Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha ya mji wa Tehran
Picha ya mji wa Tehran.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran [1] Archived 15 Februari 2006 at the Wayback Machine. ni huduma ya matangazo ya "Islamic Republic of Iran Broadcasting" (IRIB) ambayo ni redio ya taifa ya Iran (Uajemi) kwa lugha ya Kiswahili.

IRIB inarusha matangazo kwa lugha mbalimbali kama vile Kirusi, Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa Kichina na mengine.

Kwa lugha ya Kiswahili ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza siku ya Ijumaa usiku ya tarehe 30 Desemba mwaka 1994.

Kwa wakati huo matangazo ya Radio Tehran yaliyokuwa yakirushwa kwa ajili ya nchi za mashariki na katikati mwa Afrika, yalianza yakiwa na wafanyakazi wachache ambao ni Sayyid Muhammad Ridha Shushtari, Sayyid Hashim Shushtari ambaye kwa sasa ni marehemu, Muhammad Baraza, Leyla Kimani, Abdul Fatah Mussa, Ahmed Rashid, Nargis Jalalakhan na Said Kambi. Watangazaji wengine wa idhaa hii ni Asmahan Ghanima Mohammad, Salum Bendera, Mubarak Henia, Sudi Ja'afar Shaban na Hussein Hassan Kamau. Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi waliodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo.

Kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka 1997 Radio Tehran ilianza kutangaza kwa muda wa saa moja kuanzia saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki, na matangazo hayo kurejewa siku ya pili yake kuanzia saa 12:30 asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki sawa na saa 11:30 asubuhi kwa majira ya Afrika ya Kati.

Mnamo tarehe 23 Mfunguo Tatu (Dhulhijja) 1418 Hijria iliyosadifiana na tarehe 21 Aprili 1998 Milaadia, matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa hewani kwa muda wa masaa matatu katika nyakati za usiku, asubuhi na machana. Saa moja ilikuwa ni marudio ya matangazo ya asubuhi, ambayo yalikuwa yakisikika kuanzia saa saba kamili hadi saa nane kamili mchana kila siku kwa majira ya Afrika Mashariki.

Kwa hivi sasa Idhaa imeongeza wafanyakazi wake ambapo matangazo ya mchana nayo sasa yanasikika kwa njia ya moja kwa moja kuanzia saa 5:30 hadi 6:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki. Inarusha matangazo yake kwa ajili ya nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, mashariki mwa Zambia, kaskazini mwa Malawi na Msumbiji pamoja na Afrika Kusini. Inarusha pia matangazo yake kwa ajili ya nchi za Mashariki ya Kati hususan za Ghuba ya Uajemi na ina waandishi wake katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati kama vile Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Kongo.

Matangazo ya IRIB yanalenga kusambaza habari juu ya Iran na utamaduni wake. Yanalenga kusambaza mitazamo ya Kiislamu na mafundisho ya Ahlul Baiti (as) inayolingana na siasa ya Iran. Matangazo ya IRIB pia yananawabaishia Walimwengu ubeberu wa Marekani na madola ya Kimagharibi dhidi ya mataifa mengine na ukandamizaji wa utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]