Nenda kwa yaliyomo

Varus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Varus aliyeshindwa, sanamu ya kisasa, Haltern (Ujerumani)

Publius Quinctilius Varus (* 47/46 KK mjini Cremona (Italia); † 9 BK Germania) alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa kijeshi wa Kiroma.

Alitumiwa na Kaisari Augusto kwa shughuli mbalimbali. 9/8 KK alipewa ugavana wa jimbo la Afrika (Tunisia) . Kati ya 7/6 na 5/4 alikuwa gavana wa Kiroma huko Shamu (Syria) alipokuwa pia mshauri wa mfalme Herode I.

Mnamo 7 hadi 9 BK alipewa ugavana wa jimbo la Germania (leo: Ujerumani). Varus alizunguka pia ng'ambo ya mto Rhein akisindikizwa na legioni zake na kujenga barabara, kutembelea machifu wa Kigermanik na kutoa maazimio katika fitina kati ya makabila ya Kigermanik.

Mwaka 9 aliporudi pamoja na legioni tatu kutoka ziara yake alishambuliwa na jeshi la Wagermanik waliokusanywa na Arminio. Waroma walishambuliwa msituni wakajitetea kwa siku tatu mwishowe walishindwa na kuuawa wote. Varus alijiua mwenyewe alipoona atashindwa.

Augusto alihuzunika kupotea kwa jeshi kubwa. Hii ilikuwa mwisho wa majaribio ya Waroma ya kupanusha utawala wao juu ya Wagermanik upande wa mashariki ya mto Rhein.