Nenda kwa yaliyomo

Kamwangi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Kamwangi is located in Kenya
Kamwangi

Inakopatika Kamwangi

Majiranukta: 0°57′S 36°54′E / 0.95°S 36.9°E / -0.95; 36.9
Nchi Kenya
Mkoa Kaunti ya Kiambu
EAT (UTC+3)

Kamwangi ni mji mdogo katika barabara ya Thika - Naivasha. Inapatikana magharibi ya mji wa Thika. Vilevile, kuna barabara inayounganisha mji huu na Gatundu kupitia Kang'oo.

Shughuli kuu inayofanyika hapa ni biashara. Kuna soko kubwa la Jumanne na Ijumaa kila wiki. Maduka makubwa pia yanawavuta wateja kutoka katika vijiji vilivyoko karibu. Mji huu unakosa mashirika ya kifedha isipokuwa Tai Sacco iliyoko katika barabara Gatundu. Kuna vituo viwili vya mafuta.

Mji huu una ofisi za Eneo-bunge la Gatundu Kaskazini na tarafa ya Kamwangi. Ofisi za Dioo zinapatikana yapita kilomita mbili kutoka mji mkuu. Kwa sasa mji huu uko katika eneo-bunge la Gatundu Kaskazini linalowakilishwa na Mheshimiwa Clement Kung'u Waibara, aliyeng'atua Patrick Kariuki Muiruri katika uchaguzi mkuu wa 2007.

Mji huu unapatikana kwenye barabara ya Thika - Naivasha, kwa hivyo unaunganishwa na mji mingine kwa kutumia matatu (daladala). Bodaboda (pikipiki) ziko kwa wingi kuwaabirisha watu hadi vijijini. Vilevile kuna posta inayoitwa Kanjuku, ingawa Kanjuku ni mji mwingine mdogo karibu na Kamwangi.

Watu wengi Kamwangi ni Wakikuyu. Pia hakukosi wawili watatu kutoka makabila mengine. Wengi pia ni Wakristo. Makanisa yalioko ni kama Katoliki, Restoration, CLFF, n.k. Wengi wakazi katika mji huu ni wapangaji.

Hakuna hospitali ya umma isipokuwa kliniki za binafsi. Wenyeji huenda hospitali ya Gatundu, Igegania au Gakoe.

Shule za binafsi pia zinapatikana kama Wise Shepherd na Good Luck.