Christus Dominus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Christus Dominus ni maneno mawili ya kwanza ya hati iliyotolewa kwa Kilatini na Mtaguso wa pili wa Vatikano kuhusu kazi ya maaskofu. Maneno hayo yana maana ya "Kristo Bwana".

Hati hiyo ilitolewa tarehe 28 Oktoba 1965 kwa kura 2319 dhidi ya 2 tu.

Baada ya kufundisha juu ya daraja ya uaskofu katika hati "Lumen Gentium" mtaguso mkuu ulitunga hati hii kuhusu kazi ya maaskofu katika ngazi tatu:

  • ngazi ya kanisa katoliki duniani
  • ngazi ya jimbo (dayosisi)
  • uhusiano kati ya maaskofu wa majimbo jirani (kanda na nchi)

Kwanza kila askofu atazamiwa kuwa kiungo cha kundi la maaskofu ambalo linaongozwa na askofu wa Roma na kuwajibika kulichunga Kanisa zima. Wajibu huo unatimizwa kwa kushiriki katika mtaguso mkuu, ambako ni haki ya maaskofu wote, kuchangia muundo mpya wa sinodi ya maaskofu, kushughulikia kwa hali na mali misheni na majimbo yasiyo na mapadri au mali za kutosha, kuwaombea maaskofu wafungwa na wanaodhulumiwa, kuchangia katika ofisi za papa.

Pili, ni wajibu wa baadhi ya maaskofu kuchunga kwa jina la Bwana sehemu fulani ya taifa la Mungu wakitimiza kazi za kufundisha, kutakasa na kuongoza kama wachungaji halisi, ingawa wanapaswa kuheshimu mamlaka ya papa, patriarki na maaskofu wakuu. Chini ya askofu wake jimbo ni Kanisa maalumu ambamo Kanisa pekee linaishi na kutenda. Hati hiyo inaelekeza namna ya kutimiza wajibu huo (pamoja na kuagiza utungwe mwongozo maalumu ambao ufafanue zaidi), inaagiza mipaka ya majimbo irekebishwe yasiwe makubwa mno wala madogo mno, na inaratibu uhusiano na maaskofu waandamizi na wasaidizi, nafasi ya makamu na halmashauri za askofu, uhusiano na maparoko na mapadri wengine. Suala lingine gumu ni uhusiano na watawa hasa walio mapadri, ambao wamehimizwa sana kuishi kweli kama viungo vya jimbo na kujihusisha na maendeleo yake ya Kiroho na ya kitume kwa kushirikiana na askofu, mapadri na walei pamoja na watawa wengine. Pia maaskofu wazee au wenye shida nyingine wanahimizwa kujiuzulu.

Tatu, maaskofu wanahimizwa kuchangia ustawi wa Kanisa katika maeneo yao kupitia sinodi, mtaguso wa kanda au wa nchi, baraza la maaskofu, ushirikiano katika kanda, pia na maaskofu waliopewa kazi tofauti na jimbo (k.mf. uchungaji wa askari wote wa nchi yao). Maagizo yote ya hati hiyo yalikusudiwa kuongoza marekebisho ya sheria za Kanisa.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]