Nenda kwa yaliyomo

Mzinga wa nyuki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Fremu ya sega ikitolewa nje ya mzinga wa kisasa
Mzinga wa kisasa huwa na fremu za nsega ndani yake


Mzinga wa nyuki ni mahali au nafasi ambako kundi la nyuki inakaa pamoja na sega.

Porini nyuki wanatafuta tu shimo lolote au pango na kujenga sega ndani yake. Baada ya kujua faida za asali watu wameanza kutengeneza mizinga ya nyuki yaani nafasi zinazofaa ili kuvuta nyuki waingie.

Namna ya mzinga wa kidesturi katika Afrika ni nusu mbili za kipande cha mgogo kombe zinazofungwa kwa kamba na kuacha nafasi katikati. Nyuki wanaotafuta nafasi wanapenda kuingia na kuanzisha kundi jipya mle.

Tatizo ni mavuno ya asali maana yake ni lazima kufungua mzinga wote na tokeo lake pamoja na mavuno mara nyingi ni kuharibu kundi la nyuki ndani ya mzinga hasa kwa sababu malkia anauawa.

Mizinga ya kisasa inaepukana na tatizo hili kwa muundo tofauti wa mzinga.

Mzinga huwa sanduku lenye fremu kadhaa ndani yake. Nyuki hutumia fremu kujenga sega ndani ya fremu. Wakati wowote fremu inaweza kutolewa katika mzinga na kuangaliwa, kutolewa asali na kurudishwa bila kuua nyuki.