Planktoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Uduvi wa Krill inakula planktoni mimea na mwenyewe ni chakula cha nyangumi (urefu 1-2 cm)
Uduvi mdogo aina ya Hyperia ana urefu wa milimita 6
Planktoni mimea (mwani) inaonekana kama kanda buluu mbele ya pwani la Argentina (picha kutoka angani)


Planktoni (Kigiriki πλαγκτος planktos "inayoelea kwenye maji") ni jina la kujumlisha viumbe vidogo sana ama mimea au wanyama wanaoishi baharini. Wadogo jinsi walivyo hawana nguvu kuogelea dhidi ya mikondo ya bahari kwa hiyo wanaelea tu baharini wakisukumwa na mwendo wa maji.

Planktoni ni chanzo cha maisha ya viumbe vingine kama samaki hadi wanadamu wanokula samaki au kulisha mifugo yao unga wa samaki.

Aina za planktoni[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wanatofautiisha aina tatu:

  • Phytoplanktoni au planktoni mimea ni hasa aina za mwani (algae) ndogondogo inayoelea karibu na uso wa maji. Inatumia nuru ya jua kwa njia ya usanisinuru pamoja na madini ndani ya maji.
  • Zooplanktoni au planktoni wanyama ambayo ni uduvi wadogowadogo wenye ukubwa chini ya milimita hadi sentimita mbili na pia mayavuyavu.
  • Bakterioplanktoni au planktoni bakteria ambayo ni bakteria na archaea zinazooishi pamoja na planktoni nyingine

Chanzo cha mtando chakula[hariri | hariri chanzo]

Planktoni ni chanzo cha mtando chakula majini; planktoni mimea ni chanzo chake kabisa na aina nyingine za planktoni wanatumia mimea hii kama chakula chao.

Planktoni kwa ujumla ni lishe kwa viumbe vikubwa zaidi baharini kama samaki ambao wenyewe wanaliwa na viumbe vikubwa tena.

Kuna pia nyangumi na papa wanaokula planktoni moja kwa moja kwa kuichotea kwa midomo yao mikubwa pamoja na maji mengi na kusukuma maji nje kupitia meno yao ambayo ni mengi tena madogo kama chanuo au chujio na planktoni yenyewe inabaki ndani kama chakula.