Nenda kwa yaliyomo

Zavara Mponjika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Rhymson)
Zavara Mponjika
Kuanzia kushoto K-Singo (KBC), D-Rob, Fresh G, Y-Thang, Eazy B., Zavara
Kuanzia kushoto K-Singo (KBC), D-Rob, Fresh G, Y-Thang, Eazy B., Zavara
Maelezo ya awali
Jina la kuzaliwa Ramadhani Mponjika
Pia anajulikana kama Mwanavina
R.H.Y.M.S.O.N
Mwalimu
Amezaliwa 24 Novemba 1968 (1968-11-24) (umri 56)
Asili yake Dar es Salaam, Tanzania
Aina ya muziki Hip hop
Kazi yake Rapa, mwalimu, mwanaharakati, msanifu michoro
Ala Sauti
Miaka ya kazi 1988-hadi leo
Studio Mawingu Studios
Sabatatu Records
Ame/Wameshirikiana na Kwanza Unit

Zavara Mponjika (jina la kuzaliwa Ramadhani Mponjika mnamo 24 Novemba, 1968) ni mwanaharakati wa hip hop, msanifu picha (michoro), mwalimu na mwanahistoria wa Kiafrika. Mara nyingi huitwa Mwanavina, Chief Rhymson, R.H.Y.M.S.O.N - akiwa mmoja kati ya watu walioanzisha kundi la muziki wa hip hop maarufu Kwanza Unit.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Maisha na muziki

[hariri | hariri chanzo]

Huyu ni mtoto wa Dar es Salaam, kasomea Dar es Saalam na baadaye kamalizia elimu ya sekondari huko Moshi. Harakati za muziki alianza katika miaka ya 1988/89 - hasa zile harakati za kujenga KU Crew. Kulingana na Zavara, anasema wazo kuu la KU ilikuwa kuwaleta vijana pamoja na kujenga uwezo wa pamoja katika kujikwamua na magumu ya mtaa. Haikulenga muziki tu, bali hata kuondokana na hali duni ya maisha ya vijana wengi mtaani. Awali alikuwa anachana, lakini hakuwa na mipango mikubwa ya kuja kuwa labda mchanaji mkubwa au namna gani. Alikuwa anachana kwa sababu ni jambo ambalo lilikuwa moyoni mwake tu, na aliona kuchana ndiyo njia pekee ya kuonesha hisia zake machoni mwa watu au katika jamii iliyomzunguka. Hasa ukizingatia yeye ni mtu wa mwambao na huko ndiko hasa mashairi yanakotokea. Anasema ukizaliwa DAR, suala la kusikia michano ya mbele ilikuwa jambo la kawaida, haikumtisha sana kwa sababu tu, alifananisha na zile ngonjera za shule utofauti wake michano ya mbele ilikuwa inawakilishwa na lugha ya kigeni. Hapo ndipo hasa palipoanza harakati za kuchana, tena walifuata muundo uleule wa kigeni ili tu, wapite njia zilezile - huku wakifuata beats (midundo).

Kuingia mazima katika kughani (kurap)

[hariri | hariri chanzo]

Aliyemtia hamasa ya kuwa mghani, alikuwa rafiki yake mmoja marehemu sasa aliyeitwa "Gaspile" au jina halisi Abdallah Maganga (Dullah Maganga). Huyu Dullah alikuwa mtu wa mabreka (pia mabreka yalishika chati mwanzo katika miaka ya 1980 kabla ya hip hop kwa Tanzania). Katika harakati za kujichania kimpango wao, Dullah kaona mbona uwezo wa Chief ni mkubwa sana tena kupita hata wale Dullah alikuwa akiwaona wakichana katika matamasha ya kuchana. Ndipo alipomshawishi aingize mazima katika fani. Wakati huo ilikuwa zama za mapikniki, kila mtu anataka kwenda kwenye mapikniki na huko ndiko hasa balaa la kubonga liliko-kuwa linatokea. Wakati huo hasa ilikuwa Kawe Beach, Msasani Beach, baadaye kidogo Cocoa Beach, Ndege Beach na kadhalika. Sanaa mbalimbali zilifana huko moja wapo ilikuwa michano. Hiyo ilikuwa miaka ya 1988/89 - japo harakati za hip hop zilianza tangu 1985-86. Hata kaka yake alikuwa mtu wa mabreka, juhudi au maamuzi ya kuwa mshika kipaza ilikuwa ni msukumo kutoka kwa marafiki zake mtaani, haikuwa hamasa ya pesa bali jambo kutoka moyoni.

Mashindano ya kughani

[hariri | hariri chanzo]

Akiwa huko matamashani, alipata kukutana na wakongwe wa wakati huo akina Conway Francis (Chief humwita mzee wa mikogo), mchanaji mzuri sana kwa wakati huo. Shindano la kwanza kushiriki lilikuwa Kimara. Hapa alikuwa msanii wa kujitegemea - na kundi lililokuwa linavuma wakati huo ni Three Power Crew - kiongozi alikuwa Conway Francis mtoto wa Ilala na vilevile alikuwa DJ na vilevile anachana. Na kwa sifa zake kulingana na Chief, Con alikuwa mtu poa sana. Vilevile kulikuwa na mtu mmoja anaitwa Usungu a.k.a Young Millionaire, Fresh XE (Edward Mtui a.k.a King Edo). Kwa pamoja wanaunda "Three Power Crew". Sifa nyingine ya wakati ilikuwa lazima utaje eneo unalotoka katika michano kuishiria wewe wa wapi. Baadaye akataka kushiriki katika mashindano ya Kim and the Boyz (Abdulhakheem Magomero, huyu mtu muhimu katika hip hop ya TZ, alikuwa mratibu wa mashindano ya kudansi, U-DJ na baadaye hip hop Yo Raps Bonanza). Lakini Kim alimisihi Chief aungane na wenziwe ili waweze kushiriki katika shindano - kwa sababu mashindano wakati huo yalikuwa yanataka kundi na si mtu mmoja-mmoja. Ndipo hapo alifikiria kujiunga na mtu mmoja aliyekuwa anafahamiana nae katika harakati za hip hop maarufu kama MC Eddy - wakaunda Villain Gangstas wakiwa pamoja na D-Ray, G.O.D, P.G. Remmy MC a.k.a Nigga Base na wengine wengi. Baada ya muungano huu, wakawa wanatingisha hapa na pale na mashindano yalikuwa makali sana na kina Raiders Posse (watoto wa O-Bay na Kinondoni). Ungano hilo liliwezesha kushiriki katika tamasha la Kim. Watu walikuwa wanajulikana, japo magazeti yalikuwa hayaungi mkono harakati hizo kwa kile walichokiona ni kwamba ulikuwa uigizaji (hiyo 1989/90). Lakini mioyoni mwao walijua nini kitatokea hapo baadaye. Tazama leo hip hop ya TZ imezaa vijiana kama Bongo Flava, singeli na nyinginezo ambazo awali zilikuwa hazina fursa ya kusikika katika jamii ya wajamaa wa Tanganyika.

Kuanzishwa kwa Kwanza Unit

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kushiriki katika matamasha mbalimbali ya rap hatimaye wakaona heri waungane ili kutengeneza heshima ya pamoja badala ya kuwa wahasimu kama awali. Mwanzoni ilikuwa uhasimu mkubwa sana wa makundi ya rap. Ili kufika wanapopataka, Chief akaona kwanini tusiungane tukawa familia moja yenye fikra za Kikwanza ili tuondoe dhiki miongoni mwetu. Bila kusahau hata wakati huo mambo yakitokea katika ghorofa ya saba ya New Africa Hotel. Wengi waliona akina Chief mabishoo, hawana lolote bila kujua ya kwamba kuna jambo wanalianzisha kwa manufaa ya vijana wa baadaye. Hata wale waliokuwa wanabeza wakati huo hakika sasa hivi sura zao wanatafuta pa kuziweka. Chuki za kuwaona hawafanyikitu lilipelekea kutengeneza KU Crew mara moja. Wa kwanza kufuatwa ili kujenga kundi la pamoja alikuwa Adili (Nigga One - mtu matata sana katika kipaza), walivyokutana mtaa wa Mkwepu Chief akampa dodoso Adili juu ya uanzishwaji wa kundi la pamoja litakaolenga sio kutoa burudani, bali pia kuondoa hali duni ya vijana katika mtaa. Adili alikubali kwa mikono miwili jambo hili (hiyo ilikuwa katikati mwa mwaka 90). Ajabu iliyoje, katika kutekeleza azimio la kuanzisha kundi, walikuja watu karibia 20 ambao wote walikuwa na nia moja ya kuanzisha kundi. Ili kuazimia, ulipita mchujo wa kidemokrasia ili waache kila mtu katika hali ya furaha. Waliochaguliwa hasa walikuwa marapa (waghani), ma-DJ na watu wengine wawili ambao hao walihusika hasa na masuala ya kibiashara - hii ilinuia mzunguko wa kile watakacho kifanya hapo baadaye.

Biashara alisimama mtu mmoja anaitwa Samuel, DJ alikuwa Tikko (jamaa mwenye asili ya Kihindi). Mchujo ulienda wakabaki watu 15 kisha wakaanza harakati kutafuta jina la kundi na Chief akaona Kwanza ikiwa ndiyo mara ya kwanza watu wanakutana na kutengeneza kundi la namna hiyo heri iwe Kwanza Unit. Alitoa jina linalofanana kiasi na siku kuu maarufu ya Waafrika wanaoshi Marekani maarufu kama Kwanzaa. Alipendezewa na zile nguzo saba za siku kuu hiyo na kuona bora kutumia jina hilo (pia Rhymson ni mwanahistoria).[1][2][3]

Harakati baada ya kuunda KU Crew

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya maazimio, huyo mtu wa kuitwa Tikko haraka kaenda kuchongesha mafulana na watu walikuwa na hamasa ya juu hakuna mfanowe. Tikko ndiye hasa aliyekuwa anawaletea rekodi za kigeni wakati huo kwa sababu yeye kuna kipindi alikuwa anasoma mjini Londo, Uingereza. Baba yake Tikko alikuwa anamiliki kampuni ya uchanpishaji wakati huo ilikuwa inaitwa "Impreasions". Jambo hili liliwaleta pamoja vijana ili waweze kupaza sauti yao katika jamii. Kila mtu alikuwa hodari katika nafasi yake. Awali walianza kwa kuimba kwa lugha ya kigeni, lakini polepole walianza kubadili mundo na kuja kwa Kiswahili. Mtu aliyeonekana kusapoti na kufanya vizuri katika Kiswahili wakati wa zama za mpito alikuwa Fresh G. wa Tribe X alilokuwa nae Eazy B mbaya sana wa michano nae wakati huo. Inasemekana Eazy B alikuwa na floo za ajabu na uwezo wa kutunga mashairi makali yenye ujumbe mzito hakuna mfano. Mwingine D-Ray B (jina la kuzaliwa Raymond Mutagahywa - huyu wengi wanamsahau mno). Alikuwa mwandishi mzuri mno. Akina Othman Njaidi. Mwaka wa 1992, kundi likazinduliwa rasmi katika ukumbi wa Korean Cultural Center huku likiwa na usajili kamili. Na ni miongoni mwa makundi ya awali kabisa kusajiliwa rasmi - na usajili wao hadi leo uko hai pale BASATA. Vilvile Kwanza Unit ndiyo kundi la kwanza kwenda Unguja na kutumbuiza hip hop. Wao walitoa hamasa kwa vijana wa Unguja katika kujihusisha na hip-hop. Ajabu iliyoje, mlezi wa kundi hili wakati huo alikuwa Horice Kolimba. Aliwaunga mkono kwa kila hali.

  1. Zavara Mponjika akitoa somo la historia ya Afrika na kukua kwa lugha ya Kiswahili katika harakati za kujenga hip ya Tanzania - katika Tamasha la Hip Hop la Kimataifa huko Marekani.
  2. [https://africaatwork.wordpress.com/2012/08/14/lecture-by-rhymson-on-kiswahili-hip-hop-lyricism/ Ubaguzi dhidi ya hip-hop ya Tanzania na Chief Rhymson
  3. [1] Bongo’s own Zavara Mponjika aka Rhymson of the legendary hip hop crew Kwanza Unit (on the right in the picture on top) was a delegate to the festival. He was part of the first day’s Hip Hop Lecture Series where he addressed the history of hip-hop in Tanzania and aesthetics of Kiswahili lyricism.]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]