Nenda kwa yaliyomo

Chura (nyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa mnyama mwenye jina hili angalia hapa Chura

Chura (Diphda) katika kundinyota lake la Ketusi – Cetus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji wa Afrika ya Mashariki

Chura (ing. na lat. Diphda pia β Beta Ceti, kifupi Beta Cet, β Cet) ni nyota angavu zaidi katika kundinyota la Ketusi (Cetus). Ni pia nyota angavu ya 14 kwenye anga ya usiku. Mwangaza unaoonekana unacheza kati ya mag 0.75 na 0.95.

Jina

Chura ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wakitafsiri jina lao الضفدع al-difda linalomaanisha "chura"[2]. Hakuna uhakika juu ya asili ya jina hili, maana kuna pia jina tofauti ذنب ألقيتوس ألجنوب dhanab al-qaitus al-janubi yaani „mkia wa kusini wa Ketusi“. Jina la “Difda” (chura) linatumiwa na Waarabu pia kwa ajili ya nyota ya Kinywa cha Hutu ( Fomalhaut) kwa hiyo Chura inaitwa kwao "Difda ya pili“ [3].

Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulifuata mapokeo ya Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa jina la "Diphda" [4] .

Chura hutajwa kwa jina la Bayer kama β Beta Ceti yaani kwenye nafasi ya pili ingawa ni nyota angavu zaidi katika kundinyota lake.

Tabia

Chura - Diphda ni nyota jitu jekundu yenye mwangaza unaoonekana wa mag 2.04. Iko kwa umbali na Dunia wa miaka nuru 96. Masi ya Chura ni M☉ 2.8 na nusukipenyo chake R☉ 15[5] (vizio vya kulinganisha na Jua letu) . Mwangaza halisi ni -0.13 ikiwa katika kundi la spektra "K0 III".

Mng’aro wa III katika "K0 III“ unamaanisha ya kwamba hii ni nyota jitu iliyoishiwa tayari hidrojeni katika kitovu chake ikapanuka kuwa jitu jekundu na sasa inapata nishati yake kwa myeyungano wa heliamu kwenye kitovu. Itaendelea kufanya hivyo kwa miaka milioni 100 inayofuata.

Tanbihi

  1. ling. Knappert 1993
  2. Lane, Arab-English Lexicon vol 5, uk 1815
  3. Allen (1899), uk. 163
  4. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA), iliangaliwa Novemba 2017
  5. Sägesser, S. N.; Jordan, C. (March 2005), uk 1

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 59 (online kwenye archive.org)
  • Berio, P.; et al. (November 2011), "Chromosphere of K giant stars. Geometrical extent and spatial structure detection", Astronomy & Astrophysics, 535: A59 online hapa
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William : An Arabic - English Lexicon by in eight parts – 1872 (Perseus Collection Arabic Materials Digitized Text Version v1.1 of reprint Beirut – Lebanon 1968) online hapa
* Sägesser, S. N.; Jordan, C. (March 2005). "Emission measures for the single giant β Ceti". In Favata, F.; Hussain, G. A. J.; Battrick, B. Proceedings of the 13th Cambridge Workshop on Cool Stars, Stellar Systems and the Sun, held 5–9 July 2004 in Hamburg, Germany. European Space Agency. p. 931. online hapa