Nyota kibete nyeupe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Vibete vyeupe vinapatikana chini ya safu kuu ya nyota kwenye jedwali ya Hertzsprung-Russel.

Kibete cheupe (nyota kibete nyeupe, ing. white dwarf) ni nyota ndogo yenye umri mkubwa iliyo karibu na mwisho wa maisha yake. Imeshamaliza fueli yake ya myeyungano nyuklia imejikaza na kugandamiza masi yake katika mjao mdogo. Ina jotoridi ya juu usoni lakini mwangaza wake ni dhaifu. Jotoridi ya juu inasababisha rangi yake nyeupe. Jina "kibete" linatokana na mwangaza hafifu unaosababishwa na eneo dogo la uso wake.

Nyota kwenye safu kuu kama Jua huwa na nusukipenyo ya kilomita milioni lakini kibete cheupe kina nusukipenyo ya km 10,000 pekee yaani kama sayari. Hata hivyo kibete cheupe kina masi sawa na nyota katika mjao mdogo na pia graviti kama nyota. Densiti yake ni kubwa sana.

Nyota hizi zinatokana na nyota isiyo na masi kubwa na kuishia akiba ya fueli. Ni viini vya majitu mekundu vinavyobaki wakati nyota kubwa inaachana na tabaka zake za nje. Ndani ya kiini hiki cha nyota kubwa ya awali hakuna mchakato wa myeyungano nyuklia tena kwa hiyo hakuna chanzo cha nishati tena. Nuru inayoendelea kutoka ni nishati ya joto lakini hii inaendelea kupoa polepole. Masi yake inafanywa na mata iliyopotoka (degenerate matter); yaani atomu zake zinagandamizwa mno na elektroni zimeachana na viini vya atomu. Hivyo ni masi ya ioni (atomi yenye chaji) na elektroni zisizoshikamana kama kawaida. Hali hii inaruhusu viini vya atomu kukaribiana sana kuliko atomu kamili na hii inawezesha densiti kubwa ya kibete cheupe.

(inaendelea)