Yaa Asantewaa
Yaa Asantewaa | |
Yaa_Asantewaa_Museum_(4) | |
Amezaliwa | 1840 Ashanti |
---|---|
Amekufa | 1923 |
Nchi | Ashanti (leo Ghana) |
Yaa Asantewaa (* 1840; † 1923) alikuwa malkia mama wa Edweso, sehemu ya milki ya Ashanti.
Mnamo mwaka 1900 aliongoza vita ya mwisho ya Waashanti dhidi ya uenezaji wa utawala wa Uingereza kwenye Gold Coast (leo Ghana).
Historia ya awali
[hariri | hariri chanzo]Yaa Asantetwaa alizaliwa mnamo 1840 katika mji wa Besease[1], wakati ule kitovu cha ufalme mdogo ndani ya milki ya Ashanti. Kakaye Afrane Panin aliendelea kuwa Ejisuhene (mtawala) wa Ejisu. Yaa Asantetwaa aliishi maisha ya mkulima akaolewaa akamzaa binti mmoja.[2]
Baada ya kuwa mtawala Afrane Panin alimfanya dada kuwa mama malkia. Afrane Panin alikufa mwaka 1894 na hapo Yaa Asantewaa alitumia nafasi yake ya malkia mama kumteua mjukuu wake kuwa Ejisuhene mpya. Mwaka 1896 Waingereza walishambulia milki ya Ashanti wakaingia Kumasi na kumkamata Asantehene yaani mfalme wa Ashanti aliyetumwa nao ugenini. Alipaswa kukaa Shelisheli mbali na nchi yake. Waingereza walipora dhahabu na sanaa za Kumasi lakini walishindwa kupata kiti cha dhahabu cha kifalme ambacho ni ishara takatifu ya taifa lao kilichofichwa na askari wa Asantehene.
Ejisuhene yaani mjukuu wa Yaa Asantetwaa alikamatwa na kutumwa nje pamoja na Asantehene. Hivyo utawala wa Ejisu ulibaki mkononi mwa malkia mama.
Kiongozi kwenye Vita ya Kiti cha Dhahabu
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1899 gavana Sir Frederick Hodgson wa Gold Coast alifikiri ya kwamba ugumu wa kutawala Waashanti ungepungua kama yeye mwenyewe angeshika kiti cha dhahabu. Wanajeshi aliotuma kukitafuta walishindwa. Hivyo gavana Hodgson mwenyewe alienda Kumasi akaita mkutano wa watawala wa maeneo ya Ashanti akadai kupewa kiti cha dhahabu na malipo ya kodi. Hotuba ya gavana ilikasirisha viongozi lakini waliondoka kimya. Yaa Asantewaa alishiriki na kabla ya mkutano alionekana kumtania gavana kwa kusimama mbele yake na kuangalia nishani kwenye sare yake kwa muda mrefu. Baada ya kusikia madai ya gavana alimpinga kwa kumwambia hastahili kupata kiti cha dhahabu na akikitaka amrudishe Asantehene anayejua kifichio chake.[2]
Walikutana baadaye kati yao wakishauriana namna gani kujibu. Yaa Asantewaa alishiriki katika mkutano huu. Alipoona ya kwamba sehemu ya viongozi walitaka kunyamaza alitoa hotuba akiwauliza wakuu wengine namna gani waliweza kunyamaza tu na kusikiliza kimya maneno ya Mwingereza, na kama wameacha kuwa wanaume au kubadilishwa kuwa wanawake?
Katika mkutano huu Yaa Asantewaa alichaguliwa kuwa kiongozi wa vita wa Ashanti. Mwenyewe au kupitia mwakilishi alisimamia mikutano ya kupanga hatua zilizochaguliwa. Mwenyewe hakushiriki katika mapigano. [3]
Hali halisi ilikuwa nusu tu ya watawala wa kieneo walioshiriki katika vita hii. Jeshi la Ashanti ilikutanana polepole na kuviringisha Waingereza katika boma la Kumasi lakini walikosa silaha za kushambulia boma lenyewe.
Vita iliendelea hadi Julai wakati Waingereza walikusanya jeshi jipya kutoka vikosi vyao vya Sierra Leone na Nigeria na jeshi hili lilifika Kumasi kwenye Julai na kufukuza jeshi la Waashanti. Katika miezi iliyofuata walishinda upinzani wote.
Hatima ya Yaa Asantewaa
[hariri | hariri chanzo]Kuelekea mwisho wa mapigano Yaa Asantewaa pamoja na viongozi wengine alitekwa na Waingereza na kupelekwa nje ya nchi kwenda Shelisheli. Hapo alikufa mwaka 1921. Miaka mitatu baadaye Asantehene aliruhusiwa kurudi Kumasi.
Yaa Asantewaa anakumbukwa hadi leo na picha yake ilionekana kwenye pesa ya cedi 20 ya Ghana baada ya uhuru.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kufuatana na chanzo kingine alizaliwa 1932 huko Ejiasi, linganisha Mensah uk 41
- ↑ Wiafe Mensah, uk. 51
- ↑ Arhin Brempong, The role of Nana Yaa Asantewaa in the 1900 Asante War of Resistance; jarida Le Griot, Vol. VIII, 2000