Nenda kwa yaliyomo

Aden Bare Duale

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Aden Duale, 2023

Aden Bare Duale (alizaliwa katika Kaunti ya Garissa, 15 Juni 1969) ni mwanasiasa mashuhuri nchini Kenya na mwanachama wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Garissa, akamaliza mwaka wa 1981, kisha akaendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Upili ya Garissa na baadaye Moi Forces Academy, Nairobi, ambapo alihitimu mwaka wa 1987. Baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi na kupata shahada ya Elimu, kisha akapata shahada ya uzamili ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Katika uchaguzi wa mwaka 2007, Duale alichaguliwa kama Mbunge wa Eneo Bunge la Dujis kupitia tiketi ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Baadaye alihama kutoka ODM na kujiunga na chama cha United Republican Party (URP), ambapo alichaguliwa tena kama Mbunge wa Garissa Mjini katika uchaguzi wa 2013 na 2017.

Mnamo tarehe 9 Agosti 2022, Duale alichaguliwa tena kama Mbunge wa Garissa Mjini kupitia tiketi ya chama cha UDA. Hata hivyo, mnamo Oktoba 2022, Rais William Ruto alimteua kuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali yake, nafasi aliyoshikilia hadi Julai 2024, alipohamishiwa kuwa Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu.

Kwa kuwa katiba ya Kenya hairuhusu mtu kushikilia nafasi ya uwaziri na ubunge kwa wakati mmoja, Duale alilazimika kujiuzulu kama Mbunge wa Garissa Mjini baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.