Hard Price
' | |
---|---|
Posta ya Hard Price | |
Imeongozwa na | Vincent Kigosi |
Imetayarishwa na | RJ Company Mtaya. Mtendaji: Steps Entertainment |
Imetungwa na | Ally Yakuti |
Nyota | Jaqueline Wolper Vincent Kigosi Salim Ahmed Richard Masinde Salma Omar Grace Mapunda Sabrina Tamim |
Muziki na | Mbwana Mponda |
Sinematografi | Razak Ford |
Imehaririwa na | Mandela J. Ongati |
Imesambazwa na | Steps Entertainment |
Imetolewa tar. | 2014 |
Lugha | Kiswahili |
"Hard Price" ni jina la filamu iliyotoka 2014 kutoka nchini Tanzania. Filamu inachezwa na Jacqueline Wolper, Vincent Kigosi,Salim Ahmed, Salma Omar, Magdalena Munis na Richard Masinde. Filamu imeongozwa na Vincent Kigosi na kutayarishwa na RJ Company akiwa na Steps Entertainment. Filamu inahusu matata ya wanandoa na uimara wake. Wapo waume ambao si madhubuti katika ndoa na wale ambao wanachukulia familia kama kitu cha kwanza kabla ya vingine.[1]
Hadithi
[hariri | hariri chanzo]Filamu inaanza Patricia (Wolper) yupo hospitali anapewa majibu kama ni mjamzito. Bila furaha, anaondoka hospitalini. Huko baa, Justine (Kigosi) na David (Salim Ahmed), wanajadili maisha, lakini Justine anaonekana kuingizia masuala ya michepuko. David anaonekana kumuasa aache masuala ya wanawake, lakini inagonga mwamba na Justine anachukua msichana (Angel) na kwenda kulala nae hadi asubuhi ilhali mkewe nyumbani kalala peke yake. Asubuhi yake Patricia, anaenda kazini kwa mumewe, lakini David anaonekana kumtetea sahib wake dhidi ya tabia yake. Kesi imefika hadi kwa bosi mkubwa, kwa hekima na busara, Patricia aliomba msaada wa bosi amsaidie tatizo la mumewe la kutorudi nyumbani. Wakati anatoka ofisini kurudi nyumbani, anakutana na mumewe kwenye ngazi na Justine bila salaam kaanza lawama na vitisho.
Kwa unyenyekevu, mke kakubali yakaishe nyumbani. Baada ya kupata makanyo kutoka kwa bosi na rafiki yake wa karibu, anaamua kurudi nyumbani na kuyamaliza na mama watoto. Katika mazungumzo, Patricia kagusia kama ana mimba. Hapa sasa kivumbi kimeanza, hali ikabadilika na Justine akaanzisha zengwe la kutotaka ile mimba.Ray mwenye hasira anaazimia kutolewa kwa mimba mkwa nguvu zote na vitisho na kumwacha Patricia akiwa katika wakati mgumu. Huko baa, David na Justine wanajadili madhila ya familia ya Justine, kama ilivyo-ada Justine sio muelewa katika masuala ya kuweka sawa familia licha ya David kumsihi kwa hali na mali.
Bado maelewano hakuna ndani ya nyumba, Justine analala nje, anarudi nyumbani asubuhi kubadili nguo. Jambo hili linapelekea Patricia aombe kurudi kazini badala ya kushinda nyumbani bila shughuli ilhali hakuna mtoto wa kulea. Hata hivyo, msimamo wa Justine bado mkali katika ukandamizi dhidi ya mwanamke. Anaonesha ubabe na dharau kwa mwanamke yaani ile waziwazi. Suala hili akaona kheri amshtakie tena shemeji yake (David), anamweleza mume hataki mtoto na pindi atakavyokuwa na mimba maelewano hakuna hadi mimba ikiwa imetolewa. David anamshauri Patricia awe na subra. Huko kazini Justine anatengeneza mazingira ya kuwa wa kwanza kupata habari pindi mkewe anapoenda ofisini kupeleka malalamiko. Huko kambini pa wasichana, Angel anarudi kundini kusalimia kwa mbwembwe akijinasibu anamchuna Justine. Licha ya majigambo, wenziwe wanamkumbusha Angel kuwa haya ni maisha tu.
Justine anapata ajali na kupata ulemavu. Patricia anamsimanga kwa maneno makali dhidi ya vitendo vyake vya awali. Angel anarudi tena mjengoni mwa marafiki zake, huku vicheko vikitokea kwa mashoga zake juu ya majigambo yake yaliyokufa. Walimnanga na mwishowe wakamtimua.Anaamua kwenda kazini kwa Justine, anakutana na David na kumpatia kiasi cha pesa huku akimwahidi kutafuta namna ya kuwasiliana na Justine kwa msaada zaidi. Nyumbani kwa Justine, anaonekana kulipunguza nongwa, kawa mtiifu na kumuomba mkewe amzalie watoto. Bila majibu Patricia anaondoka zake kazini. Yule shogake Angel, Marry, kumbe ni changudoa, anamshawishi Angel waende kujiuza licha ya kuwa mjazimto.Wanakamatwa na kutiwa ndani, lakini baadaye anaachiwa huru peke yake hasa kwa kufuatia hali yake.
Anaamua kumpigia simu David, wanapanga kukutana lakini bahati mbaya Angel anavamiwa na machangudoa wenye hasira na kumjeruhi hadi kulazwa hospitali. David analipa pesa za huduma, na hatimaye kumrudisha nyumbani. Huko kuna taarifa chumba chake kimefungwa, hali hiyo inamshtua inapelekea kupata uchungu wa kujifungua. David anapandishwa cheo na kuhamishwa kikazi nchini Afrika Kusini. Angel anajifungua salama, na kurudi nyumbani kwa mama aliyemsaidia (Grace Mapunda). Anampa kazi kama msaidizi wake wa kuuza gongo. Justine anarudi kazini lakini anashtushwa na taarifa ya David kuhamishwa kikazi bila taarifa. Nyumba ambayo Angel anaishi, yule mama anamwomba awe mtoto wake wa hiari. Kwani tangu kuzaliwa hajawahi kupata mtoto. Nyumbani kwa Justine, wanapanga mipango ya kupata mtoto. Kwa pamoja wanakubaliana katika hili.Kule kwa mama Angel, kunaonekana mtoto amekua sasa, anaitwa Jimmy. Nyumbani kwa Justine, mimba hazishiki tena!
Washiriki
[hariri | hariri chanzo]- Jaqueline Wolper
- Vincent Kigosi
- Salim Ahmed
- Richard Masinde
- Salma Omar
- Grace Mapunda
- Sabrina Tamim
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Hard Price Ilihifadhiwa 4 Julai 2017 kwenye Wayback Machine. katika Bongo Cinema.
Makala hii kuhusu filamu fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Hard Price kama waigizaji wake, hadithi au matoleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |