Christopher Mtikila
Christopher Mtikila (1950-2015) alikuwa mchungaji wa Kikristo na mwanasiasa nchini Tanzania kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party (DP).
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Mtikila alizaliwa Iringa, kusini mwa Tanzania, mwaka 1950.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu hujuma za uchumi zinazofanywa na Wahindi (ambao aliwaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akizifungua katika mahakama za Tanzania.
Kesi za kikatiba ambazo aliwahi kuzifungua ni pamoja na kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali toka kwa Mkuu wa Wilaya na polisi.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mnamo 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba.
Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala.
Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kutambua Zanzibar. Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na si Tanzania. Hata hivyo Mtikila alibadili msimamo wake katika miaka iliyofuata kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya uchaguzi inavyotaka) na hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa kudumu.
Mtikila alikuwa ni kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Katika uchaguzi huo alipata kura asilimia 0.27.
Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila alikuwa mwanzilishi na mkuu wa kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church.
Mchungaji Mtikila alijihusisha pia na harakati za haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo kiitwacho Liberty Desk.
Mchungaji Mtikali amefariki alfajiri ya Jumapili 4 Oktoba 2015 kwa ajali ya gari kwenye kijiji cha Msolwa karibu na Chalinze[1].
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Taarifa ya Dailynews kuhusu ajali". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-10-07. Iliwekwa mnamo 2015-10-04.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Rev.Christopher Mtikila Vs. The Attorney General, Civil Case No. 5 of 1993, High Court of Tanzania Ilihifadhiwa 30 Januari 2005 kwenye Wayback Machine.
- CHRISTOPHER MTIKILA INTERVIEW Ilihifadhiwa 8 Oktoba 2021 kwenye Wayback Machine., tovuti ya filamu Heaven on Earth (2005), iliangaliwa Desemba 2018