Muundo wa dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Tabaka kwenye muundo wa dunia

Muundo wa dunia unafanana na tufe kubwa yenye rediasi ya 6370 km kwa wastani[1]. Tufe la dunia yetu imeundwa kwa tabaka mbalimbali. Sayansi ina njia kuzitofautisha kufuatana na tabia zao.

Ganda, koti, kiini[hariri | hariri chanzo]

Mara nyingi mgawanyo wa matabaka matatu hutumiwa:

  • Ganda imara la nje
  • Koti ya miamba iliyoyeyuka na kupatikana kwa hali rojorojo
  • Kiini cha chuma moto lakini imara

Joto la dunia[hariri | hariri chanzo]

Kiini cha dunia ni joto sana, sayansi inakadiria sentigredi 6000 . Joto hili linapungua hadi uso wa dunia tunapoishi. Nishati kutokana na joto kutoka ardhi inaweza kutumiwa na binadamu kwa manufaa yake.

Ganda la dunia[hariri | hariri chanzo]

Hili ni ganda la nje na sehemu ya dunia tunayoona kama uso wake. Sisi na viumbehai vyote huishi juu ya ganda la dunia. Unene wake ni km 40 tu; chini ya bahari ni nyembamba zaidi. Ganda hili limevunjika katika vipande mbalimbali vinavyoitwa mabamba ya gandunia. Vipande hivi vinaelea juu ya mwamba moto rojorojo wa chini. Kati yao vinaweza kusuguana na kusababisha mishtuko tunayosikia kama mitetemeko ya ardhi.

Miamba yake ni hasa gumawesi (basalti) na itale (granite). Kwa jumla ni nyepesi zaidi kuliko tabaka za chini hivyo ganda linaelea juu. Kuna aina mbili za ganda: ganda la kibara na ganda la kibahari. Ganda la kibara linafanya mabara. Ganda la kibahari linafanya misingi ya bahari.

Koti ya dunia[hariri | hariri chanzo]

Koti ni tabaka la mwamba lenye unene wa 2,900 km linalofunika kiini cha dunia. Iko chini ya ganda nyembamba la nje la dunia ikianza takriban 30-40 km chini ya uso wa dunia na kufikia kina cha 2,900 km. Mwamba wa koti ya dunia si imara. Kutokana na joto kubwa miamba ya koti imeyeyuka inakaa katika hali ya rojorojo. Sehemu hii ni joto zaidi kuliko ganda la juu. Katika koti ya juu ina halijoto ya sentigredi mamia kadhaa; karibu na kiini halijoto hufikia 3,200 °C hadi 4,000°C.

Koti ina sehemu mbili zilizo tofauti za juu na chini halafu tabaka la katikati.

Koti ya juu ina kiasi kikubwa cha olivino (ambayo ni mwamba wa silikati ya chuma na magnesi (Mg,Fe)2SiO4)). Katika kina kikubwa zaidi mwamba huu unazidi kubadilikabadilika kutokana na joto na shindikizo kubwa.

Shindikizo hili kubwa linazuia pia miamba ya koti kuwa kiowevu kabisa ingawa halijoto inapita kiwango cha kuyeyuka kwa mwamba kwenye uso la dunia. Katika kina cha dunia uzito wa mawe ya juu unasababisha shindikizo la kutosha ili miamba hii isiyeyuke.

Tabakamwamba na tabakalaini[hariri | hariri chanzo]

Katika koti ya juu miamba iko kwa jumla katika hali imara. Tabaka hili pamoja na ganda la nje huitwa pia "tabakamwamba". Kikemia ganda na koti ya juu ziko tofauti lakini zina tabia hii moja la kuwa na mwamba imara.

Chini ya tabakamwamba kuna takabalaini ambako mwamba una hali ya geli yaani kuwa kiowevu kiasi. Tabakalaini inaanza ndani ya koti chini tabaka ya juu.

Mwendo wa mata katika tabakalaini husababisha kuvunjika kwa mwamba imara ya tabakamwamba na kuwa na mabamba mbalimbali.

Kiini cha dunia[hariri | hariri chanzo]

Kiini cha dunia ni hasa chuma pamoja na nikeli.

Kiini cha nje[hariri | hariri chanzo]

Kiini cha nje kina hali ya kiowevu kutokana na joto kali. Mnato wake huuaminiwa kufanana na maji, halijoto yake ni kati ya 4,000 - 5,000 °C.

Kiini cha ndani[hariri | hariri chanzo]

Kiini cha ndani ni sehemu yenye joto kushinda yote duniani. Kiwango cha halijoto kinapita 5,000 °C. Lakini chuma kinaaminiwa kuwa imara si kiowevu kwa sababu ya shindikizo kubwa.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Umbo la dunia si tufe kamili. Kipenyo chake kati ya sehemu za kinyume cha ikweta kinazidi umbali kati ya ncha ya kaskazini na ncha ya kusini kwa kilomita 43. Tofauti hii inatokana na kani nje inayosababisha uvimbe kwenye mzingo wa ikweta.