Hubble (darubini)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Darubini ya Hubble kwenye obiti yake (picha ya 1997 kutoka Space Shuttle)
Picha za Hubble za galaksi M100 kabla ya matengenzo ya 1993 na baadaye zinaonyesha jinsi kasoro za awali ziliboreshwa

Darubini ya Hubble ni darubini ya anga-nje iliyotengenezwa kwa ushirikianao baina ya taasisi za NASA na ESA kwa utafiti wa nyota. Ilipokea jina lake kwa heshima ya mwanaastronomia Edwin Hubble.

Kusudi lake[hariri | hariri chanzo]

Hubble iliandaliwa na kupelekwa angani kwa gharama za USD bilioni 4.7 na gharama za kwa jumla hadi mwaka 2010 zilikadiriwa kufikia biloni 10, zikiwa pamoja na chombo chenyewe, safari 5 za matengenezo, vipuli, kamera mpya na usimamizi na wanasayansi walioko duniani. Darubini kwenye anga-nje inaweza kutambua nyota na galaksi kwa umakini usiowezekana kwa darubini zilizopo duniani kwa sababu inachukua picha na vipimo nje ya angahewa ya Dunia inayochafusha vipimo vinavyotekelezwa kwenye uso wa ardhi.

Inachunguza pande zote za spektra ya sumakuumeme yaani mnururisho kuanzia masafa marefu ya infraredi hadi upeo wa masafa fupi za urujuanimno. Kifaa chake kikuu ni kiakisi parabola chenye kipenyo cha mita 2.4. Inazunguka Dunia kwenye obiti kilomita 540 juu ya uso wa ardhi katika muda wa dakika 93[1].

Hubble ilipelekwa kwa feri ya anga-nje kwenye obiti yake mwaka 1990. Baada ya kutuma picha za kwanza ilionekana kuna kosa kwenye kiakisi lililozuia kulenga fokasi ya kutosha. Kasoro hii ilisahihishwa wakati wa matengenezo yaliyotekelezwa mwaka 1993.

Matokeo ya tafiti zake[hariri | hariri chanzo]

Hubble ililenga hasa kuangalia na kupima nyotabadilifu za kupwita katika galaksi za karibu zinazoruhusu kukadiria umbali wa galaksi hizi. Kwa jumla matokeo ya vipimo vyake

Sombrero Galaxy in infrared light (Hubble Space Telescope and Spitzer Space Telescope)
  • Tangu mwaka 1994 Hubble ilifanya utafiti wa uga ndefu (Hubble Deep Field) kwa kulenga kwenye eneo la anga-nje pasipokuwa na nyota yoyote iliyotazamiwa hadi wakati ule. Kwenye obiti yake iliweza kuchukua picha mara kwa mara kila baada ya dakika 97 kwenye kipindi cha siku 10. Ilichukua jumla ya picha 342 ambazo baada ya kuunganishwa zilionyesha galaksi 3,000. Kwa njia hii iliwezekana kuonyesha mara ya kwanza galaksi zenye umbali wa miaka ya nuru bilioni 10 zilizoweza kuthibitishwa. Matokeo haya yalipatikana kwa sababu kiasi cha fotoni (kwanta za nuru) kinachofika kutoka nyota za mbali ni kidogo sana na kwa kuongeza muda wa kuchukua picha idadi hii inaongezeka. [2]
  • Hubble ilirudia kuchukua picha za nyuga ndefu na mwaka 2012 picha ya "Hubble eXtreme Deep Field" iliunganishwa baada ya mfichuo wa jumla ya sekunde milioni 2 uliokunsaywa katika kipindi cha miaka 10; hapa galaksi 5,500 zinaonekana na umbali mkubwa ilikuwa miaka ya nuru milioni 13.2.
  • Vipimo vyake vilileta maelewano kati ya wataalamu kuwa umri wa ulimwengi ni mnamo miaka bilioni 13.7
  • Hubble ilipiga picha ya kwanza ya sayari-nje inayozunguka nyota nje ya mfumo wa Jua letu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Hubble’s orbital path, tovuti ya spacetelescope.org, iliangaliwa Julai 2019
  2. Hubble Breakthroughs. HubbleSite. Iliwekwa mnamo 31 March 2013.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Weblinks[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: