Nenda kwa yaliyomo

Giotto (kipimaanga)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kipimaanga Giotto)

Kwa msanii mwenye jina hili angalia Giotto

Giotto kwenye picha iliyochorwa
Picha iliyopigwa na kamera ya Giotto kabla ya kuharibiwa; inaonyesha mvuke inayotoka upande unaoangazwa na Jua

Giotto ilikuwa kipimaanga cha kwanza kilichotumwa kwenye mwaka 1985 na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Ulaya ESA kwenye anga-nje baina ya sayari. Ilikuwa pia mzigo wa kwanza wa kisayansi kilichorushwa kwa kutumia roketi ya Ariane. Kusudi la safari ilikuwa utafiti wa Nyotamkia ya Halley.

Jina lilichaguliwa kwa heshima ya msanii na mchoraji Giotto di Bondone aliyetazama nyotamkia hii kwenye mwaka 1301 na kuichora katika picha yake juu ya ziara ya "wataalamu wa nyota kutoka mashariki" kwenye hori ya Bethlehemu[1].

Safari ya Giotto ilipangwa pamoja na taasisi za usafiri wa anga-nje za Urusi na Japani zilizotuma pia vipimaanga vyao kuelekea Halley.

Giotto ilirushwa tarehe 2 Julai 1985 ikapita Halley tarehe 14 Machi 1986 kwenye umbali wa kilomita 596. Katika maandalizi ya safari wataalamu wa ESA walihofia wamba kipimaanga kinaweza kuharibika kikigongwa na vipande vya nyotamkia[2] kwa hiyo walipanga Giotto itatuma picha na vipimo mfululizo mara baada ya kukusanya data.

Kipimaanga kilipigwa wakati wa kuwa karibu na kamera yake iliharibiwa lakini vifaaa vingine viliendelea kufanya kazi kikarudi hadi Dunia.

Picha na vipimo vingine vilionyesha Halley ni gimba lenye umbo la kufanana na karanga. Urefu wake ni kilomita 15, unene kilomita 7-10. Uso unafunikwa na vumbi na rangi ni nyeusi. Upande unaoangzwa na Jua kuna sehemu ambako barafu imeanza kuyeyuka na kufoka nje. Gesi inayotoka ilipimwa kuwa maji 80%, monoksidi ya kaboni 10 %, methani na amonia 2.5% pamoja na viwango vidogo vya elementi nyingine kama feri na natiri[3].

  1. Biblia, Injili ya Matthayo 2
  2. Nyotamkia hufanywa na barafu na vumbi, na kila inapokaribia Jua vipande vinatoka nayo wakati barafu inaanza kuyeyuka
  3. Halley Flyby: 13 March 1986m tovuti ya ESA, iliangaliwa Mei 2019