Sheikh Muhammad Mansour Haji
Sheikh Dr Muhammad bin Mansour bin Haji (amezaliwa Zanzibar mjini katika kisiwa cha Unguja tarehe 24 Mei 1941) ni mwanazuoni wa Kiislamu.
Malezi yake
[hariri | hariri chanzo]Baba yake ni Mansour bin Haji na mama yake ni Aisha binti Salim bin Hafidh. Sheikh Muhammad alilelewa na wazazi wake wawili pamoja na babu yake Sheikh Salim bin Hafidh, pia alilelewa na jirani yao Sayyid Omar bin Ally. Wazazi wake wawili waliishi Unguja mtaa wa Msufini, wilaya ya mjini, mkoa wa mjini magharibi.
Elimu
[hariri | hariri chanzo]Mnamo mwaka 1946 Dr Muhammad Mansour alianza kupelekwa chuoni kwa mwalimu wake wa mwanzo Maalim Mandoa bin Khamisi mpaka kufikia kukhitimu Qur'an kwa mafanikio ya juu.
Pia mwaka 1947 alianza mafunzo yake ya elimu ya shule yakiwemo na masomo ya dini katika shule ya msingi ya "Gulioni Zanzibar" na kuhitimu mwaka 1955. Akiwa shuleni hapo aliweza kusoma mpaka darasa la saba kwa miaka sita tu, akiwa amerukishwa darasa la tano na kwenda kusoma darasa la sita kutokana na fahamu kubwa aliyojaaliwa na Allah.
Kisha akapata nafasi ya kujiunga katika chuo cha kiislamu "Forodhani Zanzibar" kwa kuendeleza masomo ya elimu yajuu kwa muda wa miaka mitano, kuanzia mwaka 1955 mpaka mwaka 1960. Pia hapo chuoni forodhani alianza kusoma Maahad thanawiy(sanatu thaniah).
Baada ya kuhitimu chuo cha forodhani alifanikiwa kupata fursa ya msaada wa masomo (scholar ship) kwenda kusoma Misri katika chuo kikuu cha Al-azhar mwishoni mwa mwezi septemba mwaka 1961.
Safari ya Al-azhar
[hariri | hariri chanzo]Kabla ya kukubaliwa kujiunga na masomo katika chuo cha Al-azhar, aliekewa vipingamizi vizito kwa sababu ya cheti cha masomo. Cheti chake alichowasilisha kilikuwa kimesainiwa na mzungu Mr Henry ambaye kwa Zanzibar alikuwa ndiye afisa mkuu wa elimu aliyekuwa na mamlaka ya kusaini vyeti. Na kwa sababu alikuwa sio muislamu wakajiuliza walimu wa Al Azhar itakuaje mwanafunzi aingie katika chuo kikuu cha kiislamu wakati cheti kiwe kimeidhinishwa mtu asiekuwa muislamu?. Kutokana na hilo alikataliwa kujiunga na masomo chuoni hapo.
Hali hiyo ilimlazimu Sheikh Muhammad atume telegramu kwa wazee wake Zanzibar, telegramu ndiyo ilikuwa njia rahisi ya mawasiliano enzi hizo. Wazee wake nao walimuendea mwalimu wake Sheikh Suleyman bin Alawiy (r.a.) na kumlalamikia yaliyomsibu mtoto wao. Kwa bahati nzuri Sheikh Suleyman aliagiza karatasi ya barua na akaandika barua yeye mwenyewe kumuombea mwanafunzi wake aruhusiwe kujiunga na masomo ya chuo hicho. Barua hii ilimtambulisha Sheikh Muhammad kama ifuatavyo,
"Huyo ni mwanafunzi wangu, namthibitisha umahiri uhodari na jitihada zake katika masomo na kwa upeo wa ujuzi wangu kwake, naona kwa dhana yangu anastahiki kupata fursa ya kuingia katika masomo hayo ya juu kwa jinsi ninavyomuelewa..." Bali na ziada ya maneno ya hekima aliongezea.
Ilipofika barua kule chuoni, barua ilianza kusomwa na maafisa wa chini ikipanda mmoja mmoja mpaka kumfikia mkuu wa chuo, hatimae Sheikh Muhammad aliulizwa huyu aliyeandika barua hii ni nani? na amezaliwa wapi? na amesoma wapi?
Sheikh Muhammad alijibu kuwa yule ni mwalimu wake amezaliwa Zanzibar na hajasoma elimu yake pengine popote ila hapo hapo kwa wanazuoni wa Zanzibar. Kana kwamba maelezo ya barua hayakutosheleza jinsi barua ilivyoandikwa kwa utaalamu wa hali ya juu sana, walishangaa sana kwani iliandikwa kwa fani nyingi zilizotumika katika barua ile. Ndipo baadaye Sheikh Muhammad Mansour akaruhusiwa kujiunga na chuo cha Al-azhar huko nchini Misri.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sheikh Muhammad Mansour Haji kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |