Muawiya ibn Abu Sufyan

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Muawiya ibn Abu Sufyan au Mu'awiya I (602 - 6 Mei 680) alikuwa khalifa au mtawala wa dunia ya Uislamu kati ya 661 na 680 na mwanzilishaji wa nasaba ya Wamuawiya.

Alizaliwa mjini Maka kama mwana wa Abu Sufyan kiongozi wa Waquraish na mpinzani wa mtume Muhamad. Baada ya ushindi wa Waislamu juu ya Maka alikuwa mfuasi wa Uislamu na kiongozi wa kijeshi muhimu wa Waislamu.

Wakati wa kifo cha khalifa Uthman alikuwa gavana wa Shamu akikaa mjini Dameski. Alikataa kumkubali Ali ibn Abu Talib kama mfuasi wa Uthman na khalifa wa nne.

Mwaka 657 jeshi lake lilikutana na jeshi la Ali kwenye mapigano ya Siffin. Hapo Ali alisita kummaliza Muawiya akakubali kusimamisha mapigano na kuondoa fitina kwa njia ya majadiliano. Majadiliano hayakutekelezwa kwa hiyo Muawiya alibaki katika nafasi yake kama mkuu wa Shamu hadi kifo cha Ali mwaka 661.

Hapo alikuwa mwenye nguvu kushinda viongozi weote wengine wa Waislamu akajitangaza khalifa na wapinzani walimkubali. Hata Hasan ibn Ali mwana wa Ali alikubali mapatano naye.

Muawiya aliendelea kukaa Dameski iliyokuwa sasa mji mkuu wa ukhalifa. Kipaumbele wa Madina kilikwisha. Muawiya mwenyewe aliweza kuimarisha utawala wake juu ya maeneo yote yaliyotawaliwa na Waislamu. Aliteua watu aliowasadiki kama magavana wa Misri na Iraq. Alitumia muundo wa utawala wa Bizanti na Uajemi uliokuwepo katika sehemu mbalimbali zilizotwaliwa na Waislamu kutoka milki hizi akawapa pia Wakristo vyeo katika idara mbalimbali za utawala wake; wanaojulikana hasa ni familia ya mwalimu Mkristo Yohane wa Dameski.

Muawiya alifaulu kukubaliwa kwa mwanawe Yazid kuwa mfuasi wake katika ukhalifa ingawa kwa kumtangaza alivunja mapatano yake na Hasan ibn Ali.

Chini ya serikali ya Muawiya eneo la Waislamu likaendlea kupanuliwa katika Maghreb na pia Uajemi ya Mashariki. Lakini alishindwa kuteka Bizanti ingawa jeshi lake lilishambulia Konstantinopoli mara mbili.

Muawiya I aliaga dunia mjini Dameski tarehe 18 Aprili 680.