Mbu miguu-mirefu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mbu miguu-mirefu
Tipula oleracea
Tipula oleracea
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Diptera (Wadudu wenye mabawa mawili tu)
Nusuoda: Nematocera (Diptera wenye vipapasio kama nyuzi)
Familia ya juu: Tipuloidea
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Familia 3:

Mbu miguu-mirefu (kutoka kwa Kiholanzi langpootmuggen) ni mbu wakubwa wa familia ya juu Tipuloidea katika nusuoda Nematocera wa oda Diptera walio na miguu mirefu. Kwa kawaida mabawa, yaliyo marefu pia, huwekwa kwa pembe ya kati ya 45º na 90º kwa mwili wakipumzika, lakini spishi za nusufamilia Limoniinae (Tipulidae) huyaweka pamoja juu ya fumbatio. Wanatokea kwa kawaida mahali pa unyevu mabarani kote isipokuwa Antakitiki.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Nephrotoma appendiculata mwenye rangi kali.
Ctenophora elegans anaiga nyigu.

Mbu miguu-mirefu hufanana na mbu wakubwa sana wenye mwili mwembamba na miguu mirefu sana hadi mara mbili ya urefu wa mwili wao. Wanapochukuliwa miguu huvunjika kwa urahisi (autotomy). Urefu wa mwili kwa kawaida ni sm 1-3.5, lakini wanaweza kuwa wafupi kama mm 7 na warefu kama sm 5. Mabawa ni membamba na marefu, marefu kama au mafupi kidogo kuliko mwili. Kwa hivyo, upana wa mabawa ni sm 1-6.5 na upana mkubwa kabisa wa mabawa ni sm 11[1]. Mabawa ni mangavu yakiwa na mabaka meusi au siyo. Rangi ya mwili mara nyingi huwa kijivu, kahawia au njano ili wasiweze kugunduliwa kwa urahisi na mbuai, haswa ndege. Hata hivyo, kuna spishi zilizo na rangi kali zaidi, kama zile za Nephrotona na Ctenophora, ambazo zile za mwisho huiga nyigu.

Kichwa kidogo kina pua ndefu, ambayo mara nyingi ni ndefu kama kichwa yenyewe au hata kama kichwa na pronoto pamoja. Macho ni madogo na kama shanga. Sehemu za mdomo hupunguzika sana kwa kawaida, ingawa bado zinafanya kazi katika spishi fulani. Vipapasio ni kama nyuzi na zina pingili hadi 19[2].

Mabuu wamerefuka na wana umbo la mcheduara kwa kawaida. Theluthi mbili ya nyuma ya kifuniko cha kichwa kimefungika au kupunguzika ndani ya pingili ya prothoraksi. Kimeimarishika kwa mbele na kukatwa mbele. Mandibulo ni mkabala moja na nyingine na kusogea katika bapa ya usawa au mbetuko. Pingili za mwisho za fumbatio ni laini, mara nyingi zimeimarishika kwa sehemu na kubeba spirakulo nyuma. Kisahani cha spirakulo huzungukwa kwa kawaida na papila au ndewe.

Biolojia[hariri | hariri chanzo]

Mbu miguu-mirefu hukiakia wakati wa usiku, jioni na alfajiri. Wanavutiwa na mwanga. Wakati wa mchana, wanajificha kwenye uoto. Wanaruka vibaya na kwa njia ya zigizaga. Spishi nyingi hazila, lakini wengi hujilisha kidogo kwa mbochi huku wachache wakila wadudu wadogo. Kinyume cha hiyo, mabuu ni walafi sana na wanaweza kula miani, mikroflora na dutu ya mimea inayooza, pamoja na mbao. Wengine ni mbuai[3][4]. Huishi katika udongo, katika mbao zinazooza au ndani ya maji.

Kama waharibifu[hariri | hariri chanzo]

Mbu miguu-mirefu wa vinamasi, Tipula paludosa, na mbu miguu-mirefu wa mboga, T. oleracea, ni wadudu waharibifu wa kilimo huko Ulaya. Spishi nyingine haribifu hutokea sehemu nyingine za dunia. Mabuu ya mbu miguu-mirefu ya umuhimu wa kiuchumi huishi kwenye tabaka za juu za udongo ambapo hujilisha kwa mizizi, nywele za mizizi na pengine majani ya mazao na kudumaza ukuaji wao au kuua mimea hiyo. Ni wadudu waharibifu kwenye bidhaa mbalimbali. Tangu mwishoni mwa miaka ya 1900, T. paludosa na T. oleracea zimekuwa vamizi nchini Marekani[5][6]. Mabuu yameonwa kwenye mazao mengi, pamoja na mboga, matunda, nafaka, malishoni, nyanja za nyasi na mimea ya mapambo. Wanaweza kuharibu sehemu kubwa za nyanja za nyasi, k.m. kwenye vigoe.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Afrolimnophila unijuga
  • Antocha longicornis
  • Antocha multispina
  • Austrolimnophila cladoneura
  • Austrolimnophila diffusa
  • Dicranomyia nairobii
  • Dicranomyia tipulipes
  • Dicranoptyga kenyana
  • Dicranoptyga matengoensis
  • Dolichopeza distigma
  • Elephantomyia satura
  • Erioptera cristata
  • Erioptera euzona
  • Geranomyia alberticola
  • Geranomyia obsolescens
  • Gonomyia flavonotata
  • Helius brevisector
  • Helius capensis
  • Libnotes oresitropha
  • Libnotes rhizosema
  • Limnophila allosoma
  • Limnophila obscura
  • Medleromyia tanzanica
  • Metalimnobia congoensis
  • Metalimnobia zernyana
  • Molophilus africanus
  • Molophilus nannopterus
  • Nephrotoma capensis
  • Nephrotoma elgonica
  • Nephrotoma ruwenzoriana
  • Paradelphomyia ugandae
  • Pilaria morogoroensis
  • Rhipidia afra
  • Styringomyia clandestina
  • Styringomyia vittata
  • Symplecta brevifurcata
  • Tasiocera probosa
  • Tipula elgonensis
  • Tipula flagellicurta
  • Tipula kenia
  • Tipula masai
  • Tipula uluguruensis
  • Trentepohlia curtipennis
  • Trentepohlia msingiensis
  • Trichotrimicra mbeya
  • Trichotrimicra subnuda

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Louise Moon. "'World's biggest' mosquito with 11cm wing span found in southwest China", 25 April 2018. 
  2. Watson, L. and M. J. Dallwitz. 2003 onwards. Tipulidae. Archived 13 Oktoba 2007 at the Wayback Machine. British Insects: The Families of Diptera. Version: 1 January 2012.
  3. Pritchard, G (1983). "Biology of Tipulidae". Annual Review of Entomology 28 (1): 1–22. doi:10.1146/annurev.en.28.010183.000245. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-01-12. Iliwekwa mnamo 2013-10-08.  Unknown parameter |url-status= ignored (help)
  4. Oosterbroek, P. Superfamily Tipuloidea, Family Tipulidae. Chapter 2 In: Evenhuis, N. L. (Ed.) Catalog of the Diptera of the Australasian and Oceanian Regions, Issue 86 of Bernice P. Bishop Museum Special Publication. Apollo Press. 1989.
  5. Rao, Sujaya; Listona, Aaron; Cramptonb, Lora; Takeyasu, Joyce (2006). "Identification of Larvae of Exotic Tipula paludosa (Diptera: Tipulidae) and T. oleracea in North America Using Mitochondrial cytB Sequences". Annals of the Entomological Society of America 99 (1): 33–40. doi:10.1603/0013-8746(2006)099[0033:IOLOET]2.0.CO;2.  Unknown parameter |s2cid= ignored (help)
  6. Blackshaw, R.P.; Coll, C. (1999). "Economically important leatherjackets of grassland and cereals: biology, impact and control". Integrated Pest Management Reviews 4 (2): 145–162. doi:10.1023/A:1009625724013. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-01-15. Iliwekwa mnamo 2019-08-29.  Unknown parameter |url-status= ignored (help); Unknown parameter |s2cid= ignored (help)