Nenda kwa yaliyomo

FORD-People

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

FORD-People (pia: FORD-P) ni chama cha kisiasa nchini Kenya. Kwa Kiingereza ni Forum for the Restoration of Democracy for the People. Chama hiki ilianzishwa mwaka wa 1997 baada ya farakano la chama cha FORD-Asili.

Chanzo katika FORD-Asili[hariri | hariri chanzo]

Chama cha Forum for the Restoration of Democracy (FORD) ndicho kilikuwa chama cha kwanza kujihusisha na harakati na mambo ya kisiasa tangu mwaka wa 1991, kwa kupigania kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi na demokrasia kutoka kwa mfumo wa chama kimoja na utawala wa KANU nchini Kenya. Rais Daniel arap Moi alishinikizwa na jamii ya kimataifa kuidhinisha mfumo wa vyama vingi kwa kubadilisha sehemu 2A ya katiba ya Kenya, iliyozuia kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa.

Kabla ya uchaguzi wa 1992 FORD ilifarakana kati ya wafuasi wa viongozi Kenneth Matiba kutoka Mkoa wa Kati na Martin Shikuku kutoka Mkoa wa Magharibi kwa upande mmoja na kwa upande mwingine Jaramogi Oginga Odinga kutoka Mkoa wa Nyanza. Wafuasi wa Odinga waliunda FORD-Kenya. Wafuasi wa Matiba waliendelea kwa jina la FORD-Asili.

Baada ya uchaguzi wa mwaka wa 1992, Matiba aliibuka wa pili baada ya Rais Moi, hivyo basi kuunda chama cha upinzani bungeni.

Kuundwa kwa Ford-P kutokana na farakano Matiba-Shikuku[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 1997 faragano lilitokea katika chama cha FORD-Asili kati ya mwenyekiti Kenneth Matiba na Martin Shikuku aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama. Shikuku aliyekuwa na wafuasi wengi aliendelea kushikilia hatamu za ofisi ya chama. Nyumba ya ofisi ilikuwa mali ya Matiba aliyetimuliwa ofisi ya chama chake. Lakini Shikuku alienda akishika hati ya kusajiliwa kwa chama.

Upande wa kundi la Matiba, mwanasiasa Kimani wa Nyoike alikuwa Katibu Mkuu. Bila mawasiliano na Matibawa Nyoike aliandikisha chama kipya kwa jina la Ford-People kwa sababu aliogopa kubaki bila chama iwapo Shikuku angefaulu kutetea haki ya kumiliki jina la Ford-Asili. Matiba alikata tamaa kuhusu hali ya siasa na akajiondoa katika shughuli zote za kisiasa nchini Kenya. Hivyo wa Nyoike alibaki na chama alichokuwa akiandaa kwa upande wa Matiba lakini bila kiongozi huyu.[1]

Uchaguzi wa 1997[hariri | hariri chanzo]

Wanasiasa wengi wa kundi la Matiba hawakumfuata wa Nyoike katika Ford-People bali walijiunga na vyama vingine. Chama hiki kilipata viti vitatu bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka wa 1997. Wa Nyoike hakufaulu kuingia bungeni. FORD-P kilitokea kama chama kidogo chenye mizizi na ushawishi mwingi kutoka Mkoa wa Kati.

Uchaguzi wa 2002[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2002 wa Nyoike alifaulu kupatana na mwanasiasa Simeon Nyachae aliyewahi kujiuzulu kutoka kwa chama cha KANU mwaka wa 1999. Nyachae hakujiunga na umoja wa upinzani ulioanzishwa chini ya NAK na baadaye ukajulikana kama Rainbow Coalition.

Katika uchaguzi huo,Nyachae aliibuka wa tatu katika kura ya urais na FORD-People ilifaulu kuchukua viti vyote vya Kisii na kuingia bungeni likiwa na kundi la wabunge 14 hivyo kuwa chama cha tatu baada ya NARC na KANU.

Ushirikiano na Kibaki[hariri | hariri chanzo]

Kati ya 2003/2004 mafarakano katika serikali ya NARC yalionekana kabisa hivyo wabunge wa FORD-People walitafutwa na serikali kwa kura zao. Katika mabadiliko ya serikali ya mwaka wa 2004 Nyachae aliteuliwa Waziri wa Nishati na chama chake kikaingia katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Uchaguzi wa 2007[hariri | hariri chanzo]

Katika uchaguzi huu wimbi wa chama cha ODM uliovuma katika sehemu nyingi nchini, ulikifanya chama cha Ford-People kupoteza viti 11 vya ubunge kikiwemo kile cha Simeon Nyachae.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Will Nyoike sell Nyachae? - taarifa ya "Nation" 13-05-2002 ilisomwa tar. 5.01-2008