Nenda kwa yaliyomo

Sumu kuvu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Sumu kuvu ni sumu zitolewazo na aina ya ukungu kuvu (fangasi) unaoota kwenye mbegu za nafaka jamii ya kunde, mazao ya mizizi, karanga, vyakula na malisho ya wanyama vikiwa shambani au kwenye ghala.

Sumu hizo hazionekani kwa macho, hazina harufu, hazina kionjo wala rangi, lakini kuvu inayotoa sumu hizo inaweza kuwa na rangi ya kijani, chungwa, kijivu au njano na inaweza kutoa harufu ya uvundo [1].

Kuna aina mbalimbali za sumu kuvu ambazo zimegunduliwa, lakini zile ambazo zimeonekana kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mifugo ni aflatoxin, orchratoxin A, patulin, fumonisins, zearalenone na nivalenol/deoxynivalenol [2]

Karibu asilimia 25 ya vyakula ulimwenguni vina maambukizi ya sumu kuvu na watu bilioni 2.5 wako katika hatari ya kudhurika [3]. Kuvu inaotoa sumu hizo hustawi ikiwa mazao yamekumbwa na ukame yakiwa shambani au yameshambuliwa na wadudu waharibifu, na kwenye ghala ikiwa joto na unyevu viko katika kiwango cha juu.[4]

Sumu kuvu huweza kukaa kwenye mchanga na hivyo kuvutwa sawia na rutuba wakati mimea mingine inapopandwa na kuanza kukua. Watu wanaweza kupata sumu kuvu wanapokula mimea iliyoathiriwa na sumu hizo au hata nyama ama bidhaa za maziwa kutoka kwa wanyama waliokula mimea iliyoathiriwa na sumu hizo.[5] Watoto wako katika hatari kubwa ya kupata sumu kuvu, ambayo inahusishwa na ukandamizaji wa Kingamwili, pia kusababisha ukuaji uliodumaa [6]

Athari za sumu kuvu kiafya[hariri | hariri chanzo]

Sumu kuvu aina ya aflatoxin inasababisha ugonjwa wa Aflatxicosis ambao hutegemea wingi wa sumu kuvu kwenye chakula au kinywaji atakachotumia binadamu au mnyama. Binadamu aliyekula cahkula chenye sumu kuvu huonyesha dalili kama maumivu ya tumbo, kutapika, kuvimba tumbo, homa, kuharisha, kuwa wa njano sehemu za mwili (nyayo, viganya vya mikono na miguu), kujaa maji kwenye mapafu na degedege. Uonapo dalili hizo ni vema kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya.[7]

Endapo mtu atakuwa akila chakula kilichoathiriwa na sumu kuvu kwa kipindi kirefu, husababisha madhara ya saratani ya ini, kupungua kwa kingamwili, udumavu kwa watoto na watoto kuzaliwa na mgongo wazi na damu kutokuganda kwa wakati[8].

Kuzuia[hariri | hariri chanzo]

Kupunguza na kuondokana na tatizo la uchafuzi wa sumu kuvu ni jukumu la kila mmoja kwenye mnyororo wa thamani wa chakula yaani, kuanzia shambani hadi mlaji wa mwisho. Hivyo kila mmoja atimize wajibu wake ili kuwa na chakula salama kwa afya bora. Njia kuu ya kudhibiti uchafuzi wa sumu kuvu ni usafi wa chakula.

Ili kuhakikisha sumu hizo haziwaathiri watu, mamlaka husika zimetengeneza viwango vya sumu hizo katika vyakula vinavyovumilika ili kulinda afya ya mlaji. Kwa muujibu wa sheria ya viwango Tanzania (2009) ya shirika la viwango, kiwango cha sumu kuvu ama aflatoxin katika chakula kimewekwa kuwa mls ya 5 ppb kwa aflatoxinB1 na 10 ppb kwa ujumla ya sumu ya aflatoxin katika vyakula kwa matumizi ya binadamu nchini Tanzania.

Pamoja na hayo, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani limeweka pia viwango vya sumu kuvu vinavyovumilika ili kulinda afya ya mlaji [9]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]