Nenda kwa yaliyomo

Kuku Mashuhuri Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kuku wa kizungu)
Kuku mwenye rangi nyeupe.

Kuku Mashuhuri Tanzania ni aina mbalimbali za kuku ambao wanafugwa kwa kiwango kikubwa nchini Tanzania.

Kuna idadi kubwa ya aina za kuku wanaofugwa duniani, lakini wakazi wa Tanzania wamewagawa kuku katika makundi makuu mawili: kuku ambao wanaaminika kuwepo nchini (Tanzania) kwa muda mrefu na wale ambao wameletwa tangu miaka michache kutoka nchi nyingine hasa za Ulaya na Amerika. Makundi haya hufahamika zaidi kama kuku wa kienyeji na kuku wa kigeni (maarufu pia kama kuku wa kizungu).

Jogoo

Kuku wa kienyeji

[hariri | hariri chanzo]

Kuku wa kienyeji wanatofautiana kwa umbo na rangi lakini wote wanafanana kwa mambo yafuatayo. Kwanza woteni wadogo kwa umbo na wana wastani wa uzito wa kilo 1 hadi kilo 2 wanapofika umri kamili. Kutaga kwao huwa kwa kipindi, na kwa wastani hutaga mara tatu kwa mwaka. Wataalam wachunguzi walifanya majaribio na wakaona kuwa kuku wa kienyeji alitaga wastani wa mayai 72 kwa mwaka ambapo kuu wa kigeni alitoa wastani wa mayai 182 na zaidi kwa mwaka.

Kuku wa kienyeji hutaga mayai madogo yenye uzito wa gram 28 hadi 42, ambapo kuku wa kigeni hutaga mayai makubwa kati ya gramu 56 hadi 70. Kuku wa kienyeji huanza kutaga wakati amefikia kwenye umri wa majuma 20. Kuku hawa wa kienyeji huchelewa kukua. Wanafikia uzito wa kilo moaja na robo wakati wana umri wa majuma 21, ambapo baadhi ya kuku wa kigeni wanaweza kufikia uzito wa kilo moja na nusu kati ya majuma 8 hadi 12.

Lakini kuku wa kienyeji wanazo tabia ambazo ni nzuri na zenye faida katika ufugaji.

  • Kwanza ni hodari kujitafutia chakula chao wenyewe.
  • Pili wanao uwezo wa kulalia mayai na kuangua vifaranga, ambapo kuku wa kigeni wamepoteza uwezo huu.
  • Tatu kuku wa kienyeji wanahimili sana harubu za magonjwa mengi ya nchi hizi za joto.
  • Mara nyingi ni majasiri kwa kujilinda kutokana na wanyama kama vicheche na ndege kama mwewe, ambao huwashambulia mara wanapowaona.
vifaranga na tetea(kuku jike)

Kuku wa Kigeni

[hariri | hariri chanzo]
Mfano wa kuku wa kisasa

"Kuku wa kizungu" au "kuku wa kisasa" ni aina ya kuku kutoka nchi za Ulaya au Marekani. Wakati wa uongozi wa Julius Nyerere, nyakati za Ujamaa na Azimio la Arusha, vitu vingi kutoka nchi za nje viliitwa "vya kisasa". Hivyo "kuku wa kizungu" wanajulikana pia kwa jina la "kuku wa kisasa".

Tanzania ina aina nyingi za kuku wa kigeni nao wamegawanyika katika mafungu makubwa matatu.

Kuku wa mayai

[hariri | hariri chanzo]

Kuku hawa ni wadogo kwa umbile na hutaga wastani wa mayai 230 kwa mwaka. Kuku wa mayai wamepoteza uwezo wao wa kulalia mayai na kuangua vifaranga. Kwa sababu hii wanapoanza kutaga huendelea kwa muda wa mwaka na zaidi iwapo watapewa mazingira yanayohitajiwa. Kuku mashuhuri na anayefahamika sana katika kundi hili ni Yule kuku mweupe anayefahamika kwa jina la White Leghorn.

Kuku wa kisasa wa mayai ukiwafuga kwa umakini na kufuata ushauri wa wataalamu wenye tija wanaleta matokeo mazuri.

Kuku wa nyama

[hariri | hariri chanzo]

Kuku hawa hufugwa kwa madhumuni ya kupata nyama tu. Kuku hawa wanaweza kutaga mayai iwapo watawekwa mpaka wafike wakati wa kutaga, lakini hutoa wastani wa mayai 170 kwa mwaka, ambayo hayatamletea faida mfugaji akilinganisha na gharama za matunzo ya kuku huyo kufikia muda wa kutaga. Tanzania wapo kuku aina Anak, Cobb na Chunky

Kuku ambao wanafugwa kwa madhumuni ya mayai na nyama

[hariri | hariri chanzo]

Kuku hawa ni wakubwa kuliko kuku wa mayai, lakini ni wadogo kuliko kuku wa nyama. Utagaji wao ni wastani wa mayai 212 kwa mwaka. Wastani huu wa mayai unaweza kumpatia faida mfugaji. Baada ya kutaga wanaweza kutumiwa kwa nyama kwa sababu wanakuwa na umbile kubwa.

Mfano wa kuku wa mayai na nyama ni Rhode Island Red ambaye ni kuku mwekundu. Kuku aina ya Light Sussex ambaye ni kuku mweupe na mwenye manyoya meusi shingoni, mkiani na kwenye mabawa, pia hutumika kwa nyama na mayai. Katika kundi hili la kuku wa nyama na mayai kuku aina ya New Hampshire Red na Australop pia huonekana nchini Tanzania. New Hampshire Red ni kuku mwekundu wastani. Australop ni kuku mweusi.

Uzalishaji wa kuku

[hariri | hariri chanzo]

Jinsi siku zinavyosogea mbele ndivyo hivyo utaalamu wa uzalishaji wa kuku unavyozidi kuendelea. Wafugaji wengi wa kuku binafsi au makampuni duniani, ambayo yanayo mashamba makubwa, na wanazalisha kuku wa biashara, waenaendelea kuzalisha kuku wa aina mbalimbali kwa madhumuni ya utagaji sana wa mayai au utoaji wa nyama bora. Kuku hawa hupewa majina mbalimbali na mara nyingi hutangazwa kwenye magazeti ili wafugaji wapate kununua. Kuku hawa wanazidi kuingia nchini Tanzania, kwa mfano Anak, Chunky na Cobb ambao ni wa nyama. Shaver 288 na Shaver 577 ambao ni wa mayai.

Kuku maalum wa nyama au mayai kama hawa wasitumike tena kwa kuendelea kuzalisha au kuchanganya na kuku wa kienyeji. Iwapo mfugaji atawatumia kuku hawa maalum kwa kuendelea kuzalishia au kuchanganya na kuku wa kienyeji kwa vizazi vya mbele, vizazi hivyo hudhoofika na kumletea mfugaji matatizo mengi kama magonjwa na mengineo. Kuku ambao wanafaa kuendelea kuzalishia au kuchanganya na kuku wa kienyeji ni wale ambao wenye damu halisi ya aina yake kwa mfano New Hampshire Red, Light Sussex na Rhode Island Red.

Hitimisho

[hariri | hariri chanzo]

Sehemu nyingi nchini Tanzania na ulimwenguni pote, ufugaji wa kuku unawapatia maelfu ya watu kibarua cha muda au cha kudumu kama vile wakazi wa Kitunda, jijini Dar es Salaam. Vile vile kuku wanaweza kutumia mabaki ya chakula kama pumba za nafaka mbalimbali, ili kuongeza matumizi bora ya vyakula tunavyovivuna mashambani.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Kirumbi, D.M. (1980) Ufugaji wa Kuku (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House)

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kuku Mashuhuri Tanzania kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.