tabia ya kisayansi, uelewa wao na kuuheshimu.

Sifa za malengo ya jumla[hariri | hariri chanzo]

 • Huchukua muda mrefukukamilika. Mfano hadi mwisho wa programu
 • Siyorahisi kuyapima kwa sababu hayako wazi
 • Huchukua vitendo kama kujua, kufahamu n.k.

Malengo mahususi[hariri | hariri chanzo]

Malengo mahususi ya mtaala hutokana na malengo ya jumla. Haya ni malengo yaliyokusudiwa kutimizwa na programu mbalimbali za mafunzo katika viwango mbalimbali vya elimu.

Ni kutokana na malengo mahususi kila kiwango cha ngazi fulani ya elimu ndiyo yanapatikana mahususi yanayowaongoza walimu katika kuandaa maazimio yao wanayofundishia darasani.

Maudhui haya ndio yawezayo kumuongoza mwalimu kutoa maarifa na stadi ambazo zinaweza kubadili tabia ya mwanafunzi ambayo inaweza kupimika.

Kwa mfano tunapofundisha somo la Hisabati,tunatarajia kuona mabadiliko fulani katika tabia ya mtoto kutokana na kujifunza somo zima au mada fulani. Mabadiliko hayo yanaweza yakawa maarifa,stadi au mwelekeo mwanafunzi anaouonyesha kutokana na kujifunza somo la Hisabati ambao hakuwa nao kabla ya kujifunza somo hilo.

Tunaweza kugawa malengo mahususi katika Nyanja tatu ambazo ni

 • Utambuzi
 • Stadi
 • Mwelekeo

Sifa za malengo mahususi[hariri | hariri chanzo]

 • Ni malengo yaliowazi
 • Ni rahisi kupima kufanikiwa au kutofanikiwa kwake
 • Hutumia muda mfupi wa ukamilishaji wake
 • Huumia vitendo kama fafanua,taja,eleza n.k.

Maudhui[hariri | hariri chanzo]

Katika kuunda maudhui ya mtaala ni vizuri kuzingatia maswali kama vile:

 • Ni maarifa na stadi zipi zinafaa kwa kiwango kipi cha elimu
 • Ni tabia na mwenendo upi unaofaa kurithiwa.

Misingi/vigezo vya kuchagua maudhui ya mtaala[hariri | hariri chanzo]

 • Uthabiti: Uwezo wa maudhui katika kutimiza malengo ya masomo katika kiwango husika.
 • Umuhimu: Maudhui yanayopewa kipaumbele ni yale yanayolingana hali halisi ya mausha ya jamii, uchumi wan chi inayohusika. (Ni yale yenye umuhimu katika maisha ya walengwa).
 • Mvuto: Maudhui yafaayo ni yaleyenye kuvutia na yenye kuamsha ari ya mwanafunzi ya kupenda kufahamu maudhui hayo.
 • Kufundishika: Maudhui yawe na uwezo wa kufunzika/kufundishika yaani yaendane na uwezo wa walengwa.
 • Njia na mbinu: Maudhui yazingatie mbinu na njia za kujifunzia na kufundishia
 • Muda na idadi ya maada: Maudhui yazingatie muda wa program husika. Maudhui yanapoandaliwa huwakatika mfumo wamada kubwa na mada ndogo, kulingana na mfululizo huu unatakiwa uwe unaanzia na mada rahisina kuendelea hadi zile ngumu. Mpangilio wa aina hiyo ni muhimu kwani huhusishaujifunzaji na ufundishaji kulingana na umri wa wanafunzi.

Njia na mbinu[hariri | hariri chanzo]

Ili kuweza kufanikisha tando zima la ufundishaji katika kufanikisha maudhui na malengo ya somo mwalimu hutumia vitendo mbalimbali vijulikanavyo kama njia. Na njia peke yake haiwezikufanikisha somo lazima isaidiwe na mbinu. Mbinu ni stadi maalumu inayobainisha ni jinsi gani ya kufundishia/kujifunzia itakvyowezeshwa katika tendo la kufundisha na kujifunza. Njia ni namna mwalimu anavyowasilisha mada katika mchakato mzima wa kufundisha.

Kuna njia mbili zinazoweza kutumika katika swala zima la kujifunzia na kujifunza:

 1. Njia shirikishi
 2. Njia isiyo shirikishi

Misingi ya kuchagua njia/mbinu[hariri | hariri chanzo]

 • Maudhui: Hali ya somo lenyewe na maarifa ambayo mwanafunzi wanafunzi wanatakiwa wayapate hivyo maudhui yanatakiwa yafundishike.
 • Hali ya mwanafunzi: Umri wa mwanafunzi, kukomaa na kutokomaa kiakili, mazingira yao hivyo njia/mbinu ziendane na hali za walengwa.
 • Malengo: Nini malengo ya wanafunzi wanatakiwa kufanikisha nini katika maisha yao? Njia/mbiu lazima zifanikishe malengo yaliokusudiwa.
 • Mwalimu: Uwezo mwalimu katika kutumia nji/mbinu ujuzi na utaalamu wake.

Vifaa vya mtaala[hariri | hariri chanzo]

Mtaala una vifaa vyake maalumu ambavyo vinatakiwa vitumike kwa usahihi ili kutekeleza mtaala kwa ufanisi. Vifaa hivyo ni:

 • Muhtasari
 • Vitabu vya kiada
 • Vitabu vya ziada
 • Kiongozi cha mwalimu
 • Kitabu cha mwalimu na rejea

Muhtasari[hariri | hariri chanzo]

Muhtasari ni mwongozo unaotaja kwa kifupi tu mambo yote yanayotakiwa yafundishwe katika mwaka mzima katika darasa fukani au kwa miaka kadhaa kwa kila darasa kwa mmpangilio maalumu.

Muundo wa muhtasari[hariri | hariri chanzo]

Muhtasari una sehemu kuu mbili:

 1. Utangulizi: Hii ni sehemu ambayohuelekeza sababu za kuwepo kwa muhtasari huo, muundo wake , malengo ya elimu katika kiwango husika na malengo ya kufundisha somo hilo katika kiwango hicho.
 2. Majedwali ya kutumia kufundishia: Hii ni sehemu ambayo huwa na maudhui ya somo husika yanayotakiwa kufundishwa kila mwaka. Majedwali ya kufundishia yana vipengele vikuu vilivyopangwa katika safukama ifuatavyo.

Vipengele vya muhtasari[hariri | hariri chanzo]

 1. Mada kuu na mada ndogo
 2. Lengo la kufundishia mada hiyo
 3. Mapendekezo ya njia za kufundishia na kujifunzia
 4. Vifaa /zana za kujifunzia na kufundishia

Matumizi ya muhtasari[hariri | hariri chanzo]

 • Kumwongoza mwalimu kuandaa maazimio ya kazi na maandalio ya masomo
 • Kuongoza waandishi wa kitabu cha kiada ,kiongozi cha mwalimu na vitabu vya rejea
 • Kuelekeza njia zifaazo katika kufundisha na kujifunzia
 • Kuandalia mwongozo wa upimaji wa maendeleo ya wanafunzi kwa mwaka au kwa kipindi cha miaka kadhaa
 • Kutathmini mtaala baada ya kipindi maalumu cha matumizi ya muhtasari huo.

Kitabu cha kiada[hariri | hariri chanzo]

Ni kitabu ambacho kinafafanua mada zote za muhtasari kwa ukamilifu. Kitabu hiki ndicho kinachobeba maudhui ya somo kwa ukamilifu.Mfano vitabu malimbali vya masomo vilivyomo mashuleni.

Sifa za kitabu cha kiada[hariri | hariri chanzo]

 • Kiwe chenye lugha rahisi inayo eleweka kulingana na kiwango cha mwanafunzi
 • Kiwe na mada zinazopangwa kwa mtiririko wenye mantiki kuanzia mada kuanzia mada rahisi hadi zile ngumu
 • Kiwe na maandishi yanayosomeka kwa urahisi ya kuvutia
 • Kiwe na maelekezo na mazoezi yanayomshirikisha mwanafunzi katika kujifunza
 • Kiwe kinaendana na muhtasari pamoja na kiongozi cha mwalimu.

Matumizi ya kitabu cha kiada[hariri | hariri chanzo]

Mwalimu hukitumia kwa kuelekeza maarifa. Hutumiwa na mwanafunzi pia kwa kujikumbushia na kufanya marudio.

Uchambuzi wa kitabu cha kiada[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vingi vya kiada vimeandaliwa katika mitindo tofautitofauti, hivyo ni jukumu la mwalimu w somo pengine akishirikiana na wanafunzi kuchagua kitabu kinachofaa. Ili kuweza kufanya uamuzi wa kitabu kinachofaa huna budi kuchambua kwa kuzingatia mambo yafuatayo: Kwa kiasi gani mada zote za muhtasari zimefafanuliwa kwa ufanisi pamoja na kuzingatia sifa za kitabu cha kiada.

Kiongozi cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

Hiki ni kitabu kinachompa mwalimu maelekezo ya mada ya kufundisha, jinsi ya kuifundisha, maudhui gani yafundishwe na kutumia vifaa au zana gani. Pia kinaitwa kitabu cha mwongozo kwa mwalimu.

Sifa za kiongozi cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

 • Kiwe na utangulizi ambao unaelekeza mambo makuu na muhimu yatakayo zingatiwa katika ufundishaji. Mfano mgawanyo wa muda katika kufundisha mada mbalimbali. Mada kuu zitakazofundishwa.
 • Malengo mahsusi ya kufundisha kila mada
 • Mapendekezo ya njia na mbinu za kufundishia
 • Mazoezi ya kulingana na mada zilizoko katika kitabu cha kiada
 • Jinsi ya kupima ujifunzaji wa wanafunzi
 • Majibu ya mazoezi na na maswali yaliyomo katika kitabu cha kiada
 • Mapendekezo ya vitabu vya rejea vitakavyosaidia kutoa maarifa ya ziada kuhusu mada husika.

Umuhimu wa kitabu cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

 • Humweleza mwalimu jambo la kufanya la kufanya humpa dira au mwelekeo wa ufundishaji
 • Humsaidia mwalimu kujijengea moyo wa kujiamini na hasa kama si mzoefu wa ufundishaji wa somo hilo
 • Humsaidia mwalimu katika kuandaa somo
 • Humpa mwalimu maudhui na mifano ya ziada kuzidi kuzidi kumpanua mawazo na upeo.

Dhana ya kitabu cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

 • Ni kitabu kinachotoa maelezo ya kina kuhusu ufundishaji wa somo fulani
 • Kinaelezaa jinsi ya kutenda katika hatua zote tangua uandaaji wa somo, ufundishaji hadi upimaji
 • Ni mwongozo ambao unammpa mwalimu ujuzi wa ufundishaji.

Sifa za kitabu cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

 • Kina vitendo vyote ambavyo mwalimu hupaswa kutenda katika hatua za ufundishaji
 • Kinaeleza jinsi ya kutekeleza kazi ya ufundishaji hatua kwa hatua
 • Huweza kutumiwa na mwanafunzi pia
 • Hutoa ufafanuzi wa mada kwa kiwango cha juu zaidi ili kupanua mawazo ya mwalimu na kumuimarisha zaidi kitaaluma.

Tofauti kati ya kitabu cha mwalimu na kiongozi cha mwalimu[hariri | hariri chanzo]

 • Kitabu cha mwalimu humwelekeza hatua za kufuata katika kufundisha somo au kufanya jaribio fulani. Kiongozi cha mwalimu hupendekeza njia na mbinu mbalimbali za kufundisha somo.
 • Kitabu cha mwalimu huweza kutumiwa na mwanafunzi na mwalimu. Kiongozi cha mwalimu hutumiwa na mwalimu tu.
 • Kitabu cha mwalimu huhusika zaidi na mchakato au hatua za utendaji, kam vile utafitijaribio. Kiongozi cha mwalimu huhusika na jinsi ya kufundisha mada za masomo.kwa kawaida hutumika pamoja na kitabu cha kiada.

Vyanzo vya mitaala[hariri | hariri chanzo]

Ni muhimu kujua vyanzo vya mtaala ili kuhakikisha vinahusishwa na kuzingatiwa wakati wa kuandaa mtaala. Vyanzo hivyo ni pamoja na

 • Jamii
 • Siasa ya nchi
 • Wanafunzi
 • Wazazi
 • Walimu
 • Waajiri
 • Wataalamu mbalimbali.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 • TET (1994), Ukuzaji mitaala na Kunasihi.KIUTA (DSM)

Wizara ya elimu na Utamaduni(2005).mpango wa mafunzo ya walimu kazini Daraja la IIIC/B-A: Moduli ya soma la Mitaala. Wizara ya elimu na Utamaduni.

 • TET (2013), Moduli ya kujifunzia somo la ualimu. Taasisi ya Elimu Tanzania (DSM). Retrieved on February 05,2014 from Http:www.luwingu.wordpress.com/Mitaala.
Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtaala kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.