Kanisa la Moravian Jimbo la Jamaika
Kanisa la Moravian Jimbo la Jamaika (Jamaica Province of the Moravian Church au kwa jina la kikamili The Moravian Church in Jamaica and the Cayman Islands) ni kitengo cha Kanisa la Moravian duniani. Eneo la jimbo hili ni nchi ya kisiwani ya Jamaika pamoja na funguvisiwa ya Cayman (eneo la ng'ambo la Uingereza) katika Bahari ya Karibi ya Amerika ya Kati. Jimbo hili limeanzisha pia kazi ya misioni huko Kuba.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Kanisa la Moravia lilianzishwa mwaka 1754 na wamisionari Zacharias Caries, Thomas Shallcross na Gottlieb Haberecht waliofika kutoka Uingereza. Walikaribishwa na familia mbili za walowezi Waingereza waliolima mashamba makubwa kwa kazi ya watumwa wakiwa kati ya mabwana wachache wa watumwa waliojali hali ya kiroho ya watumwa wao.
Mwanzoni wamisionari walianza kuwahubiri na kuwafundisha watumwa waliokuwa tayari lakini baadaye walianzisha wenyewe shamba kwa ajili ya ruzuku yao kwa kutumia kazi ya watumwa kama wafanyakazi. Hali ya kuwa mabwana wa watumwa ilionekana kama hasara maana watumwa wengi wawakuwaamini tena wakihubiri. 1823 Wamoravian walifunga shamba hili na kuendelea bila kuwa mabwana wa watumwa.
Sasa idadi ya watumwa waliokuwa tayari kuwasikiliza ilikua tena. Baada ya mwisho wa utumwa mwaka 1838 wakrito wapya walikuwa wengi zaidi. Mnamo mwaka 1854 yaani miaka 100 tangu kuanza kazi Wamoravian walikuwa na wakristo 13,129. Katika kipindi hiki wamisionari 193 walifika Jamaika na kushiriki katika ujenzi wa kanisa. Theluji moja kati hao walikufa kisiwani kutokana na magonjwa ya kitropiki.
Walianzisha pia kazi ya elimu. Kwenye vituo vyao waliwakaribisha watoto wa watumwa kwa shule ya Jumapili. Watoto wengi walifika siku za Jumapili iliyokuwa siku bila kazi kwa watumwa wengi. Hapa Wamoravian hawakuwafunza dini pekee bali walitoa pia kozi a kusoma na kuandika kwa wale waliotaka. Idadi kubwa ya watoto waliotafuta elimu ilileta uhaba wa walimu na hapo wamisionari Wamoravian walianza mapema kuwaandaa Wakristo wao wenye asili ya Kiafrika kuwafundisha watoto kama walimu. 1840 waliendelea kuanzisha chuo cha ualimu cha kwanza mjini Fairfield. Mnamo katikati ya karne ya 19 waliendesha shule 43 walipofundisha wavulana 1728 na wasichana 1280.
Tangu mwisho wa karne ya 19 Wajamaika wazalendo walipokelewa katika nafasi za uongozi kama wasimamizi wa makanisa na wachungaji. Askofu wa kwanza mzalendo alikuwa S. U. Hastings aliyebarikiwa 1961.
Mchungaji Mjamika Dr. Gardner alichaguliwa mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Duniani mwaka 2008.
Mikoa na utawala
[hariri | hariri chanzo]Jimbo la Jamaika limegawiwa kwa mikoa 4 na kila mmoja husimamiwa na mchungaji mkuu wa mkoa (superintendent). Kila mkuu wa mkoa huketi pia kwenye kamati kuu ya jimbo yenye wajumbe 7 pamoja na walei 2 na mwenyekiti wa jimbo. Kwa jumla kuna wachungaji 38; 33 huhudumia Jamaika, 3 Kuba na 2 Cayman.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- The Moravian Church in Jamaica and the Cayman Islands Archived 5 Julai 2008 at the Wayback Machine.. Tovuti rasmi
- Moravian Church Contributing Much to Education Archived 22 Julai 2011 at the Wayback Machine. (Jamaica Information Service 12.12.2004, iliangaliwa 13.05.2011)
- The Moravians in Jamaica: The First Hundred Years (African Cariibean Homepage, iliangaliwa 13.05.2011)
- HISTORY OF THE MORAVIAN MISSIONS IN JAMAICA (Jamaican Family Search Genealogy Research Library, iliangaliwa 13.05.2011)