Ramadhan M. Nyembe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ramadhani Mohamed Nyembe (jina la ushairi: Jua la Usiku; alizaliwa katika Mkoa wa Morogoro tarehe 4 Juni 1969) ni mshairi kutoka Tanzania.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alitokea familia ya Mohamed Ally Nyembe (1930 – 1999) na Asha Ramadhani Kitindi (mama wa nyumbani), iliyobahatika kuwa na watoto wanane, saba wakiwa wangali hai. Wazazi wake ni mchanganyiko wa makabila ya Waluguru na Wavidunda, kutoka mkoa wa Morogoro na walihamia Dodoma miaka kadhaa iliyopita.

Ndugu zake wengine ni: Salama Mohamed Ally Nyembe, Fatuma Mohamed Ally Nyembe, Mzeru Mohamed Ally Nyembe, Ibrahim Mohamed Ally Nyembe, na Ismail Mohamed Ally Nyembe.

Kama walivyo washairi na waandishi wengine, Ramadhani anatoka katika familia yenye kipaji cha uandishi wa kazi za fasihi. Baba yake, Mohamed Ally Nyembe, mfanyabiashara na mkulima, alikuwa ni mshairi maarufu mkoani Dodoma aliyetunga mashairi mengi. Baadhi ya miswada yake ya mashairi inafanyiwa kazi na wanazuoni wa Dodoma hivi sasa.

Aidha, ndugu wengine wa Ramadhani Nyembe: Salama, Fatuma, na Mzeru, ni waandishi waliobobea katika ushairi, tamthiliya, hadithi fupi na uandishi wa kazi za sinema.

Ramadhani Mohamed Nyembe, ni mtunzi mahiri, mwenye sifa adhimu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Tungo zake nyingi zimekuwa zikitoka katika magazeti, majarida na redio mbalimbali nchini.

Miongoni mwa tungo zake zinazoonesha ubunifu wa hali ya juu wa kisanaa, ni shairi lake "Mteka maji kwa fimbo, huambulia vitone"; "Kivuli cha kwenye fimbo, juani hakisitiri"; "Alaye kwa kisigino, ni dharau kwa mdomo"; "Kingeliona kisogo, macho tusingeyasifu", "Tupo Bahari ya Nyasi", na mengine mengi.

Mbali ya tungo hizo, Ramadhani ni miongoni mwa magwiji wa ngonjera waliopo hivi sasa.

Ramadhani Mohamed Nyembe ameandaa kazi kadhaa, zikiwemo hadithi za watoto, lakini hadi kufikia sasa amefanikiwa kuchapisha kitabu chake cha kwanza cha mashairi, Ngonjera, Nasaha na Uzalendo kilichosheheni tungo zenye maudhui yenye kuonya, kuelimisha, kuadibu na kuburudisha.

Kazi zake nyingine zinazokusudiwa kuchapishwa hivi karibuni:

Ramadhani ni mwajiriwa wa Mahakama ya Tanzania, katika kituo cha Dodoma.

Pia ni Makamu Mwenyekiti wa Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), Tawi la Dodoma. Aidha, kutokana na mchango wake katika fasihi ya Kiswahili, mwaka 2018 aliteuliwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) kuwa mtafiti wa kutathmini maendeleo ya Kiswahili katika asasi za Kiswahili Tanzania.

Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ramadhan M. Nyembe kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.