Angela Atim Lakor

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Angela Atim Lakor

Angela Atim Lakor
Amezaliwa 1982
Uganda
Nchi Uganda
Kazi yake Mwanaharakati


Angela Atim Lakor (alizaliwa 1982) ni mwanaharakati nchini Uganda ambaye ni mwanzilishi mmojawapo wa shirika la "Watye Ki Gen" (Tuna Tumaini) linalolenga kusaidia wanawake waliowahi kutekwa nyara na kundi la Lord's Resistance Army (LRA). Shirika hilo linawasaidia watoto wa wanawake hao kusoma na kusaidia familia kukabiliana na unyanyapaa kutokana na historia yao na LRA.

Historia na elimu[hariri | hariri chanzo]

Lakor alizaliwa katika kaskazini ya Uganda mwaka 1982. Mnamo Oktoba 1996, akiwa na umri wa miaka 14 na mwanafunzi wa shule ya mabweni huko Aboke, wanamigambo wa LRA walishambulia shule hiyo na kuwateka nyara wasichana 139. Naibu mkuu wa shule hiyo aliwafuata akafaulu kurudisha wasichana 109. Wasichana 30 walipaswa kubaki kwa LRA na Lakor alikuwa mmoja wao.[1]

Mfungwa[hariri | hariri chanzo]

Wakiwa wafungwa Lakor na wenzake walipaswa kufuata wanamigambo kwenda Sudan. Alikuwa "ameolewa" na mmoja wa makamanda wa LRA na aliteseka sana kimwili, kisaikolojia akabakwa kwa miaka mingi. Alizaa watoto wa wabakaji wake wakiwa huko. Kwenye nafasi ya mapigano kati ya kikosi cha LRA na jeshi la Sudan aliweza kukimbia upande wa Wasudan.[2]

Kazi baada ya utumwa[hariri | hariri chanzo]

Lakor alirudi Uganda alipopata msaada kwenye kituo cha World Vision mjini Gulu. Baadaye alishiriki kuanzisha shirika la Watye Ki Gen inayolenga kusaidia wenzake wa kike kurudi na kujiunga tena na jamii.

Mwezi Juni 2014, Angela alizungumza na wakuu wa Umoja wa Mataifa na kwa viongozi wa serikali kutoka nchi 140 katika "Mkutano wa Kimataifa wa Kumaliza Ukatili wa Kijinsia katika Migogoro", uliofanyika jijini London na mwenyekiti wa William Hague na Angelina Jolie.

Juhudi zake zilitambuliwa alipoalikwa mwaka 2017 kwenda Uingereza alipopokea tuzo la Marsh Award linalotolewa na Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ya Uingereza. Tuzo hilo la Marsh huwasilishwa kwa watu kwa mchango mkubwa katika kutengeneza amani na kulinda amani.[3]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. https://www.hrw.org/news/2016/10/07/remembering-wisdom-ugandas-aboke-girls-20-years-later Remembering the Wisdom of Uganda’s Aboke Girls, 20 Years Later, Tovuti ya Human Rights Watch ya 7 Oktoba 2016, iliangaliwa Aprili 2023
  2. https://www.itv.com/news/2014-06-10/sexual-violence-survivor-speaks-of-hope-for-other-victims-at-start-of-summit Sexual violence in war survivor hopes summit will help other victims, Tovuti ya itv.com ya 10 Juni 2014, iliangaliwa Aprili 2023
  3. https://www.christiantoday.com/article/former.child.soldier.in.lords.resistance.army.receives.peace.award/117584.htm Former child soldier in Lord's Resistance Army receives peace award, Tovuti ya Christiantoday.com ya 02 Novemba 2017, iliangaliwa Aprili 2023
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Angela Atim Lakor kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.