Mnyamawamtuka moyowamkia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Dinosauri
Umbo la Sauropoda, pamoja na Mnyamawamtuka
Umbo la Sauropoda, pamoja na Mnyamawamtuka
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Sauropsida (Wanyama wanaofanana na watambaazi)
Nusungeli: Diapsida (Wanyama wenya mashimo mawili kando la fuyu la kichwa)
Oda ya juu: Dinosauria (Wanyama kama dinosauri)
Oda ya chini: †Sauropodomorpha
Familia ya juu: †Sauropoda
Familia: †Titanosauria
Nusufamilia: †Lithostrotia
Jenasi: †Mnyamawamtuka

Gorscak and O'Connor, 2019

Mnyamawamtuka moyowamkia ni aina ya dinosauri ambaye visukuku vyake viligunduliwa kuanzia mwaka 2004 katika bonde la mto Mtuka upande wa kusini wa Ziwa Rukwa, karibu na kata ya Galula nchini Tanzania.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la Mnyamawamtuka linarejelea mahali ambako mifupa yake iligunduliwa yaani bonde la mto Mtuka. Sehemu ya pili ya jina „mkiawamoyo“ imechaguliwa kutokana na umbo la mifupa ya mkia wake inayofanana na moyo.

Mnyamawamtuka m. ni kati ya aina chache za dinosauri zenye majina ya Kiswahili, pamoja na jenasi ya Shingopana.

Tabia[hariri | hariri chanzo]

Tabia kadhaa ya mnyama huyo zinaonekana kutokana na mifupa yake yaliyopatikana kama visukuku. Mwili wake ulifanana kiasi na mjusi lakini alikuwa mkubwa sana, akiwa na kiwiliwili kikubwa, shingo ndefu, kichwa kidogo na mkia mrefu. Titanosauri walikula majani.

Mnyama aliyepatikana kwenye mto Mtuka alikuwa kijana bado ambaye hakufikia vipimo vya mkubwa. Alikuwa na uzito wa takriban tani 1.5, urefu wa mita 1.5 kiunoni na urefu wa mita 7.6 kuanzia kichwani hadi mwisho wa mkia wake. [1]

Ugunduzi[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 2004 visukuku vya mifupa mikubwa viligunduliwa kwenye mtelemko mkali wa korongo la mto Mtuka. Ilionekana haraka mifupa ilikuwa ya aina ya dinosauri. Ugumu wa kufika kwenye mabaki hayo uliwalazimisha wagunduzi kuendelea na kazi hii miaka kadhaa. Uchimbaji uliongozwa na wataalamu wa Chuo kikuu cha Ohio wakishirikiana na wenyeji wa Tanzania.

Tangu mwaka 2009 sehemu kubwa ya kiunzi cha mifupa ilipatikana. Utafiti uliofuata ulichukua tena miaka hadi wagunduzi walipoweza kuonyesha matokeo yake mwaka 2019.

Uainishaji[hariri | hariri chanzo]

Mnyama huyo aliishi takriban miaka milioni 70-100 iliyopita. Mifupa yake inaonyesha alikuwa mmoja wa Titanosauria, kundi kubwa la Sauropoda waliokuwa na wanyama wakubwa zaidi walioishi kwenye nchi kavu.

Kuna tabia zinazofanana na Malawisauri aliyepatikana kisehemu kwenye Malawi ya kaskazini.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Linganisha makala ya Geggel kwenye livescience.com

Marejeo ya Nje[hariri | hariri chanzo]