Kanuni ya Archimedes

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kanuni ya Archimedes ni kanuni ya kisayansi iliyotambuliwa miaka 2000 iliyopita na mtaalamu Mgiriki Archimedes. Inaeleza nguvu ya ueleaji wa gimba ndani ya midia kama kiowevu au gesi.

Inasema:
Nguvu ya ueleaji wa gimba ndani ya midia ni sawa na nguvu ya uzito wa kiasi cha midia kilichosogezwa na gimba.

Archimedes aligundua kanuni hii alipotazama vitu vilivyowekwa katika maji. Kila mtu anayeogelea mtoni anajisikia mwepesi. Gimba linaloingia ndani ya maji linaonekana nyepesi kuliko gimba lilelile kwenye nchi kavu. Lakini masi yake haibadiliki.

Nguvu ya ueleaji ndani ya kiowevu

Hadithi jinsi Archimedes alitambua kanuni[hariri | hariri chanzo]

Archimedes alitambua hiyo alipopewa kazi ya kuchunguza kiasi cha dhahabu ndani ya taji la mfalme.

Alihangaika kwa muda mrefu hadi siku moja alipata usuluhisho wakati wa kuoga. Aliona ya kwamba maji bafuni yalipanda juu wakati alipoingia akaelewa ya kwamba mjao wa mwili ulichukua nafasi ya kiasi cha maji ambayo yalisogezwa kando na hii ilionekana kwa kupanda juu kwa uwiano wa maji wakati wa kuingia ndani ya chombo cha bafu.

Archimedes aliendelea kuelewa ya kwamba upungufu wa uzito aliosikia ndani ya maji ulikuwa sawa na uzito wa maji yaliyosukumwa kando. Hii ilimsaidia kupima taji kwa kulinganisha kiasi cha maji yaliyosukumwa na kiasi fulani cha dhahabu tupu chenye uzito uleule sawa na taji na mjao wa taji lenyewe.

Umuhimu wa kanuni ya Archimedes[hariri | hariri chanzo]

Kanuni yake ya ueleaji inafaa katika media kama viowevu au gesi. Meli na boti hazizami chini ndani ya maji kwa sababu zinasogeza maji kando na kupata ueleaji kwa njia hii. Densiti ya meli yote ni ndogo kuliko densiti ya maji hivyo inaelea.

Hata puto na ndegeputo hutumia kanuni hiyohiyo kwa kujaza nafasi ya ndani kwa gesi yenye densiti ndogo kuliko densiti ya hewa.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]