El Ninyo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

El Ninyo (kutoka Kihispania El Niño tamka "ninyo"), pia El Nino ni tukio la halihewa linalotokea kwenye nusutufe ya kusini ya dunia kila baada ya miaka kadhaa. Dalili za El Ninyo ni kuongezeka kwa mvua kushinda hali ya kawaida.

El Ninyo ni tukio la eneo la Bahari Pasifiki lakini athari zake zinaweza kugusa maeneo mengine na pia Afrika ya Mashariki iliwahi kuona mvua mkali kutokana na El Ninyo.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina El Ninyo kwa Kihispania lamaanisha "mtoto" kwa maana "mtoto Yesu" kwa sababu hutokea wakati wa Krismasi yaani sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu. Jina lilibuniwa na wavuvi wa Peru walioona uhaba wa samaki baharini wakati wa tukio hili.

Jina kamili la kitaalamu ni "El Ninyo-mbembeo wa kusini" (El Niño-Southern Oscillation (ENSO)).

Sababu[hariri | hariri chanzo]

El Ninyo hutokea kama halijoto ya maji kwenye uso wa bahari ya Pasifiki inapanda juu ya kiwango cha kawaida. Mkondo wa maji ya vuguvugu unatokea kila mwaka mnamo wakati wa Krismasi kwenye pwani la Ecuador na Peru na kwa kawaida hudumu wiki chache. Lakini kila baada ya miaka 2-5 unaendelea kwa miezi kadhaa.

Kuwepo kwa maji ya vuguvugu kunaongeza mvuke hewani ambayo ni msingi wa kuongezeka kwa mvua katika maeneo fulani pamoja na ukame usio kawaida katika sehemu nyingine. Australia na Asia ya Kusini Magharibi huwezi kuona ukame lakini jangwa la Peru kuona mvua nyingi. Katika Afrika ya Mashariki yote miwili inaweza kutokea ama ukame au mvua nyingi. Mabadiliko haya yanaathiri kilimo.