Kennedy Odede

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kennedy Odede ni mwanaharakati wa kijamii, mjasiriamali wa kijamii, na mwandishi kutoka Kibera, Kenya.

Maisha ya Kennedy Odede[hariri | hariri chanzo]

Kennedy Odede alizaliwa katika kijiji kidogo nchini Kenya katika mwaka wa 1984. Mama yake hakuwa ameolewa wakati Kennedy anazaliwa, kwa hivyo watu wa kijiji hawakumpenda Kennedy au mama yake na walisema kuwa Kennedy alikuwa mwanaharamu. Kuzaliwa kwa Kennedy kulikuwa kugumu sana lakini yeye na mama yake hawakufa. Siku ya kuzaliwa kwa Kennedy, kulikuwa na mvua kubwa, na watu wa kijiji walifikiri kuwa kuzaliwa na wakati mvua inaponyesha ni ishara kwamba Kennedy angekuwa kiongozi mkubwa. Mama yake alimpa jina la “Kennedy” kama rais wa Marekani John F. Kennedy. Wakati alipokuwa na miaka miwili, familia yake ilihamia Kibera nje ya jiji la Nairobi. Katika eneo la makazi duni la Kibera, Kennedy na familia yake waliishi katika umaskini uliokithiri. Kwa sababu ya unyanyasaji wa nyumbani, Kennedy aliondoka nyumbani kwao akiwa na umri wa miaka kumi na aliishi kwa barabara.[1]

Kibera, Kenya[hariri | hariri chanzo]

Eneo la makazi duni la Kibera nchini Kenya

Kennedy aliishi katika eneo la makazi duni la Kibera kwa miaka mingi. Eneo la makazi duni la Kibera ni eneo nje ya Nairobi, Kenya. Kibera ni mojawapo ya makazi duni makubwa zaidi katika Afrika na makazi duni makubwa zaidi katika nchi ya Kenya. Haifahamiki kikamilifu ni watu wangapi ambao wanaishi Kibera, lakini watu wanadhani kuwa ni kati ya nusu milioni na milioni. Watu wanaoishi Kibera ni maskini sana. Watu wengi wana Virusi Vya Ukimwi na kuna ubakaji mwingi. Pia, hakuna maji safi na hakuna shule zakutosha.[2]

Shining Hope for Communities (SHOFCO)[hariri | hariri chanzo]

Nembo ya "Shining Hope for Communities"

Katika eneo la makazi duni la Kibera, Kennedy alipitia umaskini, ukatili, na masuala ya kijinsia. Yeye alitaka kuanzisha shirika la wanawake, watoto, na watu wengine. Odede alikuwa na vitabu vya Martin Luther King Jr., Marcus Garvey, na Nelson Mandela, na alitiwa msukumo na wao. Viongozi hawa walimtia msukumo kupigania watu wa jamii yake, na ndipo alipoanzisha shirika ambalo linaitwa SHOFCO (Shining Hope for Communities).[3] Kwa sasa, SHOFCO ni shirika la mashinani kubwa zaidi katika Kenya. Shirika la SHOFCO limesaidia zaidi ya watu milioni 2.4 katika makazi duni nchini Kenya. SHOFCO lina programu kama:

  • Maji na Usafi wa Mazingira
  • Huduma za Kiafya
  • Huduma Muhimu
  • Mpangilio Endelevu wa Maisha
  • Uongozi na Elimu kwa Wasichana[4]

Uongozi na Elimu ya Wasichana ilikuwa moja wapo ya programu muhimu kwa Kennedy kwa sababu aliona wanawake na wasichana wengi wakifanyiwa ukatili wa nyumbani na ubakaji Kibera. Wasichana wengi hawakupata fursa ya kwenda shule. Kwa hivyo, Odede alianzisha “The Kibera School for Girls” ambayo inasaidia wasichana kwenda shule, kuwapitia chakula, na kuwasaidia kukaa salama. Kuna zaidi ya wanafunzi mia saba thelathini na tatu shuleni humo. Wasichana hawa wakiwa shuleni wana uwezakano mdogo wa kuambukizwa VVU, na pia wanakuwa watetezi wa jamii zao.

SHOFCO wameshinda tuzo nyingi kama: Excellence in Improving Access to Primary Care Services, 2018 Hilton Humanitarian Award, Mother Teresa Memorial Award for Social Justice, 2020 Future Awards Africa, na tuzo nyingine nyingi.[5]

Kennedy ni kiongozi mkuu katika jamii yake na watu wa Kibera wanamwita “Mayor”.

Chuo Kikuu cha Wesleyan[hariri | hariri chanzo]

Chuo Kikuu cha Wesleyan

Baada ya uchaguzi wa Kenya wa mwaka wa 2007, kulikuwa na vurugu nyingi nchini Kenya na Kibera. Kennedy alihitajika kuondoka nchini Kenya na alitaka kwenda Marekani kwa sababu mpenzi wake, Jessica Posner, aliishi Marekani. Jessica alijua kuwa kupata viza kwa Kennedy ingekuwa vigumu, kwa hivyo, alimsaidia kupata viza ya mwanafunzi kwa kwenda kusoma katika chuo kikuu cha Marekani. Kennedy Odede hakuwa na elimu rasmi, lakini alikuwa mwerevu sana. Kennedy alidahiliwa katika Chuo Kikuu cha Wesleyan katika jimbo la Connecticut. Yeye alikwenda katika Chuo Kikuu cha Wesleyan na aliendelea kutafuta pesa na kusaidia jamii yake ya Kibera huku akipata elimu yake. Baada ya kuhitimu na shahada ya heshima, alirudi nchini Kenya.[6]

Maisha ya Kennedy kwa Sasa[hariri | hariri chanzo]

Kwa sasa, Kennedy amemuoa Jessica Posner na wana watoto. Wao bado wanafanya kazi na SHOFCO na jamii ya Kibera. Katika mwaka wa 2015, wao waliandika kitabu kuhusu maisha na safari yao ambacho kiliitwa Find Me Unafraid. Kitabu hiki kilibuka na kuwa kitabu bora kwa mauzo katika New York Times.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Kennedy Odede", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2022-10-18, iliwekwa mnamo 2022-11-02 
  2. "Kibera", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2022-10-04, iliwekwa mnamo 2022-11-02 
  3. "Shining Hope for Communities", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2022-08-10, iliwekwa mnamo 2022-11-02 
  4. "Home". Shofco (kwa en-US). Iliwekwa mnamo 2022-11-02. 
  5. "Dr. Kennedy Odede". Concordia (kwa en-US). Iliwekwa mnamo 2022-11-02. 
  6. Kennedy., Odede, Find me unafraid, ISBN 1-5046-4838-2, OCLC 1306345939, iliwekwa mnamo 2022-11-02