Amina (malkia wa Zazzau)
Amina, anayejulikana pia kama Aminatu (alifariki mwaka 1610), alikuwa mtu wa kabila la Kihausa. Anatajwa kama kiongozi wa kihistoria wa watu wa Kihausa wa Zazzau, eneo linalojulikana leo kama mji wa Zaria katika Jimbo la Kaduna, kaskazini-magharibi mwa Nigeria.[1]
Inaaminika kuwa alitawala katika karne ya 16. Hata hivyo, uwepo wake bado ni wa mjadala miongoni mwa wanahistoria. Baadhi yao wamehoji usahihi wa simulizi zinazomhusu, kwani hadithi za maisha yake zimechanganyika na masimulizi ya baadaye na ya mdomo.
Maisha ya awali
[hariri | hariri chanzo]Amina alizaliwa katikati ya karne ya 16 BK kwa Mfalme Nikatau, mtawala wa 22 wa Zazzau, na Malkia Bakwa Turunku (takriban 1536–1566).[2] Amina alikuwa na dada mdogo aliyeitwa Zaria, ambaye jina lake linahusiana na mji wa kisasa wa Zaria (Jimbo la Kaduna), uliobadilishwa jina na Waingereza mapema karne ya ishirini.[2][3] Kulingana na hadithi za mdomo zilizokusanywa na mwanahistoria wa utamaduni David E. Jones, Amina alilelewa katika mahakama ya babu yake na alipendwa naye sana. Babu yake alimfundisha kwa uangalifu kuhusu masuala ya kisiasa na kijeshi, huku akimtembeza mahakamani.[4]
Akiwa na umri wa miaka kumi na sita, Amina alipewa cheo cha Magajiya (mrithi wa kiti), na kupewa watumwa wa kike arobaini (kuyanga).[3] Tangu utotoni, Amina alikuwa na wachumba kadhaa waliotaka kumuoa. Jaribio la kupata mkono wake lilijumuisha kutoa watumwa kumi kila siku kutoka kwa Makama na watumwa wa kiume hamsini na watumwa wa kike hamsini pamoja na mifuko hamsini ya kitambaa cha rangi nyeupe na buluu kutoka kwa Sarkin Kano.[3]
Baada ya kifo cha wazazi wake mwaka 1566 au karibu na hapo, ndugu yake Amina akawa mfalme wa Zazzau. Wakati huo, Amina alikuwa amejitokeza kama mwanajeshi mkuu katika kikosi cha farasi cha nduguye na akawa maarufu kwa ujuzi wake wa kijeshi.[2] Leo hii bado anasherehekewa katika nyimbo za sifa za jadi za Hausa kama Amina binti wa Nikatau, mwanamke mwenye uwezo kama mwanaume aliyeweza kuongoza wanaume katika vita.[2]
Ushiriki wa malkia na upanuzi wa Zazzau
[hariri | hariri chanzo]
Baada ya kifo cha kaka yake Karami mwaka 1576, Amina alipanda kiti cha ufalme kama malkia.[3] Zazzau ilikuwa mojawapo ya Falme za Hausa saba za awali (Hausa Bakwai), nyingine zikiwa Daura, Kano, Gobir, Katsina, Rano, na Garun Gabas.[3][5] Kabla ya kuchukua kiti cha enzi, Zazzau ilikuwa mojawapo ya falme kubwa zaidi na pia chanzo kikuu cha watumwa waliokuwa sehemu ya biashara ya watumwa katika masoko ya Kano na Katsina pamoja na wafanyabiashara Waarabu.[6]
Miezi mitatu tu baada ya kutawazwa malkia, Amina alizindua kampeni ya miaka 34 dhidi ya majirani zake, ili kupanua eneo la Zazzau.[3][4][5] Jeshi lake, lenye askari 20,000 wa miguu na askari 1,000 wa farasi, lilikuwa limepata mafunzo mazuri na lilionekana la kutisha.[4] Moja ya tangazo lake la kwanza kwa watu wake lilikuwa wito wa kuwaambia wakaliishe silaha zao upya.[4] Aliteka ardhi kubwa hadi kufika Kwararafa na Nupe.[3]
Hadithi zilizotajwa na Sidney John Hogben zinasema kwamba alipata mpenzi mpya katika kila mji alikopita, na kila mmoja alikutana na hatima ileile ya kusikitisha asubuhi: mpenzi wake wa muda mfupi alikatwa kichwa ili hakuna aweze kuishi kusimulia hadithi hiyo.[3] Chini ya Amina, Zazzau ilidhibiti ardhi zaidi kuliko hapo awali. Ili kulinda ardhi hiyo, Amina alizungusha miji yake kwa kuta za udongo, ambazo zilibaki hadi ukoloni wa Uingereza mnamo mwaka 1904. Baadhi bado zipo na zinajulikana kama ganuwar Amina (kuta za Amina).[3]
Kifo
[hariri | hariri chanzo]Mazingira halisi ya kifo cha Amina hayajulikani kwa uhakika. Mwanazuoni wa Kiislamu wa karne ya 19, Dan Tafa, anaeleza kuwa alifariki katika eneo lililoitwa Attaagar. Wakati huo, eneo hilo lilikuwa sehemu ya ufalme wa Zazzau, uliotajwa kuwa miongoni mwa falme kubwa za Kihausa, huku Bauchi ikijumuisha maeneo mengi.
Kwa mujibu wa taarifa za Tafa, Sidney John Hogben anaripoti kuwa Amina alifariki Atagara, karibu na Idah ya leo, akieleza kuwa wakati huo alikuwa amesogeza mipaka ya Zazzau hadi kusini mwa mto Niger-Benue.[7]
Hata hivyo, bado kuna utata mkubwa kuhusu mahali halisi alipofariki. Baadhi ya waandishi wamedai alikufa Vom Jos, huku wengine wakisisitiza kuwa alifariki Atagara (Idah ya leo).[3]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ [https://www.pbs.org/wgbh/globalconnections/mideast/questions/women/ PBS.org - Global Connections: Roles of Muslim Women]
- 1 2 3 4 Smith, Bonnie G. (2008). The Oxford Encyclopedia of Women in World History (kwa Kiingereza). Oxford University Press. ISBN 9780195148909.
{{cite book}}: line feed character in|title=at position 4 (help) - 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 Hogben, S.J. (1966). Emirates of Northern Nigeria. London: Oxford
University Press. ku. [https://archive.org/details/emiratesofnorthe0000ahmk/page/215
215]–255.
{{cite book}}: line feed character in|pages=at position 63 (help); line feed character in|publisher=at position 7 (help) - 1 2 3 4 Women in world history : a biographical encyclopedia. Commire, Anne., Klezmer, Deborah. Waterford, CT: Yorkin
Publications. 1999–2002. ISBN 078763736X. OCLC 41108563.
{{cite book}}: line feed character in|publisher=at position 7 (help)CS1 maint: others (link) - 1 2 Jones, David
E (2000). Women Warriors: A History. Brassey's. uk. [https://archive.org/details/womenwarriorshis0000jone_t6i4/page/84
84]. ISBN 1-57488-206-6.
{{cite book}}: line feed character in|first=at position 6 (help); line feed character in|page=at position 67 (help) - ↑ Crowder, Michael. (1978). The story of Nigeria (tol. la 1st publ. in this non-net). London: Faber and Faber. ISBN 0571112102. OCLC 178813654.
- ↑ Tafa, Dan. Rawdat al-Afkaar (PDF). Timbuktu, Mali: Sankore Institute.
{{cite book}}: line feed character in|title=at position 7 (help)
| Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Amina (malkia wa Zazzau) kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |