Solistasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Solstice)
Tarehe na saa za UTC
za sikusare na solistasi duniani[1][2]
Tukio Sikusare Solistasi Sikusare Solistasi
Mwezi Machi Juni Septemba Disemba
Mwaka
Siku Saa Siku Saa Siku Saa Siku Saa
2018 20 16:15 21 10:07 23 01:54 21 22:23
2019 20 21:58 21 15:54 23 07:50 22 04:19
2020 20 03:50 20 21:44 22 13:31 21 10:02
2021 20 09:37 21 03:32 22 19:21 21 15:59
2022 20 15:33 21 09:14 23 01:04 21 21:48
2023 20 21:24 21 14:58 23 06:50 22 03:27
2024 20 03:07 20 20:51 22 12:44 21 09:20
Mwelekeo wa kituo (mgawanyiko kati ya usiku na mchana) inategemea msimu.

Solistasi (pia:solistisi, kutoka ing. solstice[3]) ni jina la siku mbili katika mwaka ambako tofauti kati ya urefu wa mchana na usiku ni kubwa zaidi kuliko siku zingine. Hutokea mara mbili kwa mwaka.

Tarehe ya kwanza ni 20 au 21 Juni na ya pili ni tarehe 21 au 22 Desemba.

Watu wanaoishi sehemu za jirani na ikweta huwa hawatambui tofauti kati ya muda wa mchana na usiku, ila kadri wanavyoishi mbali zaidi upande wa kusini au kaskazini wa ikweta, tofauti huwa kubwa zaidi.

Kwa kawaida kuna tofauti kati ya urefu wa mchana na usiku isipokuwa kwenye ikweta. Karibu na ncha za Dunia muda wa usiku na mchana unaweza kuwa mrefu hadi karibu nusu mwaka lakini kwa kawaida kuna majira ya mchana mrefu na usiku mrefu zinazobadilishana polepole. Mwendo huu unatokea kinyume kwenye nusutufe mbili za Dunia yaani wakati mchana unarefuka kwenye nusutufe ya kaskazi usiku unarefuka kwenye nusutufe ya kusi.

Katika kanda za karibu na ikweta tofauti hizi hazionekani kirahisi lakini kwenye nusutufe za Dunia upande wa kusini na kaskazini ya ikweta zimetambuliwa tangu karne nyingi na zimekuwa siku muhimu kwa makadirio ya kalenda mbalimbali.

Wakati wa solistasi ya Juni, Jua linafika mahali pa juu zaidi kwenye anga wakati wa adhuhuri kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazi ya Dunia, baadaye inaanza kushuka yaani kuonekana chini zaidi angani wakati wa adhuhuri hadi sikusare ya Septemba. Kwa hiyo njia yake angani ni ndefu na hivyo muda wa mchana ni mrefu. Siku hiyo hiyo ya solistasi ya Juni, Jua linafika mahali pa chini angani pawezekanavyo wakati wa adhuhuri kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia. Hapa njia yake angani ni fupi hivyo muda wa mchana ni mfupi. Kinyume chake muda wa usiku unabadilika kuwa mrefu au mfupi.

Vivyo hivyo wakati wa solistasi ya Desemba Jua linafika mahali pa juu kwenye anga wakati wa adhuhuri kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kusi ya Dunia, baadaye inaanza kushuka yaani kuonekana chini zaidi angani wakati wa adhuhuri hadi sikusare ya Machi. Siku hiyo hiyo, Jua linafika mahali pa chini angani pawezekanavyo wakati wa adhuhuri kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazi ya Dunia.

Marejeo

  1. United States Naval Observatory (January 4, 2018). Earth's Seasons and Apsides: Equinoxes, Solstices, Perihelion, and Aphelion. Jalada kutoka ya awali juu ya 2007-10-13. Iliwekwa mnamo 2017-12-21.
  2. Astro Pixels (February 20, 2018). Solstices and Equinoxes: 2001 to 2100.
  3. Asili ni neno la Kigiriki ἡλιοστάσιον hēliostásion "kusimama kwa Jua")