Kizio astronomia
Kizio astronomia (ing. Astronomical Unit AU) ni kipimo cha umbali kwa ajili ya matumizi katika elimu ya astronomia. Kinalingana na umbali wa wastani kati ya dunia na jua.
Urefu wake ni mita 149,597,870,691 au kwa kifupi takriban kilomita milioni 150. Umbali huu ni sawa na wastani ya umbali kutoka kitovu cha dunia hadi kitovu cha jua.
Vipimo vilivyo kawaida duniani kama kilomita vinaweza kutumiwa katikia astronomia lakini vinaleta namba kubwa mno. Hivyo astronomia imebuni vipimo vyake vinavyorahisisha kutaja umbali wa magimba katika anga la ulimwengu. Mara nyingi astronomia hutumia kipimo cha mwaka wa nuru kwa kupima umbali katika ulimwengu. Lakini kwa umbali za karibu zaidi jinsi ilivyo ndani ya mfumo wa jua letu kizio astronomia kimechaguliwa.
63,241.077 vizio astronomia vinafanya mwaka wa nuru 1.
| Jina la sayari / gimba | Umbali hadi jua kwa vizio astronomia |
|---|---|
| Utaridi (Mercury) | 0.39 |
| Zuhura (Venus) | 0.72 |
| Dunia | 1 |
| Mirihi (Mars) | 1.52 |
| Mshtarii (Jupiter) | 5.2 |
| Zohari (Saturn) | 9.58 |
| Uranus | 19.23 |
| Neptuni | 30 |
| Ukanda wa Kuiper | kuanzia 30 |
| Pluto | 39 |
Chombo cha angani kilichofika mbali hadi sasa ni "Voyager 1". Kipo sasa takriban vizio astronomia 122 kutoka jua kimeshapita Pluto na ukanda wa Kuiper.