Nenda kwa yaliyomo

James Joyce

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu ya James Joyce mjini Dublin

James Augustine Aloysius Joyce (2 Februari 1882 - 13 Januari 1941) alikuwa mwandishi na mshairi kutoka nchini Ueire.

Amejulikana hasa kwa riwaya zake za Ulysses (1922) na Finnegans Wake (1939) pamoja na hadithi fupi za "Dubliners" (1914).

Dubliners, 1914

Joyce alikuwa mwenyeji wa mji wa Dublin. Hata kama sehemu kubwa ya maisha yake aliishi nje ya Ueire mji huu wa nyumbani uliendelea kuwa mahali pa masimulizi yake na watu wa Dublin ni watu amabo maisha yao huonekana katika maandishi ya James Joyce.

James alizaliwa 1882 kama mtoto wa kwanza kati 10 katika familia ya Waeire wakatoliki. Wazazi walimtuma kwenye shule za kikanisa kwa nia ya kumfanya padre wa kanisa katoliki lakini James alijitenga na kanisa alipofikia umri wa miaka 16.

Baada ya masomo ya kwanza kwenye chuo kikuu cha Dublin aliendelea huko Paris (Ufaransa) alipojiandikisha 1902 kama mwanafunzi wa tiba na sayansi. Mwaka uliofuata akarudi Dublin bila kumaliza masomo akajipatia maisha kama mwalimu wa nyumbani.

1904 alikutana na Nora Barnacle aliyeendelea kuwa mke wake akazaa naye watoto wawili; walioa rasmi baadaye 1931. James na Norma waliondoka katika Ueire wakaendelea kuishi Pula, Trieste, Zürich, Paris na London. Joyce alifanya kazi mbalimbali kama mwandishi wa magazeti au mwalimu wa lugha.

1907 alitoa kitabu chake cha kwanza kilikuwa mkusanyiko wa mashairi ulioitwa "Chamber Music".

Riwaya yake mashuhuri "Ulysses" ilianza kuchapishwa kisehemu katika gazeti „The Little Review“ kwenye miaka ya 1918–1920 ikatolewa kama kitabu 1922 mjini Paris. Mwanzoni kilisambazwa kwa matatizo kwa sababu lugha yake inajadili waziwazi habari za mapenzi na kitabu kilipigwa marufuku Uingereza na Marekani kwa miaka kadhaa. Hata hivyo kiliendelea kuonyesha athira kubwa juu ya fasihi ya Kiingereza kikatafsiriwa pia kwa lugha 30.

Kwa jumla Joyce hakuandika mengi. Maisha yake yote alipambana na matatizo ya kifedha akategemea mara kwa mara usaidizi wa marafiki. Alikuwa na ugonjwa wa macho uliomfanya kuwa karibu kipofu miaka ya mwisho wa maisha yake. Aliaga dunia mjini Zürich.

Makala hii kuhusu mwandishi fulani wa Ulaya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu James Joyce kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.